Na Mhaiki Andrew, Songea
MMOJA wa wadau wa soka wa mjini Songea, Ruvuma, anajipanga kuanzisha mashindano ya soka kwa shule za Sekondari za manispaa hiyo.Lengo la mashindano
hayo ni kuendeleza soka kuanzia ngazi za shule, ambapo yatachezwa kwenye Uwanja wa Shule ya Msingi, Matarawe mjini Songea.
Akizungumza mjini Songea jana, Mratibu wa mashindano hayo, Alfonce Bakulebakule, alisema alivutiwa na viwango vya soka vilivyooneshwa na wanafunzi wakati wa mashindano ya Shule za Sekondari (UMISETA), yaliyomalizika hivi karibuni.
Alisema shule za sekondari zina wachezaji wazuri na wenye vipaji, lakini wamekosa watu wa kuwaendeleza zaidi.
Alisema mafanikio ya wachezaji hao, yatasaidia kutoa mchango mkubwa kwa manispaa hiyo na mkoa wao.
Mdau huyo alisema serikali kupitia wizara husika, imerejesha mashindano ya UMISSETA, lakini hayako katika mpango mzuri kama ilivyokuwa miaka ya zamani.
Alisema miaka ya nyuma, klabu mbalimbali wakati wa usajili, zilikuwa zikiitupia macho michuano ya UMISSETA na shule za msingi (UMITASHUMTA), kwa ajili ya usajili wa timu zao, lakini kwa sasa hilo halipo.
Alisema kabla ya kuanzisha michuano hiyo, atahakikisha anadhibiti mamluki ambao wataweza kuitia doa michuano hiyo.
Alisema shule itakayogundulika kutumia wachezaji mamluki, itaondolewa kwenye mashindano hayo.
"Ninaamini kama walimu wote watakuwa na busara, wakiwatumia wanafunzi wao, michuano hii itakuwa na mvuto kwa mashabiki wa soka," alisema.
Bakulebakule alisema yupo katika hatua za mwisho za kuomba kibali cha kuanzisha mashindano hayo kutoka Chama cha Mpira wa Miguu Songea (SUFA), kupitia kwa Ofisa Elimu wa Sekondari Manispaa ya Songea ili shule zitakazoshiriki zipate ruhusa.
Naye, Katibu Mkuu wa SUFA, Ajabah Chitete, alisema wamepokea taarifa za maneno, lakini wamemtaka mratibu huyo kuwapelekea taarifa ya maandishi.
Alisema mratibu huyo awapelekee barua ya kuomba kuendesha michuano hiyo kupitia kwao, kabla ya kupekelekwa kwa Ofisa Elimu Manispaa hiyo ili atoe ruhusa kwa wanafunzi kushiriki mashindano hayo.
No comments:
Post a Comment