13 July 2011

...Kutesa U/Taifa Ligi Kuu

Na Zahoro Mlanzi

SAA chache baada ya Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) kuzitaka klabu ambazo hazijawasilisha majina ya viwanja watakavyotumia kwa ajili ya Ligi Kuu Bara
ikiwemo Yanga, mabingwa hao wa Bara na Afrika Mashariki na Kati, wamepanga kuiomba serikali kutumia Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.

Mbali na Yanga, klabu nyingine ambazo mpaka sasa hazijaweka wazi viwanja watakavyotumia ni Simba, Moro United, Villa Squad, JKT Ruvu na African Lyon.

Timu hizo zimeathirika na marekebisho yanayoendelea Uwanja wa Uhuru, Dar es Salaam, ambapo hutumia kama uwanja wao wa nyumbani na kwamba kuna uwezekano mzunguko wa kwanza ukamalizika uwanja huo ukawa haujakamilika.

Akizungumza na gazeti hili muda mfupi baada ya Ofisa Habari wa Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF), Boniface Wambura kuzungumzia suala hilo, Katibu Mkuu wa Yanga, Selestine Mwesigwa, alisema mpaka jana hawajui ni uwanja upi watakaoutumia kwa ajili ya ligi hiyo.

"Tatizo hatujui Uwanja wa Uhuru utamalizika lini, lakini mpango wetu wa awali, kama Uhuru ukishindikana tutazungumza na wizara ili tuone uwezekano wa kuutumia Uwanja wa Taifa," alisema Mwesigwa.

Alisema ana imani sasa hivi serikali itawaelewa ndio maana wataanza mapema kuzungumza nao ili kujua kitakachoendelea.

Alipotafutwa Katibu Mkuu wa Simba, Evodius Mtawala kuzungumzia suala hilo, simu yake ya kiganjani iliita zaidi ya mara tano bila kupokelewa.

Mapema kabla ya kuulizwa Yanga suala hilo, Wambura alisema wanazikumbusha timu zote za Ligi Kuu kuwasilisha majina ya viwanja ambavyo zitatumia kwa ajili ya ligi kuu itakayoanza Agosti 20, mwaka huu.


Alisema mpaka jana klabu zilizowasilisha maombi ya viwanja watakavyotumia ni Mtibwa Sugar
(Manungu), Azam FC (Chamazi), Ruvu Shooting Stars (Mlandizi), Coastal Union (Mkwakwani) na Toto Africans (CCM Kirumba).

Nyingine ni Oljoro JKT (Sheikh Amri Abeid), Polisi Tanzania (Jamhuri, Dodoma) na Kagera Sugar (Kaitaba).

Alisema klabu za Yanga, Simba, Simba, Moro United, Villa Squad, JKT Ruvu na African Lyon bado hazijafanya hivyo na kuzitaka zitume majina ya viwanja vyao haraka, kwani kabla ya kuruhusiwa kutumika ni lazima vithibitishwe na Kurugenzi ya Ufundi ya TFF.

Katika hatua nyingine, Wambura alisema kipindi cha uhamisho wa wachezaji kwa msimu wa mwaka 2011/2012 kinamalizika Julai 15, mwaka huu, wakati mwisho wa usajili ni Julai 20, mwaka huu.

Alisema kwa upande wa klabu za Ligi Kuu, usajili wao unaanzia kwa timu za pili (U-20), hivyo zinatakiwa kukabidhi usajili wa timu hizo kwanza na baadaye za timu zao za kwanza.

Aliongeza kwamba, klabu zote za ligi kuu tayari zina namba za siri kwa ajili ya kufanya usajili wa wachezaji wa kigeni na dirisha dogo la usajili litafunguliwa tena Novemba 1 hadi 30 mwaka huu.

2 comments:

  1. Mwaka jana uwanja wa uhuru ulifungwa kwa maandalizi ya kuapishwa Raisi na mwaka huu inajulikana ni mpk 9 Desemba maadhimisho ya Uhuru miaka 50 kwa hiyo kwisha kwake na kuanza kuutumia ni baada ya sherehe za Uhuru.Kuwe na uwanja mbadala pale Jangwani au ule wa Karume uboreshwe uwe wa kisasa kiasi na kuwekwe viti,matatizo ya kutegemea uwanja huu ni kero, au kila Klabu ijitahidi kumaliza viwanja vyao na uwe kwa kimataifa kama unavyoonekana na utakavyokuwa wa AZAM

    ReplyDelete
  2. Ni kweli huu wakati wa timu kujikakamua na kuwa na uwanja wake.Pia namshangaa mwesigwa kusema yeye anaanza mapema kuzungumza na wizara kuutumia uwanja wa taifa wakati wahusika wanalijua hilo na ndio maana kila timu imeshapewa taarifa ya kutafuta kiwanja mbadala.Mwesigwa ongea kama mtu aliyekwenda shule.

    ReplyDelete