18 August 2011

Kizimbani kwa kumtishia askari

Na Rehema Maigala

MFANYABIASHARA Bw.Adolfu Lukosi (28), mkazi wa Sinza Wilaya ya Kinondoni amefikishwa Mahakama ya Mwanzo Kinondoni kujibu shitaka la kutishia
kuua askari.

Ilidaiwa mahakamani hapo juzi kuwa Agosti 4, mwaka huu,mshitakiwa alimtamkia mlalamikaji koplo Victoria kuwa ni lazima atamuua kwa kumchoma moto yeye na gari yake .

Mbele ya Hakimu, Bi. Hanipha Mwingira, ilidaiwa na karani wa mahakama, Bi. Sharifa Dunia, kuwa mshitakiwa alimtishia mlalamikaji kuwa atamchoma moto hadi afe.

Mshitakiwa alikana shitaka hilo na yupo nje kwa dhamana hadi kesi hiyo itakapotajwa tena Agosti 22, mwaka huu.

Pia, Bw.Babilon Alex (21), mkazi wa Kunduchi Wilaya ya Kinondoni amefikishwa Mahakama ya Hakimu Mkazi Kinondoni kujibu shitaka la kuvunja ofisi na kuiba.

Ilidaiwa mahakamani hapo kuwa,Julai 16, mwaka huu,mshitakiwa alivunja ofisi ya Inter Press Tanzania na kuiba vitu mbalimbali vilivyokuwemo ndani vyenye thamani ya sh.17,300,000 mali ya ofisi hiyo.

Vitu vinavyodaiwa kuibiwa ni,gari la ofisi namba za T.385 AYN, kompyuta na vifaa vingine.

Mbele ya Hakimu Bw.Yohana Yongolo ilidaiwa na Mwendesha Mashitaka Bw.Mtani Magoma kuwa,mshitakiwa aliiba vitu hivyo mali ya mlalamika.

No comments:

Post a Comment