13 July 2011

CHANETA kutangaza kikosi cha Taifa hivi karibuni

Na Amina Athumani

CHAMA cha Netiboli Tanzania (CHANETA), kinatarajia kutangaza timu ya Tanzania itakayoshiriki michuano ya Mataifa ya Afrika mara baada ya kumalizika kwa
mashindano ya Klabu Bingwa Tanzania, Jumamosi.

Akizungumza kwa njia ya simu kutoka jijini Arusha kwenye michuano hiyo inayofanyika katika Uwanja wa Shekh Amri Abeid, Mwenyekiti wa CHANETA, Anna Bayi alisema, maandalizi ya timu hiyo yatafanyika mara baada ya kumalizika kwa michuano hiyo.

"Kwa sasa tunaangalia kwanza wanamichezo kupitia mashindano haya ya Klabu Bingwa ambayo kwa kiasi kikubwa, yamekuwa na upinzani mkubwa kutoka katika timu shiriki," alisema Anna.

Alisema kwa sasa timu ya taifa na kambi vimevunjwa, lakini baada ya mashindano watatangaza kikosi cha taifa kitakachokuwa wa Bara na  Zanzibar.

Alisema kutokana na timu ya Taifa kuchaguliwa kupitia mashindano mbalimbali, ana imani mashindano hayo yatasaidia kupatikana kikosi bora.

Anna alisema fainali ya michuano hiyo itachezwa Jumamosi, baada ya kuzishirikisha timu 16 katika michuano hiyo iliyoanza kuchezwa Julai 3, mwaka huu.

CHANETA ni chama kimojawapo kitakachopeleka timu kwa mara ya kwanza kwenye michuano ya Mataifa ya Afrika, ikiwemo timu ya soka ya wanawake ya Twiga Stars.

No comments:

Post a Comment