05 July 2011

Pinda aipa PPF mtihani kuhusu elimu

Na Gladness Mboma

WAZIRI Mkuu Mizengo Pinda, ameushauri Mfuko wa Pensheni kwa Watumishi wa Umma (PPF), kuangalia uwezekano wa kutoa mafao ya elimu kwa watoto wa
wanachama wa mfuko huo waliofariki hadi kidato cha sita badala ya kuishia kidato cha nne.

Waziri Mkuu alisema hayo jana wakati alipotembelea jengo la PPF katika Maonyesho ya 35 ya Kimataifa ya Biashara yanayoendelea katika Viwanja vya Mwalimu Nyerere
Sabasaba Dar es Salaam.

Ushauri huo ulikuja baada ya Bw. Pinda kuonana na mwanafunzi wa darasa la tano Ernest Mwinchumu (10), ambaye anasomeshwa na mfuko huo baada ya baba yake Bw. Julius Mwinchumu, ambaye alikuwa mfanyakazi wa Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO) kufariki dunia.

"Ninaupongeza sana mfuko huu kwa kubuni  mpango huu wa utoaji wa mafao ya elimu, utasaidia watoto ambao wazazi wao wamejiunga na mfuko huo, huyu mtoto anavyofaidika ameanza kusomeshwa toka akiwa chekechea na ataendelea
kusomeshwa hadi kidato cha nne, jambo hili ni zuri.

"Huyu mtoto msimwache aishie kidato cha nne pekee, atakuwa mtu wa kutangatanga, angalieni utaratibu wa kumsomesha hadi kidato cha sita ili kumwekea msingi imara,"alisema.

Alisema wazazi wa kiume hasa wanapofariki wanawake wanaangaika na watoto lakini kama atafariki akiwa amejiunga na mfuko huo utamsaidia kama ulivyo kwa mtoto Ernest.

Naye Ofisa Uhusino wa PPF, Bi. Lulu Mengele, alisema mfuko huo unasomesha zaidi ya watoto 1,300 ambao wazazi wao ni wanachama katika shule mbalimbali nchini mpango ambao ulianza tangu mwaka 2003.

Alisema baba wa mtoto huyo alikuwa mwanachama wa PPF na alifariki mwaka 2009 na alikuwa mfanyakazi wa TANESCO na kwamba mke wake Bi. Rachel Mwinchumi, kwa sasa anafidi mafao ya aina tatu ambayo ni mafao ya kifo, utegemezi na elimu.

Alisema ushauri wa Waziri Mkuu kutaka waendelee kusomesha watoto hao hadi kidato cha sita utaangaliwa na kufanyiwa kazi na kwamba wazazi wengi wamefurahishwa na utaratibu huo.

No comments:

Post a Comment