15 August 2011

29 watolea macho kiti cha Rostam

Makada 13 wavaana CCM, 15 CHADEMA
CUF yateua aliyegombea mwaka jana


KINYANG'ANYIRO cha ubunge katika Jimbo la Igunga kimezidi kupamba moto na hadi jana walikuwa wameomba kuwania nafasi hiyo iliyoachwa
wazi na Bw. Rostam Aziz walikuwa 29.

Wakati hali ikiwa hivyo, chama cha NCCR-Mageuzi kimetangaza kutokuweka mgombea Igunga badala yake kuunga mkono wenzao kutoka upinzani lakini kwa sharti kama wataunganisha nguvu.

CUF yateua mgombea

Chama cha CUF kimemtangaza Bw. Leopard Mahona kuwa mgombea wake katika jimbo hilo na kuwa kampeni zao zitajulikana kama 'Operesheni ya chagua Mahona' huku kikitoa onyo kwa vyama vingine vinavyotumia fedha kupata kujipatia ushindi pasipo halali.

Akizungumza na waandishi wa habari Dar es Salaa jana, Naibu Katibu Mkuu Tanzania Bara, Bw. Julius Mtatiro alisema kuwa jina la Bw. Mahona lilipitishwa na Kamati ya Utendaji katika kikao kilichokaa Agosti 7-8, mwaka huu mjini Zanzibar.

Katika uchaguzi uliopita Bw. Mahona alishindana na aliyekuwa Mbunge, Bw. Rostam Aziz kabla ya kujiuzulu hivi karibuni na kupata kura 11,321 dhidi ya 35,674.

Bw. Mtatiro alisema kuwa mgombea huyo ana uwezo mkubwa wa kiutawala na kiu ya kuleta maendeleo, pia anakubalika kwa wananchi wa Igunga.

"Tuna uzoefu mkubwa Igunga, tuna mtandao mkubwa na ndio maana tuna uhakika kabisa wa kuchukua jimbo, pia tulituma vikosi mkakati mapema kuweka sawa mazingira ya ushindi, lakini watalaamu wetu wamefanya utafiti wamebaini kuna baadhi ya vyama vyenye nguvu ya kifedha vinataka kuchakachua matokeo, sisi hatuwezi kukubali hali hiyo," alisema.

Bw. Mtatiro alisema kuwa siasa chafu zenye lengo la kuhujumiana haziwezi kusaidia wananchi na taifa kwa ujumla na pia haziwezi kuondoa umasikini unaowakabili wananchi.

Chama hicho kimemuonya Msajili wa Vyama vya Siasa, Bw. John Tendwa kutowabatiza majina ya ajabu yenye lengo la kukidhoofisha kwenye ushiriki wake katika uchaguzi huo.

Alisema wameshtushwa na kauli ya Bw. Tendwa kuwa CUF  kimezindua kampeni ijulikanayo 'Lolote liwe' huku Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) kikisema 'Chukua jimbo' na Chama cha Mapinduzi (CCM) 'Okoa jimbo.

Bw. Mtatiro alisema kuwa CUF haijazindua kampeni yoyote katika jimbo la Igunga na kwamba 'jina lililotajwa na Bw. Tenda kama kampeni ya chama chao limejaa taswira kadhaa za  kukichafua na kukidhoofisha, kwa kuwa inafahamika ndicho chenye asilimia kubwa ya kushinda'.

NCCR-Mageuzi yakaa kando

Kwa upande wake NCCR-Mageuzi hakitasimamisha mgombea jimboni humo badala yake kinaelekeza nguvu zake kwa 'mgombea mmoja' atakayepitishwa na vyama vya upinzani.

Kauli hiyo ilitolewa Dar es Salaam jana na Katibu Mkuu wa chama hicho, Bw. Samuel Ruhuza wakati akitoa tamko la chama hicho kwa waandishi wa habari kuhusu uchaguzi huo.

Bw. Ruhuza alivitaka vyama vya upinzani vilivyobaki, vitafakari kwa kina na kupata njia muafaka kwa kusimamisha mgombea mmoja ili kuhakikisha ushindi unapatikana bila kujali itikadi za vyama vyao, ili mradi mshindi atoke kambi ya upinzani badala ya kutapakanya kura zao.

Alisema kuwa NCCR-Mageuzi kama chama cha siasa kingependa kushiriki katika uchaguzi huo kutokana na mtandao mzuri uliopo kwenye jimbo hilo, hata hivyo katika utafiti wa kisayansi kimebaini na kujiridhisha kwamba vyama vya upinzani vina nafasi kubwa ya kushinda katika uchaguzi huo kama vitaweka mgombea mmoja.

Alisema kama vyama vyote vya upinzani vitasimamisha mgombea wake kila kimoja, havitashinda na hatimaye kuipa ushindi CCM ambacho kina nafasi ndogo sana ya ushindi.

Alisema kuwa chama chake kimekuwa kikionyesha ushirikiano sana lakini kimekuwa kikiangushwa na vyama vingine na kutolea mfano uchaguzi wa mwaka jana kuwa hawakuona sababu ya kusimamisha wagombea katika majimbo ya Bariadi Mashariki, Karatu, Vunjo na Hai kwa kuamini kwamba vyama pinzani ambavyo vilisimamisha wagombea vitashinda kwa lengo la kuiangusha CCM.

13 wajitokeza CCM

Chama Cha Mapinduzi juzi kilifunga shughuli ya uchukuaji fomu ambapo makada 13 walikuwa wamejitokeza kuwania nafasi iliyoachwa wazi na Bw. Aziz.

Katibu wa NEC, Itikadi na Uenezi, Bw. Nape Nnauye alisema jana kuwa uteuzi wa mgombea wa chama hicho utafanyika Agosti 18, mwaka huu.

CHADEMA wapigana vikumbo

Kwa upande wake, CHADEMA tangu kuanza uchukuaji fomu Agosti 10, mwaka huu mpaka jana asubuhi walikuwa wamejitokeza watu 15 na mwisho wa shughuli hiyo ni kesho.

Akizungumza na Majira jana akiwa katika Kijiji cha Igulubi, Igunga, Mkurugenzi wa Mafunzo na Oganaizesheni wa CHADEMA, Bw. Benson Kigaila alisema kuwa Agosti 17, mwaka huu itakuwa ni siku ya kupitia majina ya waliochukua fomu.

"Siku inayofuata mkutano mkuu wa wilaya utakaa kupiga kura ya maoni, Kamati ya Utendaji ya Wilaya itakutana kufanya uteuzi wa awali, kisha Agosti 20, Kamati Kuu ya chama itafanya uteuzi wa mwisho wa jina la mgombea ubunge," alisema.

Kuhusu hoja ya wapinzani kugawana kura, Bw. Kigaila alisema: "Nakwambia hivi kura za Igunga hazitagawanyika. Hazikugawanyika Tarime. Hazikugawanyika Busanda. Hazikugawanyika Biharamulo na hazitagawanyika Igunga.

"Kama kuna mtu anatumia kigezo cha kura za uchaguzi mkuu mwaka jana, hizo ni takwimu za mezani na za kipuuzi. CCM hapa hawana lao, maana wananchi wana matatizo kibao wamewachoka. CUF kama wanasema mgombea wao alipata kura nyingi, basi wakumbuke Busanda ilikuwaje," alisema.


UPDP yaanza mchakato


Kwa upande wake, UPDP kimetangaza kuwa kiko katika mchakato wa kuweka mgombea katika uchaguzi huo.

Naibu Katibu Mkuu wa chama hicho, Bw. Felix Makuwa alisema kuwa wameshawasiliana na viongozi wa chama chao jimboni humo, na mchakato wa kusimamisha mgombea unaendelea.

"Tunatumia haki yetu kikatiba kama chama cha siasa kilicho hai, nasi tutaingia katika kinyang'anyiro hicho na tuna imani tutafanya vizuri," alisema.

Kwa mujibu wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi uchaguzi jimbo humo kufanyika Oktoba 3, mwaka huu.

Imeandaliwa na Rabia Bakari, Rachel Balama na Peter Mwenda, Benjamin Masese na Tumaini makehe

 

2 comments:

  1. Hii nzuri, Safi Sana. Kuwepo na uigo mpana wa ushindani. Tunasupport Chadema!

    ReplyDelete
  2. chadema waachane watu waamue naomba sana msiwe kama ccm. wagombea wote 15 wapelekwe kwenye mkutano wa wilaya na kura zipigwe na atakaye pata kura nyingi ndiye huyo huyo na hakuna kikao chochote kinachofuata kuamua vinginevyo bila hivyo mtakuwa mmepora demokrasia ya watu ya kuchagua.

    ReplyDelete