01 August 2011

Chadema yamshukia

Frederick Werema

Ni kuhusu sheria ya kuzuia maandamano

Aneth Kagenda na Tumaini Makene

BARAZA la Vijana wa CHADEMA (BAVICHA) limemshukia Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Jaji Fredrick Werema, likihoji uwezo wake wa kushikilia nafasi hiyo, baada ya kutoa kauli kuwa itungwe sheria ya kudhibiti maandamano.


Akizungumza na waandishi wa habari Dar es Salaam jana, Mwenyekiti wa BAVICHA Taifa, Bw. John Heche alisema kuwa hawatakubaliana na tabia ya serikali, kutunga sheria kwa manufaa ya kisiasa ya chama kilichoko madarakani, zikiwa na nia ya kudhibiti watu au kundi fulani.

Akidai kuwa ana wasiwasi na uwezo wa Jaji Werema katika kufanyia kazi vitu alivyovisomea, aliongeza kusema kuwa kauli hiyo ya Jaji Werema inakwenda kinyume na matamko kadhaa ambayo Tanzania imetia saini kuyaridhia likiwemo Tamko la Haki za Binadamu, ambalo linaunga mkono maandamano, ikiwa ni njia ya watu kuelezea hisia zao, za kukubali ama kupinga jambo fulani.

Katika kauli hiyo ya Jaji Werema aliyoitoa mwishoni mwa wiki wakati akitoa mchango wake kama ex-official na kunukuliwa na baadhi ya vyombo vya habari, alisema kuwa kuna haja ya kurekebisha sheria ili kudhibiti maandamano katika maeneo ambayo watu si washiriki wa maandamano hayo, akitolea mfano wa nchi ya Ujerumani kuwa ina utaratibu huo.

"Nimesikia hapa kauli mbalimbali zinazohamasisha maandamano na wengine wanasema tutaandamana mpaka kieleweke na wengine wanasema kutoka Mwanza mpaka Dar es Salaam, tunasema ndiyo ni haki ya kisheria, lakini lazima tuzingatie kwamba wapo wasiopenda maandamano haya," alinukuliwa Jaji Werema akisema bungeni Ijumaa.

"Hivi kama CHADEMA wangekuwa kila siku wanaamka na kuandaa mandamano ya kuiunga mkono au kuishangilia CCM na kumsifia Kikwete na serikali yake, Werema angetoa tamko hilo? Na hii inatokana na kauli za wabunge wengi wa CCM na mawaziri ambao katika michango yao mingi wamekuwa wakilaani maandamano ya amani ya CHADEMA.

"Huu umekuwa utaratibu wa CCM. Mwaka 1995 walipoona Mrema anaweza kumshinda Mkapa wakatunga sheria kuondoa ulazima wa mshindi wa urais kupatikana kwa zaidi ya asilimia 50 ya kura, wakaleta simple majority (mwenye kura nyingi kutangazwa rais). Kumbukeni Werema aliwahi kupinga katiba mpya, aliwahi kuandaa muswada wa hovyo. BAVICHA tunasema hili halikubaliki. Tuko tayari kuandamana mpaka uvunguni mwa Werema kuonesha hivyo.

"Maandamano yanawanyima usingizi na kuwatisha. Hawataki wananchi waelezee hisia zao juu ya ufisadi, gharama za maisha, umeme na matatizo mengine yanayowakabili. Atuambie maandamano gani ya CHADEMA ambayo hayakuingiliwa na polisi yaliwahi kuwa na vurugu. Ni pale tu polisi walipoingilia kama ilivyokuwa Arusha, ndipo vurugu zimekuwa zikiibuka," alisema Bw. Heche.

Kwa upande wake Mwenyekiti wa BAVICHA, Mkoa wa Mbeya, Emmanuel Mwakanjila, alisema kuwa ingelikuwa vyema Jaji Werema akaonesha uwezo wake kwa kuishauri serikali itunge sheria kali za kudhibiti na kuchukua hatua dhidi ya ufisadi na mafisadi, ambao kwa namna moja ama nyingine umechangia hali mbaya waliyonayo Watanzania kwa sasa.

Huku akisema kuwa hawaungi mkono namna wabunge wao wanavyotendewa bungeni, akisema anaamini wanasimamia maslahi ya wananchi, Bw. Heche pia alisema kuwa operesheni yao ya Igunga, iliyoongozwa na BAVICHA, ilifanikiwa kwani wamekutana na kuzungumza na wanavijiji katika maeneo yao wakisikiliza kero zao na kujadili mstakabali wa nchi.

5 comments:

  1. Uwezo wa viongozi wengi uko chini man! Kweli CHADEMA they are doing right! Tunapenda peoples party!

    ReplyDelete
  2. Ni hatari sana kwa nchi na raia wake kuwa na viongozi wabovu kuanzia mawaziri wabunge mpaka mwanasheria mkuu tena?tuwaunge mkono hawa wachache wa cdm wanaotutetea jamani.

    ReplyDelete
  3. KWA USEMI HUO HUO WA WEREMA, TUKO WATU WENGI TUNAICHUKIA CCM ATUNGE SHERIA BASI LEO ITAKAYOIPIGA MAARUFU CCM ISIWEPO. THAT IS A VERY CRAZY IDEA HAKUNA MTU ANAYELAZIMISHWA KWENDA KWENYE MAANDAMANO WATU WANAKWENDA KWA HIYARI YAO. BADALA YA KUSHUGULIKIA MATATIZO GENUINE YA WATANZANIA UNATUMIWA NA CCM KISIASA WAZI WAZI.

    ReplyDelete
  4. Uwezo wa Fredrick Werema uko below average ana kauli zilizochoka sana na sijui Kikwete amemteuje mtu kama huyu kushika nafasi kama hiyo !If anything hata hiyo taaluma yake inatia mashaka !Anaendeleza sinema za kina Hosea wa TAKUKURU na Feleshi DPP .Nchi hii inahitaji Uongozi mbadala!

    ReplyDelete
  5. Serikali ya Tanzania ina mchezo wake wa kupoteza wakati ili wamalize muda wao madarakani. Ni serikali gani hii ambayo haitaji changamoto! ni aibu nchi kuongozwa kihuni namna hii. Tunaomba viongozi walio madarakani wamwogope kama siyo kumheshimu Mungu na watimize wajibu wao. Kuwa kiongozi ni chaguo la Mungu, ila haitakiwi kukufuru kiasi hiki. Tunaomba viongozi wote wa dini mbalimbali tuwe na novena (maombi maalum) ya kuomba, ili rehema na baraka za Mungu ziwajeuze viongozi wetu wawe wacha Mungu na kutimiza wajibu wao. Kila mbinu imetumiwa ya kujaribu kuleta changamoto ya wao kuona hali halisi na kuwajibika ila wanakaidi kupendekeza mambo ambayo hayana tija kwa jamii. Maandamano yanapingwa, ufisadi na rushwa vinadekezwa, inaonekana usani mtupu badala ya hatua za vitendo kuchukuliwa ili mradi muda uzidi kwenda mbele, siyo halali hivyo viongozi wetu. Sasa wanataka tufanye nini, jamii inaendelea kuumia, hiyo laani watoto wa viongozi wataweza kuibeba kweli? Viongozi wetu angalieni hilo na kulitathimini. Mungu awabariki na mjitahidi kubadilika, Mungu ibariki Tanzania. Amen

    ReplyDelete