Na Frank Balile
SERIKALI kupitia Wizara ya Mambo ya Ndani inawahoji wachezaji 13 wa timu ya soka ya Red Sea ya Eritrea, baada ya kujisalimisha wizarani hapo mwishoni mwa
wiki na kuomba hifadhi ya ukimbizi.
Kwa mujibu wa taarifa ya wizara hiyo iliyosainiwa na Msemaji wa wizara hiyo Isaac Nantanga, wachezaji hao waliokuwa wakishriki kwenye michuano ya Kagame Castle Cup, walishindwa kusafiri na wenzao Julai 9, mwaka huu.
Mara baada ya kikosi hicho kuondoshwa hatua ya robo fainali ya michuano hiyo, walitakiwa kuondoka Julai 9, mwaka huu kwa kutumia ndege ya Shirika la Ndege la Kenya kwenda kwao, lakini hawakutokea Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere Dar es Salaam.
Mahojiano hayo yanayofanywa na wizara hiyo kupitia Idara ya Wakimbizi ni utaratibu unaoelekezwa kufuata sheria za nchi na za kimataifa kuhusu watu wanaoomba hifadhi.
Taarifa hiyo ilisema, baada ya mahojiano hayo ambayo yalitarajiwa kukamilika jana, zitafuata taratibu nyingine kuhusu maombi ya wachezaji hao.
Nantanga katika taarifa yake, alisema mahojiano ya awali yanayofanywa ni kwa ajili ya kujua sababu zilizowafanya wachezaji hao kushindwa kurejea kwao, na kuziangalia kama zinaweza kuwapa hadhi ya ukimbizi kutokana na sheria za kitaifa na kimataifa.
Taarifa hiyo ilisema wachezaji hao kwa sasa wanahifadhiwa na Shirika la Umoja wa Mataifa la Kuhudumia Wakimbizi (UNHCR).
Pia, hati za kusafiria za wachezaji hao zinashikiliwa na Idara ya Uhamiaji.
Katika michuano ya Kagame, timu ya Red Sea ambao ni mabingwa wa Eritrea ilifanikiwa kucheza hatua ya robo fainali dhidi ya Yanga na kufungwa changamoto ya mikwaju ya penalti 5-4.
Kikosi hicho kilishika nafasi ya pili katika Kundi A lililoongozwa na Simba, Vital'O ya Burundi, Etincelles ya Rwanda na Ocean View ya Zanzibar. Yanga ilitwaa ubingwa wa michuano hiyo.
No comments:
Post a Comment