29 July 2011

Wataalam wa Shoulinj Kempo kuwasili Agosti

Na Salim Nyomolelo

WACHEZAJI wa mchezo wa Shoulinj Kempo ambao asili yake nchini Japan, wameanza maandalizi ya kupokea wageni kutoka Japan wanaotarajiwa kusaili nchini
mwezi ujao.

Wageni hao watafika nchini kuangalia maendeleo ya mchezo huo.

Akizungumza na Majira jana, Mwalimu wa mchezo huo juu kensh, Omary Mohamed, alisema maandalizi ya kuupokea ugeni huo, yameshaanza na wapo katika hatua za mwisho za kutafuta ukumbi.

Alisema mipango yao ni kutumia ukumbi wa hoteli ya Starlight ya jijini Dar es Salaam.

Alisema madhumuni makubwa ya wataalam hao wa mchezo huo, ni kujenga uhusiano na kukuza mchezo huo nchini.

Alisema watasaidia kutoa mafunzo ya mbinu mbalimbali za kujihami na kutoa mitihani kwa wachezaji wa ngazi za mkanda mweusi.

"Tunategemea wachezaji mbalimbali wa mchezo huu kushiriki kuupokea ugeni huu, na pia kufanya maonesho ya mchezo huu," alisema Omary

Omary alisema maonesho hayo yatakuwa tendo ambalo litafanyika Agosti 28, mwaka huu.

Alisema wachezaji wote watafanyiwa semina ili waweze kutambua umuhimu na malengo ya shoulinj kempo.

Alisema wageni hao watafika nchini mapema Agosti ili waweze kupata muda wa kutoa mafunzo mbalimbali, kuwaandalia mitihani na kufahamiana kabla ya kufanya maonesho .

"Tunawakaribisha watu wote kushuhudia mchezo huu wa kujihami na hakutakuwa na kiingilio, lengo letu ni kutoa burudani kwa umma ili waone mbinu mbalimbali za kujihami," alisema.

Alisema mbali na kujihami,  mchezo huo hufundisha watu mazingira mbalimbali ya kuishi na jamii katika kudumisha upendo, amani na afya.

No comments:

Post a Comment