18 August 2011

Wabunge wamlipua Msekwa

*Msigwa asema anagwa maeneo ya kitalii Ngorongoro
*Ole Telele amtaka Waziri Maige kuvunja bodi yake
*Waziri Maige akaangwa kwa wanyama waliotoroshwa


Na Waandishi Wetu, Dar, Dodoma

KAMBI ya Upinzani Bungeni imemtaja Makamu Mwenyekiti CCM, Bw. Pius Msekwa ambaye pia ni
mwenyekiti wa Bodi ya Hifadhi ya Ngorongoro kuwa amejigeuza mwenyekiti mtendaji wa hifadhi na kufikia hatua ya kugawa maeneo kwa wafanyabiashara kwa ajili ya shughuli za kitalii kinyume na taratibu.

Uovu mwingine ulioibuliwa na kambi hiyo ni pamoja na wizi wa wanyamapori wapatao 130, ambao walisafirishwa kupitia Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Kilimanjaro (KIA) kwenye ndege ya Qatar.

Akiwasilisha maoni ya kambi hiyo, Waziri Kivuli Maliasili na Utalii, Mchungaji. Peter Msigwa (Iringa Mjini-CHADEMA), alisema hali hiyo inachangia kudhoofisha rasilimali za Watanzania.

“Pamoja na matatizo mengine mengi, hifadhi ya taifa  ya Ngorongoro inakabiliwa na tatizo la kuwa na mwenyekiti wa bodi anayevuka mipaka ya majuku yake, tuna ushahidi kuwa Makamu Mwenyekiti wa CCM, Mhe. Pius Msekwa ambaye ndiye mwenyekiti wa bodi hiyo, amegeuka kuwa mwenyekiti mtendaji anayefanya kazi ya kutoa 'offer' kwa wafanyabiashara wenye mahitaji ya kujenga hoteli za kitalii huku akiwaelekeza maeneo, kazi ambayo si yake,” alisema Mchungaji. Msigwa.

Mchungaji Msigwa alisema kutokana na utaratibu huo unasababisha mgongano mkubwa wa kimaslahi na wenye madhara makubwa katika hifadhi hiyo.

“Haiwezekani mwenyekiti wa bodi ya ngorongoro ambaye moja ya majukumu yake ni kukagua hali halisi ya hifadhi hiyo, ajiingize  katika shughuli za utendaji, tena zilizo nyeti kama hizo. Mheshimiwa Naibu Spika, Kambi Rasmi ya Upinzani inaitaka serikali kuchukua hatua kali dhidi ya mwenyekiti huyu wa bodi mara moja kwa kukiuka mipaka ya majukumu yake na tunaahidi kuipa serikali ushirikiano kuhusiana na tuhuma hizi,” alisema Bw. Msigwa.

Akichangia mjadala huo, Mbunge wa Ngorongoro, Bw. Saning'o Telele alimtaka Waziri wa Maliasili na Utalii, Bw. Ezekiel Maige kuvunja Bodi ya Ngorongoro inayoongozwa na Msekwa, huku akifafanua tuhuma kuwa amegawa eneo la kujenga Hoteli ya Kitalii kwenye hifadhi hiyo na kuonya kuwa wananchi watapimana naye nguvu kwa kukataa ijengwe mahali hapo.

Utoroshaji wayamapori

Akizungumzia sakata la utoroshaji wa wanyamapori, Mchungaji Msigwa alisema haiwezekani wanyamapori hai 130 wakiwemo twiga, waibwe na kusafirishwa kupitia uwanja huo bila taarifa yoyote kutoka wizara husika.

"Kambi ya Upinzani inaitaka serikali kuwachukulia hatua za kisheria na nidhamu aliyekuwa Katibu Mkuu wa Wizara hii, Bw. Ladislaus Komba na Mkurugenzi wa Idara ya Wanyamapori, Bw. Erasmus Tarimo kwa uzembe uliopelekea au kufanikisha wizi wa wanyamapori hai 130, wakiwemo twiga, uhalifu uliofanyika Novemba 26, mwaka jana," alisema Mchungaji Msigwa.

Alisema moja ya majukumu makuu ya wizara hiyo ni pamoja na kulinda rasilimali za nchi na mali kale dhidi ya matumizi haramu ya kuhakikisha utoaji bora wa huduma za kitalii unafanyika.

“Lakini mheshimiwa spika utoroshaji huu wa wanyamapori unaonyesha viongozii na watumishi hawa wa umma wameshindwa kutimiza wajibu wao hivyo kambi ya upinzani inaitaka serikali kuwawajibisha kwa sababu ya kuzembea wajibu wao na kusababisha wizi uliofanyika,” alisema Mchungaji Msigwa.

Kwa mujibu wa mbunge huyo, serikali inapaswa kuwawajibisha wakuu na watendaji wote wa vyombo vya usalama waliopewa dhamana ya moja kwa moja ya kulinda maliasili lakini wakaachia wizi huo kutendeka.

"Na tunaitaka serikali ilieleze bunge hili wanyama wetu hao wako wapi mpaka sasa?" alihoji.

Kwa upande wake Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Ardhi, Maliasili na Mazingira imesema serikali imepata kigugumizi kutolea ufafanuzi wa wizi wa wanyamapori 116 hai na ndege 16 walioibwa nchini Novemba 24, mwaka jana kama wanarudishwa nchini na wahusika kuburuzwa mahakamani.

“Kwa hakika kuna dalili kubwa ya uzembe na kulindana ndani ya Wizara hii na ndiyo maana kumekuwa na kigugumizi katika kushughulikia ushauri wa kamati," alisema Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge, Ardhi, Maliasili na Utalii, Bw. James Lembeli.

"Mheshimiwa naibu spika wanyamapori walioibwa wana thamani ya sh. 163,732,500 na ndege hai wana thamani ya sh. 6,838,000 kupitia uwanja wa KIA na ndege ya jeshi la Qatar.

“Na mpaka Kamati yetu inatoa taarifa hii ndani ya bunge lako tukufu, haijulikani wanyama wale baada ya kupakiwa pale Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Kilimanjaro walipelekwa wapi wala bado wapo hai," aliongeza

Kwa mujibu wa Bw. Kembeli kamati imebaini kuwa uharamia huo ulifanywa na Watanzania na kwamba kigugumizi cha serikali kushughulikia suala hilo kimeisikitisha kamati yake kwa kuwa rasilimali iliyoibwa ni adimu na haijulikani ipo wapi na itarudishwa lini hapa nchini nchini.

Akichangia hoja hiyo, Mbunge wa Sikonge, Bw. Juma Nkumba alishangaa jinsi wanyama hao wanavyoweza kutoroshwa katika nchi yenye vyombo vya ulinzi vya kutosha na kupendekeza wanyama hao kama bado wako hai warudi na kama wamekufa mafuvu yao yarejeshwe.

Mamlaka makubwa ya waziri


Mchungaji Msigwa alisema kuwa sheria ya Wanyamapori ya mwaka 2009 namba 38 (3)(e) imempa madaraka makubwa waziri mwenye dhamana katika mchakato mzima wa ugawaji wa vitalu vya uwindaji, ikiwemo kuteua wajumbe watano wa kuingia kwenye Kamati ya Ushauri ya Ugawaji wa Vitalu vya Uwindaji.

Baadhi ya wajumbe walioteuliwa na Waziri Maige kuingia kwenye kamati hiyo ni Bw. Benno Malisa (Makamu Mwenyekiti wa UVCCM na Bw. Daniel Nsanzungwako (ambaye pia ni kada wa CCM),” aliongeza.

Bw. Msigwa alisema kutokana na uteuzi huo kambi hiyo imeshtushwa na uteuzi wa wajumbe hao kuingia kwenye kamati hiyo ya kumshauri wakati hawana vigezo vinavyotakiwa, ikiwemo ujuzi na uzoefu kwenye masuala ya utawala, na uhifadhi wa mazingira unaohusiana na uwezeshaji wa kiuchumi,” alisema Bw. Msigwa.

Imeandaliwa na Godfrey Ismaely, Pendo Mtibuche na Peter Mwenda



5 comments:

  1. Hongera Chedema kwa kuzidi kufichua uovu na uozo wa viongozi wa nchi hii wasioshiba na wasio na kiasi. BRAVO CHADEMA.

    ReplyDelete
  2. Ukweli kabisa sasa nchi inakwenda pabaya tusipokuwa makini. Jamani jamani Mwenyenzi Mungu atuepushe kabisa na ufisadi mkubwa kama huu. Ndio maana tunasisitiza kuwa kumnyooshea kidole Mh.Lowasa na Mh.Chenge peke yao sio vizuri mafisadi huko CCM wako wengi. Haya mpaka Makamu Mwenyekiti wa CCM Pius Msekwa naye ni fisadi mkubwa aliyebobea lakini hapo hapo ni mmojawapo wa waliowataka Rostam, Lowassa, Chenge kujivua gamba kumbe naye ana magamba. Sasa yeye awe wa kwanza kujivua gamba kwa sababu ni Makamu Mwenyekiti wa Chama Tawala kilichotangaza kujivua gamba. Hivi mtu kama Kijana BENO MALISA kupewa wadhifa mkubwa kiasi hicho wakati hana vigezo vyo vyote manake nini haswa? Mbona kuna wasomi wazoefu wengi tu huyu Waziri Maige naye ana ajenda yake ya siri kuhusu uteuzi huu. Atueleze.

    ReplyDelete
  3. KWANI NYIE MLIDHANI Msekwa ni mtu msafi sana





















    Kwani nyie mlidhani huyu jamaa ni mtu msafi sana kwa vile ni Makamu wa ccm. Nani msafi katika chama hicho cha mafisadi. Wako kuliibia taifa kila leo. Yeye kaanza kula si leo bali tangu zamani.
    Watanzania vijana tunamtazama tu, lakini hajui siku moja yatamtokea puani. CCM na serikali yake wote wachafu wananuka ufisadi.

    ReplyDelete
  4. Ni hayo matumbo tu wanayojali. Ukisikia yakiongea utadhania yanajali maslahi ya Watanzania lakini ni porojo tu. Kwanza mijitu kama Msekwa hayapendi hata kidogo kuona mlalahoi ameinuka ubavu. Wanataka kuona walalahoi wote kuwa watumwa nao wawe mamwinyi. Wamefanywa vibaraka wa ukoloni mambo lena wakabakia kuchekelea na kuishangilia hali hiyo ya kufanya taifa kuwa mali ya wageni. Wanatupeleka pabaya hawa akina msekwa na gende lake la white collar criminals.

    ReplyDelete
  5. jamani watanzania wenzangu, hali ni mbaya sana. Wanyama wanaibwa, ngorongoro inaliwa, mafuta hakuna, umeme mgawo. jamani watanzania tuamke. Watanzania tumekuwa zoba mno ndo maana hawa viongozi wa ccm wanaiba mchana kweupeeee.

    Maana sasa upole wa watanzania umezidi kiasi.

    Tuandamane tuitoe hii serikali dhalimu ya ccm.

    jamani misri, tunisia, libya wameweza. Hata jirani zetu malawi wameweza jee sisi watanzania vipi.

    Njaa zitatuuwa watanzania na uoga wetu.

    Wanaume wanatelekeza familia mke na watoto kisa wamenyang'anywa ardhi halafu vigogo wa ccm wanahodhi. Jamani familia zinateseka wakati rasilimali zetu watanzania zinaishia mfukoni kwa familia kuu za ccm???

    Watanzania tuamke jamani

    ReplyDelete