Na Humphrey Shao
JESHI la Polisi limefanikiwa kukamata watuhumiwa sita waliokuwa wakijiusisha na uuzaji wa tiketi bandia, katika mchezo wa fainali ya Kombe la Kagame uliozikutanisha
timu za Simba na Yanga.
Hayo yameelezwa na Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kipolis Temeke, David Misime alipokuwa akizungumza na wandishi wa habari jijini Dar es salaam jana.
Kamanda Misime alisema mbali na tiketi hizo feki, pia askari wake walifanikiwa kuwatia hatiani watu tatu ambao walikuwa wanafanya biashara ya ulanguzi wa tiketi kwa kuuza kinyume na bei, ambayo ilipangwa na TFF.
"Watuhumiwa wote wapo katika kituo cha Polisi cha Chang'ombe na watafikishwa katika Mahakama ya Wilaya ya Temeke kwa ajili ya kujibu tuhuma zinazowakabili," alisema Misime.
Alisema mashindano ambayo yalimalizika juzi kwa Yanga kutwaa ubingwa, yalifanyika kwa usalama zaidi kuliko mashindano yoyote na yamekuwa na mafaniko makubwa katika suala la usalama.
Pia aliwapongeza mashabiki wa timu zote mbili kwa utulivu waliounesha na kusema kuwa sasa mashabiki wengi wameelimika na wanafahamu nini maana ya ushabiki, kwani imekuwa tofauti na miaka ya nyuma ambapo mechi kama hiyo ikimalizika kunakuwa na matukio ya ajabu.
Alisema licha ya eneo hilo umeme kutoweka kwa takribani dakika 40, lakini hakuna kitu kibaya ambacho kilitokea na kuwaathiri watu.
No comments:
Post a Comment