26 August 2011

Mkurugenzi atoa ufafanuzi sakata la madiwani Arusha

Na Jane Edward, Arusha

SAKATA la kutimuliwa madiwani watano wa Chama cha Demokrasi na Maendeleo (CHADEMA), Jijini Arusha, limechukua sura mpya baada ya Mkurugenzi wa
Jiji hilo, Bw. Estomih Chang'a, kujibu tuhuma za kuwaruhusu madiwani hao kuendelea kutekeleza majukumu yao wakati chama kimewavua uanachama.

Akizungumza na waandishi wa habari jana, Bw. Chang'a alisema yeye binafsi wala Meya wa Jiji hilo Bw. Gaudence Lyimo, hawana mamlaka ya kuwasimamisha madiwani hao isipokuwa Ofisi ya Waziri Mkuu, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI).

Alisema kwa mujibu wa Sheria ya Serikali za Mitaa, Mamlaka za Miji Ibara ya 8 ya mwaka 1982, kifungu cha 26, kifungu kidogo cha kwanza (e), inasema Mwenyekiti wa Halmashauri ana uwezo wa kumfahamisha Waziri husika juu ya madiwani kupoteza udhamini na uanachama ili aweze kutoa tamko.

Alisema Bw. Lyimo alimuandikia barua Waziri mwenye dhamana Bw. George Mkuchika Agosti 12,2011 yenye kumbi namba MD/US/101/1/107 ili aweze kutoa tamko au mwelekezo juu ya hatma ya madiwani hao.

“Nimepokea barua kutoka TAMISEMI ambapo Bw. Mkuchika alisema, kwa kuzingatia masharti ya kifungu cha 39 (1) (f), cha Sheria ya Ukaguzi wa Serikali za Mitaa, hatua ya kuvuliwa uanachama inasababisha mhusika kupoteza sifa ya kuwa diwani,” alisema.

Alisema kwa kuwa madiwani hao wamefungua kesi ya madai namba 17/2011 katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Arusha kupinga kufukuzwa uanachama, Ibara ya 13 ya Katiba ya Jamhuri wa Muungano wa Tanzania ya mwaka 1977, inasema haki za raia na wajibu na maslahi ya kila mtu, yatalindwa na kuamuliwa na mahakama pamoja na vyombo vinginevyo vilivyowekwa kwa mujibu ya sheria.

Aliongeza kuwa, katika kutekeleza masharti ya katiba hiyo Serikali, taasisi au mtu yeyote, haruhusiwi kutoa uamuzi jambo ambalo liko katika mahakama hivyo ni vyema mahakama isubiliwe itoe uamuzi ili madiwani hao wajua hatma ya uanachama wao.

Bw. Chang’a aliongeza kuwa, katika kutekeleza sheria ya mahakama mtu au Serikali haipaswi kutolea ufafanuzi swala la madiwani hao hivyo wataendelea kuwa madiwani wanaotambulika mpaka hapo mahakama itakapotoa uamuzi.

4 comments:

  1. ukifukuzwa kazi na kampuni yeyote ile huwezi kuendelea kutambulika kama mfanyakazi wa kampuni usika na kama ukienda mahakamani basi hautoendelea kufanya kazi mpaka pale mahakama itakapokurudisha kazini. kitendo cha serikali kuendelea kuwatambua na kuwalipa watu waliofukuzwa na chadema ni jitihada zake za kutaka kuendeleza migogoro isiyo na tija.

    ReplyDelete
  2. Unajua sheria? acheni kujifanya mnajuakila jambo. No research no right to speak

    ReplyDelete
  3. Sijui ni kwa nini serikali hii ya CCM inafanya mambo ya kutuudhi hata wanachama wachache wa CCM tuliobaki na kuvuta subira kwamba labda watajirekebisha na mambo kuwa sawa tena! Kwa hakika wanatusukumia upinzani, na haswa haswa CHADEMA ambao sasa ndiyo wanaonekena kama watetezi wa wanyonge badala yetu sisi CCM.
    Inasikitisha kuona eti ofisi ya Waziri Mkuu haijamwelekeza Mkurugenzi wa Jiji la Arusha juu ya kuvuliwa udiwani kwa madiwani wa CHADEMA ambao chama chao kimetamka rasmi kuwavua uanachama.
    Mantiki ya kawaida kabisa hapa ni kama wataendelea kulipwa posho na kuingia katika Baraza la Madiwani watakuwa wanakiwakilisha chama kipi? Nasema hivi kwa sababu hawakuchaguliwa kama wagombea Binafsi, hoja ambayo serikali na Mahakama kuu ilipinga, walichaguliwa kupitia chama ambacho kwa sasa kimewakana; je wanabaki kuwakilisha chama kipi? CCM?
    Hapa kuna dhana mbili tu za kwa nini Waziri Mkuu hajachukua hatua za kuusimamisha uwakilishi wao rasmi, au CHADEMA wanabwabwaja majukwaani tu bila ya kuziandikia ofisi za waziri Mkuu na Mkurugenzi, au Waziri Mkuu na ofisi yake ni wazembe wa kuchukua hatua na hivi kuiaibisha serikali na chama chetu.
    Ikiwa mtaendelea na utendaji wa namna hivi basi tujiandae kuchukua nafasi iliyopata CUF mwaka jana maana hata sisi wenye roho ngumu sasa tumechoka.

    ReplyDelete
  4. Huu ni ushambenga kabisa............haiwezekani mtu akafukuzwa uanachama akakimbilia mahakamani halafu iwe kinga ya kutofukuzwa hata kama ameonewa labda kwa mahakama kumpa kinga tajwa................mahakama haijawapa kinga hiyo....................mbona mbunge akitenguliwa na mahakama na kukataa rufaa hamsemi aendelee na Ubunge hadi rufaa yake ikaamuliwa vinginevyo...............ccm kwa vile wananufaika na hao madiwani haramu na ndiyo maana wanatafuta tafsiri haramu za kisheria kuhalalisha dhuluma dhidi ya wapigakura wa Arusha...

    ReplyDelete