26 August 2011

Dereva aliyesabisha kifo cha mbunge kortini

Na Rehema Mohamed

DEREVA aliyekuwa akiendesha gari lililosababisha kifo cha Mbunge wa Baraza la Wawakilishi Zanzibar, Bw.Mussa Khamisi Silima na
mkewe Bi.Mwanakheri Ally (48), Bw.Chazard Sebunga (31) amesomewa kesi ya kusababisha vifo muda mfupi baada ya kuruhusiwa kutoka Taasisi ya Tiba ya Mifupa (MOI).

Dereva huyo alisomewa mashitaka hayo Dar es Salaam jana na  mwendesha Mashitaka Bw.Nassoro Katunga, mbele ya Hakimu wa Mahakimu wa Mahakama ya Wilaya Ilala, Bi.Joyce Minde.

Bw.Katunga alidai kuwa mtuhumiwa huyo alitenda kosa hilo Agosti 21, mwaka huu saa 9 alfajiri Dodoma eneo la Nanenane Mzunguni.

Ilidaiwa kuwa mtuhumiwa akiwa anaendesha gari namba T 509 AJC Toyota Corolla pasipo uangalifu kwa watumiaji wengine wa barabara, hakuchukua tahadhari wakati akilipita  gari namba T 330 AYE Isuzu ERL aina ya lori ,lililokuwa na tela T 673 ATS.

Alidai kuwa wakati akitoka upande wa kushoto kwenda kulia kulipita gari hilo aligongana na gari aina ya Scania T 497 ASW  lililokuwa linatoka mbele yake na kusababisha ajali hiyo.

Mashitaka mengine anayomkabili mtuhumiwa huyo ni kusababisha majeraha  kwa abiria Bi.Salma Juma aliyekuwa katika gari T 509 AJC Toyota Collora.

Bw.Katunga alidai kuwa upelelezi wa kesi hiyo bado haujakamilika. Mshtakiwa alikana mashitaka hayo, hata hivyo alikosa dhamana baada ya kushindwa kutimiza masharti ya dhamana. Kesi hiyo iliahirishwa Septemba 9, mwaka huu.

No comments:

Post a Comment