15 August 2011

Simba kamili kuivaa Yanga

*Kazimoto atolewa POP

Na Zahoro Mlanzi

KLABU ya Simba imetamba ipo tayari kuumana na watani zao wa jadi, Yanga katika mchezo wa Ngao ya Jamii kesho kutwa kutokana na majeruhi waliokuwa
nao kwa muda mrefu wote kupona.

Mbali na hilo, klabu hiyo imesema kiungo wao mpya, Mwinyi Kazimoto aliyevunjika mfupa wa mguu naye anaendelea vizuri na ameshatolewa plasta ngumu (POP) na ameanza kukanyaga kidogo kidogo.

Akizungumza kwa simu akiwa njiani na timu yao kurudi Dar es Salaam wakitokea Arusha jana, Ofisa Habari wa klabu hiyo, Ezekiel Kamwaga alisema kikosi chao kipo tayari kwa mchezo huo kwani mpaka sasa hawana majeruhi yeyote.

"Kiukweli timu ipo vizuri licha ya michezo yetu tuliyocheza Arusha kutokuwa na matokeo mazuri lakini kwa ujumla wachezaji wameshaanza kufahamiana ni hicho ndicho kitu kizuri," alisema Kamwaga na kuongeza;

"Pia wale majeruhi wetu akina Ulimboka (Mwakingwe), Uhuru (Seleman) na wengine wote wameshapona na wapo katika viwango vizuri isipokuwa Kazimoto yeye bado anauguza mguu wake uliovunjika," alisema.

Akizungumzia michezo yao ya kirafiki waliyocheza dhidi ya Victors ya Uganda na kufungwa bao 1-0 na kutoka suluhu na AFC Leopards ya Kenya, alisema kocha Mosses Basena aliitumia michezo hiyo kuona wachezaji wake aliowasajili na sasa ameshajua nini la kufanya.

Kwa upande wa suala la Uhuru, alisema Daktari wao, Cosmas Kapinga alishampiga X-ray kiungo huyo na imegundulika kwamba mfupa uliovunjika umeshaungana na anaweza kuanza kukanyaga kidogo kidogo.

Alisema kupona haraka kwa kiungo huyo kumezidisha hamasa kwa wachezaji wengine kujituma na kufanya mazoezi kwa bidiii.

KIUNGO mchezeshaji wa Simba, Mwinyi Kazimoto, anaendelea vizuri na matibabu yake ya mfupa wa mguu uliovunjika, daktari wa timu, Dk. Cosmas Kapinga, amesema.

Kazimoto aliumia katika dakika ya 17 ya mchezo wa fainali ya Kombe la Kagame dhidi ya Yanga baada ya kuumizwa na kiungo wa Yanga, Juma Seif Kijiko.

Lakini akizungumza na tovuti ya klabu, www.simba.co.tz jijini Dar es Salaam leo, Kapinga alisema maendeleo mazuri ya afya ya Kazimoto yamesababishwa zaidi na nidhamu yake ya hali ya juu ya kufuatilia matibabu.

"Kazimoto amenifurahisha sana. Katika wachezaji wenye nidhamu ya hali ya juu ya kufuata ushauri wa kitaalamu Mwinyi ni mmoja wao. Lile P.O.P alilofungwa mguuni limeanza kulegea na yeye hasikii maumivu yoyote.

"Katika tiba, kama POP limeanza kulegea na mchezaji hasikii maumivu, hiyo maana yake ni kuwa mfupa umeanza kuunga. Hii ni ishara kuwa ataweza kuondolewa hilo POP katika muda wa siku 45 kama tulivyokuwa tumesema awali.

"Ili mgonjwa apone maumivu ya aina ya aliyoyapata Kazimoto, ni lazima afuate kila anachoshauriwa na daktari. Asikanyage chini mguu, akilala basi mguu uwe juu ya mto na pia asivute sigara wala kunywa pombe. Na masharti yote hayo Mwinyi ameyafuata kwa uadilifu mkubwa. Tunashukuru sana," alisema Dk. Kapinga.

Hadi wakati anatolewa uwanjani, Mwinyi ndiye aliyekuwa nyota wa mechi hiyo ya fainali na wachambuzi mbalimbali wa soka, kikiwamo kituo cha SuperSport, walisema kuwa Simba isingefungwa iwapo kiungo huyu angecheza kwa dakika 90 tu za mechi hiyo.

  

No comments:

Post a Comment