29 July 2011

Jahazi Modern kutesa Morogoro leo

Na Mwandishi Wetu

BENDI ya muziki wa taarab ya Jahazi Modern 'Wana wa nakshi naksi', kesho watafanya onesho maalumu mkoani Morogoro lijulikanalo kwa jina la Uwongo wa Mwisho wa
mwezi, kwenye ukumbi wa hoteli ya Savoi.

Akizungumza jijini Dar es Salaam, Mkurugenzi wa bendi hiyo, Mzee Yusuph, alisema   onesho hilo ni muhimu kwa wakazi wa mkoa huo na zawadi kwao kutokana na ushirikiano mkubwa wanaotoa kwa kundi hilo linapokuwa mkoani humo.

Yusuph alisema mbali ya kutambulisha nyimbo mpya, pia watapiga nyimbo zao zote kali za zamani na kutoa fursa kwa mashabiki kuchagua nyimbo wanazotaka.

Alizitaja baadhi ya nyimbo za zamani zinazotamba mpaka sasa ni VIP, My Valentine, Daktari wa Mapenzi, Langu Rohoni na Nilijua Mtasema.

“Wimbo mpya tutakaowapa mashabiki wetu wa Morogoro ni Surprise, nina imani wataupenda sana,” alisema.

Alisema wamejiandaa vilivyo na onesho hilo ambalo litasindikizwa na kundi la Khanga Moja ndembe ndembe, ambao ni mabingwa wa minenguo nchini.

“Hii ni zawadi kwa wakazi wa Morogoro na vitongoji vyake, tumeamua kufanya shoo ya nguvu ambayo itaweka historia mkoani humo,” alisema Yusuph.

No comments:

Post a Comment