26 August 2011

Airtel yajitosa Rock City Marathon 2011

Na Mwandishi Wetu

KAMPUNI ya simu za mkononi Airtel Tanzania, imetoa sh. milioni 15 kama udhamini wake katika mashindano ya riadha ya kilomita 21 ya ‘Rock City Marathon 2011’, yatakayofanyika
Septemba 4 mwaka huu Jijini Mwanza.

Akizungumzia fedha hizo Meneja Uhusiano wa kampuni hiyo Jackson Mmbando, alisema udhamini huo ni hatua inayothibitisha jinsi kampuni yake ilivyodhamiria kidhati kuinua michezo mbalimbali nchini.

Alisema pamoja na mambo mengine, Airtel imekuwa na mikakati na programu mbalimbali zinazochangia kukua kwa sekta ya michezo nchini na kwamba riadha ni sehemu ya michezo wanayoona, inastahili kuwekewa nguvu na wadau.

“Wote mnajua tumekuwa na mchango mkubwa nchini katika kuinua michezo mbalimbali na udhamini wetu, katika hili unadhihirisha dhamira ya dhati tuliyonayo katika hili na tutaendelea kufanya hivi kwa kadri uwezo utakavyokuwa unaruhusu,” alisema Mmbando.

Wadhamini wengine ambao tayari wamejitosa katika mashindano ya mwaka huu ni pamoja na  Geita Gold Mine, Kampuni ya Ndege Tanzania (ATCL), New Africa Hotel, Mfuko wa Pensheni wa Taifa (PPF), Mfuko wa Taifa wa Hifadhi ya Jamii (NSSF), Bank M, MOIL, New Mwanza Hotel, Shirika la Hifadhi ya Wanyapori Tanzania (TANAPA) na Bodi ya Utalii Tanzania (TTB).

Naye Mratibu mashindano hayo kutoka Kampuni ya Capital Plus International (CPI), Zaituni Ituja alisema wanaandaa mashindano hayo kwa mara ya tatu mwaka huu na kwamba mbio hizo zitaanzia Uwanja wa CCM Kirumba, kwenda njia tofauti za jiji la Mwanza na kumalizikia katika uwanja huo.

Alisema kuhusu zawadi alisema washindi wa kilometa 21, watapata sh. 500,000 kwa pande zote mbili za wanaume na wanawake, huku atakayevunja rekodi ya mwaka huu ya dakika 59, atapata zawadi ya jumla ya sh. milioni moja na watakaoshika nafasi ya pili watapata sh. 300,000.

Mratibu huyo alisema watakaoshika nafasi ya tatu watapata sh. 200,000 huku nafasi ya nne hadi 12 kila mmoja atapata sh. 90,000 na watakaoangukia katika nafasi ya 13 hadi 50 kila mmoja atapatiwa kifuta jasho cha sh. 30,000 wakati washindi 21 wa mbio za kilometa 5, kilometa 3 kwa walemavu, kilometa 3 za wazee na kilometa 2 kwa watoto watapatiwa sh. 25,000 kila mmoja kama kifuta jasho.

No comments:

Post a Comment