01 August 2011

Stars kuanza na Chad Kombe la Dunia

Na Frank Balile


TIMU ya taifa ya Tanzania 'Taifa Stars', itaanza kampeni yake ya kusaka tiketi ya kucheza fainali za Kombe la Dunia mwaka 2014, kwa kucheza na Chad.


Mechi hiyo itakuwa ya awali kabla ya kuingia kwenye Kundi C, itachezwa kati ya Novemba 11 mpaka 15, ambapo ikishinda mechi zote, itasonga mbele kwenye kundi hilo.

Kama Stars itaichapa Chad, itakutana na timu za Ivory Coast, Morocco na Gambia, ambapo mshindi katika kundi hilo, ataungana na washindi wengine wa makundi kucheza hatua inayofuata, kabla ya kwenda nchini Brazil ambako fainali hizo zitapigwa.

Ratiba ya michuano hiyo ilipangwa juzi karibu ba ufukwe wa Copacabana jijini Rio de Janeiro nchini Brazil, ukiongozwa na Katibu Mkuu wa Shirikisho la Kimataifa la Mpira wa Miguu (FIFA), Jerome Valcke.


Stars ni miongoni mwa timu 29, ambazo kwenye viwango vya ubora vya FIFA vya Julai mwaka huu katika Afrika ziko chini ya timu 24 bora, hivyo kulazimika kuanzia hatua hiyo ya kuchujana zenyewe kabla ya kuingia hatua ya makundi ambayo itachezwa kuanzia Juni 1, 2012 hadi Septemba 10, 2013.

Taarifa iliyotumwa na Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) na kusainiwa na Msemaji wake Boniface Wambura, ilisema kwa mujibu wa viwango vya FIFA vya Julai mwaka huu, Tanzania iko katika nafasi ya 127, wakati Chad ni namba 158.

Kwa upande wa Afrika, Tanzania ni namba 33 na Chad 43. Nchi 52 kati ya 53 za Afrika zimeingia katika michuano hiyo ya Kombe la Dunia. Ni Mauritania pekee ambayo haikuthibitisha ushiriki wake.

Timu 10 za juu kwa ubora barani Afrika ambazo zimeongoza makundi 10 ya Afrika katika upangaji ratiba ni Afrika Kusini, Tunisia, Cote d’Ivoire, Ghana, Burkina Faso, Nigeria, Misri, Algeria, Cameroon na Senegal.

Afrika ina nafasi tano kwenye fainali za Kombe la Dunia, huku Ulaya ikiongoza kwa kuwa nazo 13.

Boniface Wambura
Ofisa Habari
Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF)

No comments:

Post a Comment