Na Rehema Mohamed
UPANDE wa Jamhuri katika kesi ya wizi ya sh. bilioni 2.2 katika Akaunti ya Madeni ya Nje (EPA) Benki Kuu ya Tanzania, (BOT), imeiomba Mahakama ya Hakimu Mkazi
Kisutu kuwaona washitakiwa wa kesi hiyo kuwa na kesi ya kujibu.
Washtakiwa katika kesi hiyo ni Mweka Hazina wa Chama cha Mapinduzi (CCM), Mkoa wa Kigoma, Bw.Rajabu Maranda, na ndugu yake, Bw. Farijala Hussein.
Ombi hilo lilitolewa jana mahakamani hapo na wakili wa serikali Bi. Arafa Msafiri, mbele ya jopo la mahakimu likiongozwa na hakimu Bi.Fatma Masengi, wakati kesi hiyo ilipofikishwa mahakamani hapo kwa ajili ya upande wa mashitaka kufanya majumuisho.
Bi.Msafiri alidai kuwa upande wa mashitaka umethibitisha mashitaka yote saba wanayotuhumiwa nayo washitakiwa kulingana na ushahidi uliotolewa mahakamani hivyo wanaiomba mahakama hiyo ione kuwa washitakiwa wote wana kesi ya kujibu.
Akianza na uthibitisho wa shitaka la pili la kufoji nyaraka ikiwemo hati ya usajili wa jila la biashara la kampuni ya Money Planners, wakili huyo alidai wamethibitisha kwa ushahidi uliotolewa na Msajili Msaidizi wa BRELA Bw.Noel Shani.
Alisema Msajili huyo msaidizi alisema hazitambui nyaraka hizo kwa kuwa yeye alihusika katika usajili wa kampuni halali yenye jina hilo.
Ushahidi mwingine ni maelezo ya onyo ya mshitakiwa wa pili Bw. Hossein kuwa alijaza fomu hizo kwa majina ya uongo aliyopewa na mshitakiwa wa kwanza.
Katika shitaka la tatu la kuwasilisha nyaraka hizo katika benki ya United Bank of Afrika (UBA) kwa ajili ya kufungua akaunti ili kujipatia ingizo kutoka BoT alidai tuhuma hiyo wameithibitisha kwa ushahidi uliotolewa na mtaalam wa maandishi.
Alisema, pia maelezo ya onyo ya mshitakiwa wa pili ambaye alisema walikubaliana wapeleke benki nyaraka hizo kwa ajili ya kazi hiyo ni uthibitisho kuwa watuhumiwa wana kesi ya kujibu.
Shitaka la nne la kufoji nyaraka ya makubaliano ya kukabidhiana deni kati ya kampuni ya B.C and Grancel ya Ujerumani na kapuni ya Money Planner and Consultancy, alidai ushahidi wa mazingira unaonesha ilifojiwa na walijipatia zaidi ya sh.bilioni 2.2
Shitaka la tano la kuwasilisha nyaraka hiyo BoT kwa ajili ya kujipatia fedha hizo alidai wamelithibitisha kutokana na maelezo ya mshitakiwa wa kwanza ambaye alisema kuwa ndiye aliyeziwasilisha.
Katika shitaka la sita la wizi wa zaidi ya sh.milioni 660 alidai kuwa kwa jinsi washitakiwa walivyoghushi nyaraka mbalimbali na kuziwasilisha BoT na hatimaaye kujipatia fedha washitakiwa wameidanganya chombo hicho cha fedha nhivyo malipo hayo yalifanyika chini ya udanganyifu.
Hata hivyo wameiomba mahakama kama itaona kuwa washitakiwa hawataguswa na kosa la wizi basi ione kuwa wamejipatia fedha hizo kwa njia ya udanganyifu.
Shitaka la saba la kujipatia fedha zaidi ya sh.bilioni 2.2 kwa njia ya udanganyifu ambapo pia Bi.Msafiri ameiomba mahakama ione washitakiwa wana kesi ya kujibu kutokana na ushahidi uliotolewa awali.
Katika shitaka la kwanza kula njama ya kutenda kosa Bi.msafili alidai wamethibitisha shitaka hilo kutokana na ushahidi wa makosa mengine ulioonesha wazi kuwa toka awali washitakiwa walipanga njama ya kuiibia BoT.
Akitoa mfano, wakili huyo alidai maelezo ya onyo ya washitakiwa wote ambayo walisema kuwa walikubaliana kupanga anwani ya kampuni yao ambayo ni Magomeni Mapipa, pia walishauriana kufungua akauti,usajili wa jina la kampuni na mengineyo ambavyo vinathibitisha walikula njama.
Baada ya kumaliza kutoa maelezo hayo, Hakimu Masengi alisema mahakama itatoa uamuzi wake Julai 18 mwaka huu kama washitakiwa wana kesi ya kujibu au la.
No comments:
Post a Comment