Na Stella Aron
JESHI la Polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam, linamshikilia mtoto mwenye umri wa miaka saba (jina tunalihifadhi), kwa uchunguzi zaidi baada ya kukiri kushiriki vitendo vya
ushirikina na kujaribu kumuua mama yake mzazi, Bi. Jane Berege (27), mkazi wa Tegeta jijini humo.
Mtoto huyo alisababisha baadhi ya askari wa Kituo Kikuu cha Polisi Dar es Salaam, kuacha shughuli zao kutokana na kuelezea matendo mbalimbali anayofanya ya kishirikina.
Kaimu Kamanda wa Polisi Mkoa wa Ilala, Bi. Sada Juma alithibitisha jeshi hilo kumshikilia mtoto huyo kwa ajili ya uchunguzi wa akili kwa kile alichodai kuwa ni kutokana na serikali kutoamini masuala ya uchawi.
Alisema sababu za mtoto huyo kufikishwa kituoni hapo ni baada ya kuzuka kwa malumbano makali kati yake na mama yake juzi katika eneo la kivuko cha Kigamboni ambapo mama alikuwa akienda kuomba msaada kwa ndugu.
Kamanda Sada alisema kutokana na hali hiyo baadhi ya watu walikusanyika ambapo polisi walilazimika kuwachukua wote wawili ili kupata taarifa zaidi.
Alisema mtoto huyo ambaye amekuwa akizunguka na sare za shule ni mwanafunzi wa darasa la kwanza katika shule ya Ebeneza, katika mahojiano naye alikiri kushiriki vitendo hivyo.
Kamanda Sada alisema kwa mujibu wa mama wa mtoto huyo, amechoka na vitendo anavyofanya mtoto huyo kiasi cha kusababisha ndugu kumkataa kufika nyumbani kwao.
"Huyu mama anaamini kuwa vitendo anavyofanya mwanaye ni vya kishirikina, lakini sisi kama hatuamini hilo na tunamshikilia kwa ajili ya uchunguzi zaidi ili kufahamu kama mtoto huyo ana akili timamu au la," alisema Kamanda Sada.
Kamanda Sada alidai kuwa hivi karibuni, mtoto huyo alimkaba mama yake na matokeo yake akapata ugonjwa wa shinikizo la damu na kusababisha alazwe hospitali.
No comments:
Post a Comment