Na Zahoro Mlanzi
KOCHA Mkuu wa timu ya taifa 'Taifa Stars' Jan Poulsen, amemwita beki wa Simba Victor Costa 'Nyumba' katika kikosi chake kitakachoivaa Nigeria katika mechi ya kuwania
kucheza fainali za mataifa ya Afrika mwakani.
Mbali na Costa, kocha huyo pia amemwita kiungo mchezaji wa Yanga Juma Seif 'Kijiko' kwa ajili ya kuimarisha sehemu kiungo.
Mechi hiyo ya Taifa Stars dhidi ya Algeria inatarajia kupigwa Septemba 3, mwaka huu katika wa Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.
Beki huyo kwa mara ya mwisho kuitumikia timu hiyo ilikuwa mwaka 2007, lakini aliumia akiwa mazoezini na Stars ambapo baadaye akaondoka nchini kwenda Msumbiji kucheza soka la kulipwa katika Klabu ya HCB de Songo kwa miaka mitatu kabla ya kurejea tena Simba msimu huu.
Akizungumza Dar es Salaam jana wakati wa kutangaza kikosi hicho Poulsen, alisema ameita wachezaji 23 lakini kati yao wawili ni wapya tofauti na waliozoeleka.
“Nimeita wachezaji 23, wakiwemo Costa na Kijiko ambao ni wapya na saba ni wanaocheza soka la kulipwa nchi za nje na waliobaki ni wanaocheza ligi ya ndani, ambapo kambi itaanza Jumapili mchana na jioni ya siku hiyo mazoezi yataanza,” alisema Poulsen.
Akiwazungumzia Costa na Kijiko, alisema Costa amemuona katika mchezo wa Simba na Yanga na mingine ya kirafiki, ambapo kutokana na uwezo aliouonesha na uzoefu wake katika kukaba ameona amjumuishe katika kikosi hicho.
Kwa upande wa Kijiko, alisema alishamuona tangu zamani na hata alipomwambia akachezee timu ya taifa ya vijana, chini ya umri wa miaka 23 dhidi ya Shelisheli alionesha kiwango kizuri.
Wachezaji wengine walioitwa katika kikosi hicho na timu zao kwenye mabano ni makipa Juma Kaseja (Simba), Shaaban Kado (Yanga) na Shaaban Dihile (JKT Ruvu), mabeki ni Shadrack Nsajigwa (Yanga), Idrisa Rajab (SOFAPAKA), Amir Maftah na Juma Nyosso (Simba) na Aggrey Morris (Azam).
Viungo ni Nurdin Bakari (Yanga), Shaaban Nditi (Mtibwa Sugar), Jabir Aziz (Azam), Salum Machaku (Simba), Ramadhani Chombo (Azam), Henry Joseph (Kongsvinger ya Norway) na Nizar Khalfan (Vancouver Whitecaps-Canada) na washambuliaji ni Mrisho Ngassa (Azam), Mbwana Samatta (TP Mazembe), Abdi Kassim ‘Babi’ na Danny Mrwanda (DT Long ya Vietnam), Athuman Machupa (Vasuland) na John Bocco (Azam).
Aliongeza kwamba miongoni mwa wachezaji wanaocheza soka la kulipwa Babi na Mrwanda, hana uhakika kama watakuja kutokana na timu yao inaweza kufanya kama wakati uliopita kwa kuwazuia, lakini waliobaki watafika kwa wakati.
Mchezo huo ni kwa ajili ya kuwania kufuzu kucheza fainali za ya Afrika zitakazofanyika mwakani katika nchi za Guinea ya Ikweta na Gabon.
No comments:
Post a Comment