17 August 2011

Miss Tanzania watembelea kaburi la Sokoine

Na Mwandishi Wetu

WANYANGE wanaowania umalkia wa Vodacom Miss Tanzania 2011, juzi walitembelea kaburi la Waziri Mkuu, Edward Moringe Sokoine lililopo wilayani
Monduli, Arusha.

Warembo hao wako katika ziara ya mafunzo iliyoandaliwa na kampuni ya Vodacom, walianzia mkoani Morogoro katika hifadhi ya Taifa ya Mikumi.

Wakiwa eneo la Monduli,  wanyange hao walipokelewa na mtoto wa Sokoine, Namelok  ambaye pia ni Mbunge wa Viti Maalum (CCM) Mkoa wa Arusha.

Mbunge huyo aliwapa historia fupi ya maisha ya baba yake, hasa alipokuwa Waziri Mkuu, wakati wakiwasili wilayani Monduli, warembo hao walipokelewa na mke wa Waziri Mkuu mstaafu, Regina Lowasa na viongozi wengine wa wilaya hiyo.

Namelok alipata nafasi ya kuwaasa warembo hao wanaowania umalkia wa Tanzania.

Aliwataka warembo hao watumie ziuri ziara zao za kutembelea vivutio vya utalii na maeneo ya kihistoria ili wakaihamasishe jamii kuhusu umuhimu wa elimu kwa watoto wa kike, hasa jamii ya kimasai.

Alisema jamii ya kimasai ambayo inajishughulisha na ufugaji, haijatoa kipaumbele kumsomesha mtoto wa kike, hivyo ziara ya warembo hao inaweza kutumika kubadilisha mtizamo huo.

 Akizungumzia ziara hiyo, Meneja Uhusiano na Habari kwa Njia ya Mtandao wa Vodacom Tanzania, Matina Nkurlu, alisema washiriki hao walijifunza vitu mbalimbali alivyovifanya hayati Sokoine enzi za uhai wake.

Mara baada ya kutoka katika eneo hilo, warembo hao 30, walitembelea Shule ya Maasai Girls iliyopo Monduli.

"Ziara yetu bado inaendelea na warembo wanaendelea kujifunza kupitia elimu inayotolewa na wataalam mbalimbali wanaokutana na warembo. Ni matumaini yetu wataitumia elimu hii kulitangaza taifa katika medani za kimataifa," alisema Nkurlu.
Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Lino Agency ambao ndio waandaaji wa Vodacom Miss Tanzania, Hashim Lundenga, alisema warembo hao watatembelea Mamlaka ya Hifadhi ya Ngorogoro (NCAA), ili kujionea moja ya maajabu saba ya dunia.


No comments:

Post a Comment