30 August 2011

Manispaa Ilala yadaiwa kuuza eneo la wazi

Na Mwandishi Wetu 
 
MEYA wa Manispaa ya Ilala Bw.Jerry Silaa na Mkurugenzi wa Manispaa hiyo Bw. Gabriel Fuime wanadaiwa kuruhusu ama kuzembea hadi kuuzwa eneo la
wazi lililopo mbele ya jengo la kampuni ya CMC Automobiles Mtaa wa Maktaba, Dar es Salaam.
 
Hata hivyo walipoulizwa na gazeti hili kwa njia ya simu wiki iliyopita wote wawili kwa nyakati tofauti walikiri eneo hilo kumilikiwa na kampuni binafsi ya CMC Automobiles lakini wakadai hawajui kampuni hiyo ilipataje eneo hilo.
 
“Ni kweli hata watu wa serikali ya mtaa waliniambia kuwa eneo hilo linamilikiwa na
mtu binafsi kimakosa ila sikupata muda wa kufuatilia undani wake,” alisema Meya wa
Ilala Bw.Silaa na kuongeza:
 
“Lakini kumbuka kuwa kuna maeneo tuliyatoa kwa watu wenye uwezo wa kuyapendezesha wafanye hivyo kwa ajili ya kulipendezesha Jiji inawezekana huyo alipata kwa njia hiyo.”
 
Hata hivyo alipoulizwa iwapo lengo lilikuwa ni kupendezesha maeneo ya mji kwa manufaa ya jamii, kwa nini CMC Automobiles imejenga uzio wa gharama kubwa kuzuia watu wasipite eneo hilo alikiri kuuona uzio huo na kusema ni kosa kuujenga kwa kuwa hata kama ilipewa kwa ajili ya kupendezesha eneo hilo lilitakiwa kuendelea kuwa wazi.
 
Kwa upande wake Mkurugenzi wa Manispaa hiyo Bw.Fuime aliomba apewe muda ili afanye
uchunguzi kuhusu kampuni hiyo ilipataje eno hilo kisha atatoa majibu. “Kweli hata mimi nimeona amejenga uzio katika eneo hilo na nakiri ni eneo la wazi lakini nipe muda nifanye uchunguzi nitakupatia majibu,” aliseama.
 
Alipoulizwa kuwa uzio huo umejengwa toka muda mrefu na yeye anakiri kuuona siku nyingi kwa nini hakuchukua hatua mapema, huku kibali cha ujenzi wa uzio huo kikitolewa na ofisi yake, mkurugenzi huyo alisisitiza kutoa majibu yote baada ya kufanyika uchunguzi wake.
 
Habari kutoka vyanzo vyetu vya habari ndani na nje ya manispaa hiyo zinadai kuwa eneo hilo limeuzwa kinyemela kwa kushirikisha baadhi ya watu wenye vyeo vya juu katika manispaa hiyo ambao walipokea shilingi milioni 60 na kugawana milioni 20 kila mmoja.
 
Mwandishi alipofika katika ofisi za kampuni hiyo zinazopakana na eneo hilo alizuiwa
kuonana na Mkurugenzi wa kampuni hiyo aliyetajwa kwa jina la Bw.Abdul Hajji.
 
Karani wa mkurugenzi huyo alidai kuwa Bw.Abdul Hajji si mkurugenzi wa kampuni bali yeye ni mwenyekiti wa Bodi ya kampuni hivyo hawezi kuzungumzia suala lolote linalohusu kampuni hadi awepo mkurugenzi mtendaji ambaye alidai amesafiri nje ya nchi.
 
Naye mwenyekiti wa serikali ya Mtaa wa Kisutu lilipo eneo hilo Bw.Yussuf Mohamed alipopigiwa simu aelezee iwapo CMC Automobiles ilipitishia maombi ya kupatiwa eneo hilo kwake, aling’aka kwa hasira na kusema hajui suala hilo na hajawahi kuona ombi lolote. “Usiniulize mimi waulize Manispaa,” alisema na kisha kukata simu.
 


No comments:

Post a Comment