*Vikundi vya ulinzi Temeke vyapewa mafunzo
Stella Aron na Charles Lucas
JESHI la Polisi nchini limetoa tahadhari kwa wananchi kusherehekea Sikukuu ya Id el Fitr kwa amani na utulivu bila kuvunja sheria.Taarifa iliyotolewa na
Msemaji wa jeshi hilo, Bi. Advera Senso, imesema kutokana na uzoefu jeshi hilo, wananchi wengi hupenda kutumia siku hiyo kufanya uhalifu.
“Waumini wengi siku hiyo hupenda kuabudu na kumalizia sherehe katika maeneo ya starehe, wengine hupenda kufanya uhalifu katika hivyo tunatoa tahadhari kwa wahusika,” alisema.
Aliongeza kuwa, katika kutekeleza kampeni ya utii wa sheria bila shuruti, wananchi wanapaswa kuzingatia kanuni, taratibu, sheria za nchi na kuepuka vitendo vya uhalifu.
“Wananchi ambao watatoka katika makazi yao, wasiache nyumba wazi na kama kuna mtu wanamtilia shaka, watoe taarifa haraka katika Kituo cha Polisi, madereva wote waepuke mwendo kasi na kuacha kujaza abiria kupita kiasi au kutumia kilevi wawapo kazini,” alisema Bi. Senso.
Alisema wamiliki wa kumbi za starehe wazingatie matumizi ya kumbi zao katika uingizaji watu kulingana na uwezo wa kumbi kwani baadhi yao huendekeza tamaa ya fedha kwa kujaza watu kupita kiasi na kusababisha mafaa.
Katika kuhakikisha kuwa wananchi wanashereheke sikukuu kwa amani na utulivu, jeshi hilo limejipanga kikamilifu kuimarisha ulinzi katika maeneo ya kuabudia, barabarani, fukwe za bahari na kumbi za starehe.
Aliongeza kuwa, wadau wote wa ulinzi watoe ushirikiano ili kuhakikisha hakuna vitendo vya uvunjifu wa amani katika kipindi chote cha sikukuu.
Wakati huo huo, Jeshi la Polisi Mkoa wa Temeke, limetoa semina elekezi kwa vikundi mbalimbali vya ulinzi shirikishi mkoani humo ikiwa ni juhudi za jeshi hilo kupambana na vitendo vya uhalifu hasa katika kipindi cha sikukuu ya Id el Fitr.
Akizungumza na Majira Dar es Salaam jana, Kamanda wa Polisi mkoani humo, David Misime, alisema lengo la mafunzo hayo ni kuimarisha amani na utulivu kwa wananchi.
Aliwataka wazazi, kutowaacha watoto watembee peke yao bila kuwa na waangalizi ili wasipotee ambapo jeshi hilo, limejipanga vizuri kudhibiti vitendo vyote vya uhalifu.
“Wamiliki wa kumbi za starehe, wazingatie sheria na taratibu za kuendesha biashara zao ili kuepuka maafa, watu ambao watafanya disko toto bila vibali watachukuliwa hatua za kisheria.
“Madereva ambao wataendesha magari ya kwenda fukwe za Kigamboni, wazingatie sheria za usalama barabarani badala ya kuendesha kwa ushabiki na kusababisha ajali,” alisema.
Alisema baadhi ya maeneo waliyotembelea na kuongea na vikundi mbalimbali ni Mbagala, Mbande na Chamazi.
Alitoa wito kwa wakazi wa Temeke, kuwa watulivu na kuchukua tahadhali ili kuzuia uharifu na kusherehekea sikukuu kwa amani.
No comments:
Post a Comment