05 July 2011

Wataka uchunguzi Barabara ya Kilwa uharakishwe

Na Godfrey Ismaely

WANANCHI wa Mkoa wa Dar es Salaam wameitaka Wakala wa Barabara (TANROADS) mkoani humo kuharakisha uchunguzi wa barabara ya Kilwa ili hatua za haraka
ziweze kuchukuliwa dhidi ya  mkandarasi na watendaji wa serikali wanaohusika.

Wakizungumza na Majira kwa nyakati tofauti juzi na jana, wananchi hao walisema wana shaka kuwa iwapo Waziri wa Ujenzi Dkt. John Magufuli, hatasimamia suala kwa karibu zaidi uenda uchunguzi unaoendelea kutofanyika kwa ufanisi.

Walisema kimsingi wanakubaliana na kumpongeza Dkt. Magufuli kukataa kupokea barabara hiyo iliyojengwa chini ya kiwango lakini kunahitajika umakini zaidi katika hatua za uchunguzi kwa kuwa uenda baadhi ya watendaji wa serikali wanahusika baada ya kurubuniwa.

"Hata kama hii barabara ilijengwa kwa msaada na watu wa Japan huu siyo ujenzi kabisa, ni bora kupoteza muda kupata uhakika, umakini zaidi unahitajika katika uchunguzi unaoendelea," alisema Bw. Exaverine Thomas mkazi wa Mbagala Zakhiem Manipaa ya Temeke.

Kwa wake Bi. Evaline Martin, mkazi wa Mtoni Sabasaba alisema maamuzi ya Waziri Magufuli kukataa makabidhiano ya barabara hiyo yalikuwa na nia njema na inayofaa kupongezwa ingawa bado jitihada zaidi zinahitajika kujua ukweli.

"Uchunguzi siyo jambo la kawaida, umakini unahitajika zaidi kabla ya kupata takwimu za awali na hata zinazofanya tathimini kwa kuwa wasipofanya hivyo tutakuwa tunadangayana tu," alionya Bi. Martin.

Naye Bw. Elias Gorge, mkazi wa Mtoni Mtongani alisema serikali na hata wahisani wamelenga kuwaimarisha miundombinu lakini kwa mtazamo wake baadhi ya wakandarasi siyo waaninifu.

Majira ilipomtafuta Meneja wa TANROADS Mkoa wa Dar es Salaam Bw. James Nyakabari, kupata ufafanuzi juu ya lini uchunguzi huo utakamilika na barabara hiyo kukabidhiwa alisema panahitajika muda kwa kuwa uchunguzi bado unaendelea.

"Siwezi kulizungumzia hilo kwa sasa ila ninachofahamu ni kwamba barabara ya Kilwa inahitaji muda kabla ya makabidhiano kwa kuwa ipo katika hatua za uchunguzi," alisema Bw. Nyakabari.

Mwanzoni mwa mwezi Mei akiwa katika ziara ya  kukagua miundombinu mbalimbali, Waziri Dkt.  Magufuli, aliamua kuisusia barabara hiyo  baada ya kugundua imejengwa chini ya kiwango.

Kampuni iliyojenga barabara hiyo ni Kajima kutoka Japan.Waziri Dkt. Magufuli pia alitaka uchunguzi ufanyike mara moja ili hatua zaidi zichukuliwe.

Kupitia mwito huo mwishoni mwa mwezi Juni mwaka huu TANROADS walitangaza kuwa tayari uchunguzi ulianzia eneo la Bandari hadi Mbagala Rangi Tatu shughuli inayotarajiwa kufikia mwisho Julai 19 mwaka huu kabla ya kukabidhi ripoti hiyo Wizarani.

No comments:

Post a Comment