29 July 2011

TBL yaziremba Yanga, Simba

Na Amina Athumani

KAMPUNI ya Tanzania (TBL) kupitia kinywaji chake cha Kilimanjaro, jana wamezikabidhi vya vya michezo timu za Simba na Yanga kwa ajili ya maandalizi ya Ligi Kuu Bara
itakayoanza mwezi ujao.

Kilimanjaro ndiyo wadhamini wakuu wa timu za Yanga na Simba, walitoa vifaa hivyo vyenye thamani ya sh. milioni 70.

Vifaa hivyo ni sehemu ya mkataba wa timu hizo ni TBL, ambao ni kwa ajili ya ligi msimu ujao.

Akizungumza Dar es Salaam jana wakati wa kukabidhi vifaa hivyo, Meneja wa Bia ya Kilimanjaro, George Kavishe, alisema zikiwa zimebaki siku chache kabla ya kuanza kwa msimu wa ligi kuu,  wameamua kugawa vifaa hivyo ili iwe chachu ya maandalizi kwa timu hizo ambazo zinajiandaa na mechi ya Ngao ya Jamii itakayopigwa Agosti 17, mwaka huu kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.

Alisema kila timu ilikabidhiwa vifaa vyenye thamani ya sh. milioni 35.

Alivitaja baadhi ya vifaa vilivyogawiwa kwa kila timu ni mipira 30, viatu jozi 35, fulana vipande 10 na saa nne za mazoezi.

"TBL ingependa kutangaza tena jinsi tunavyoguswa na michezo nchini  kwa kudhamini klabu kongwe zenye mashabiki wengi nchini," alisema Kavishe

Alisema kampuni yao inaonesha jinsi inavyothamini maendeleo ya soka nchini, na kwamba inawaongezea morali wachezaji.

Katibu Mkuu wa Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF),  Angetile Osiah, aliipongeza kampuni hiyo kwa kutimiza sehemu ya masharti ya mkataba wao kwa kutoa vifaa mapema ili timu zijiandae.

"Sisi kama TFF tunaipongeza TBL kwa kuona umuhimu wa kuvitoa mapema vifaa, hii itakuwa chachu kwa timu zetu kuweza kufanya vizuri zaidi ya hapo na pia tunazipongeza Simba na Yanga kwa kuweza kuwashawishi TBL kuendelea kuwa nao kama hivi," alisema.

Bila kujali itikadi zao za upinzani wa jadi, wawakilishi wa timu hizo waliishukuru TBL kwa kuendeleza uhusiano mzuri wa muda mrefu.

 Ofisa Habari wa Yanga, Louis Sendeu alisema vifaa hivyo ni chachu kwao kuendeleza ubingwa.

Kwa upande wake Makamu Mwenyekiti wa Simba, Godfrey Nyange 'Kaburu', alisema wataendelea kuheshimu mkataba huo na kuvitumia vifaa hivyo kama ilivyopangwa na kwamba wataendeleza ushindani ili waweze kukaa kileleni kama ilivyokuwa msimu wa miaka ya nyuma.

Yanga walitwaa ubingwa wa Ligi Kuu Bara msimu wa 2010/2011.

No comments:

Post a Comment