12 July 2011

Kazimoto kukaa nje mwezi mmoja

Na Zahoro Mlanzi

KIUNGO wa timu ya taifa 'Taifa Stars' na Simba, Mwinyi Kazimoto yupo hatihati kucheza mchezo wa Ngao ya Jamii utakaopigwa Agosti 13, mwaka huu dhidi ya Yanga baada ya
kuumia juzi na kupewa mapumziko ya mwezi mmoja.

Kazimoto aliyejiunga na Simba akitokea JKT Ruvu aliumia kifundo cha mguu katika mchezo wa fainali wa mashindano ya Kagame Castle Cup, ambapo timu yake ililala kwa bao 1-0 dhidi ya Yanga.

Baada ya kuumia, mchezaji huyo alitolewa nje kwa machela na baadaye alikwenda kupatiwa huduma ya kwanza ambapo alirudi kukaa benchi la wachezaji la akiba dakika tano kabla ya mchezo huo kumalizika huku mguuni kwake alionekana kufungwa barafu.

Akizungumza na gazeti hili Dar es Salaam jana, mmoja wa makocha wa timu hiyo, Abdallah Kibadeni 'King' alisema mara baada ya kumalizika kwa mchezo huo wa fainali, walimpeleka hospitali kumfanyia uchunguzi zaidi.

"Kiukweli aliumia vibaya licha ya wakati ule unaweza kuona kama ameumia kidogo lakini kwa mujibu wa daktari wetu amesema atakaa nje ya uwanja kwa mwezi mmoja akiuguza majeraha yake," alisema Kibadeni.

Alisema mwezi huo mmoja umeanza tangu jana na kwamba mpaka Agosti 9 ndipo watakapokwenda kuangalia tena maendeleo yake na baada ya hapo ndipo atakapoweza kuanza mazoezi.

Kuumia kwa kiungo huyo katika mchezo wa juzi, pengo lake lilionekana licha ya kuingia Mohamed Banka kwani kwa dakika alizocheza ni dhahiri alionesha kiwango cha juu.

Kazimoto mchezo huo ndiyo wa kwanza tangu idaiwe amesajiliwa na timu hiyo ambapo katika mashindano hayo ameingizwa katika dakika za mwisho lakini hata hivyo hakuwa na bahati kumalizia mchezo huo.

No comments:

Post a Comment