05 July 2011

Upinzani wataka Chenge abanwe kwa rada

Na Grace Michael, Dodoma

KAMBI ya Upinzani Bungeni, imeitaka Serikali kuwachukulia hatua za kinidhamu na kisheria kwa kuwafikisha mahakamani haraka iwezekanavyo waliohusika na
ununuzi wa rada akiwemo Mwanasheria Mkuu wa serikali wa kipindi hicho.

Mbali na hilo, Kambi hiyo ilipinga fedha za rada kulipwa kupitia serikalini kwa kuwa serikali haiaminiki na hasa ikizingatiwa kuwa fedha hizo zilipotelea mikononi mwa serikali yenyewe.

Ingawa haikumtaja jina, aliyekuwa Mwanasharia Mkuu wa Serikali wakati huo ni Bw. Andrew Chenge ambaye kwa sasa ni Mbunge wa Bariadi Magharibi.

Mapendekezo hayo yalitolewa bungeni jana na Msemaji wa Kambi ya Upinzani, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma, Bi. Sazan Lyimo wakati akiwasilisha hotuba ya bajeti ya wizara hiyo ya mwaka 2011/2012.

"Kambi ya upinzani tunaona kuwa bila watuhumiwa hawa kuchukuliwa hatua, ni dhahiri kuwa taifa haliwezi kuwa na uhakika wa kuzilinda vizuri fedha hizo za rada pindi zikilipwa pamoja na fedha zingine za umma ambazo zinaendelea
kupotea kwa kuwa umekuwa ni utamaduni wa serikali kutochukua hatua,” alisema B. Lyimo.

Aidha walipinga nia ya Kampuni ya BAE ya kutaka kulipa fedha hizo kupitia Asasi zisizo za kiserikali za Uingereza kwa kuwa hatua hiyo itakuwa ni udhalilishaji mkubwa kwa Watanzania wote kwamba hawana uwezo wa kuamua na kusimamia mambo yake.

“Tunataka Bunge lako tukufu lijadili na liazimie kuanzishwa kwa akaunti ya muda ya fedha za rada, itakayosimamiwa kwa pamoja na wawakilishi wa Asasi zisizo za kiserikali za Tanzania, wawakilishi wa sekta binafsi na mwakilishi wa serikali na tunataka fedha hizi zilipwe haraka iwezekanavyo kupitia akaunti hiyo,” alisema Bi. Lyimo.

Kambi hiyo pia iliomba bunge lichukue wajibu wa kujadili na kuamua kipaumbele cha matumizi ya fedha hizo chini ya usimamizi wa akaunti hiyo kwa kuzingatia zaidi maslahi ya wengi kadri fedha hizo zitakavyoonekana kutosha.

Aidha azimio hilo limpe mamlaka Mkaguzi na Mdhibiti Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) kukagua matumizi ya fedha hizo kama anavyofanya kwa fedha nyingine za umma.

Fedha zinazotakiwa kulipwa na BAE ni takribani sh. bilioni 75.2 za Tanzania ambazo kampuni hiyo, iliamriwa kuzilipa baada ya kubaini kuwepo ukiukwaji mkubwa wa sheria na taratibu katika ununuzi wa rada hiyo.

Akizungumzia suala la matumizi mabaya ya fedha za umma, Bi. Lyimo alisema kuwa kutokana na kitendo cha serikali kulipa mishahara kwa wafanyakazi hewa na kusababisha kupoteza kiasi cha sh. bilioni 26.6, aliomba ufanyike uchunguzi wa kina na wahusika wote waliofanikisha wizi huo wachukuliwe hatua haraka.

Kambi hiyo, pia iliitaka serikali kujieleza kwa nini ilitumia mabilioni ya fedha za walipa kodi kujenga nyumba za kuishi watumishi wa serikali na baadaye kuziuza.

“Wakati nyumba hizi zikiuzwa, baadhi ya mawaziri wanakaa hotelini huku gharama ya siku ikiwa ni sh. 500,000 hadi 600,000, ina maana kiongozi mmoja aliyekaa hotelini tangua aapishwe atakuwa ametumia sh. milioni 110.2, je, serikali
imechukua hatua gani dhidi ya viongozi waliouza nyumba hizo?” alihoji Bi. Lyimo.

Kambi hiyo pia ilizungumzia taasisi za wake wa marais ambapo ilisema kuwa uanzishwaji wa taasisi hizo unaleta picha mbaya kuwa zinaanzishwa kwa maslahi binafsi zaidi kuliko kusaidia jamii.

Alisema kuwa ipo haja kwa serikali kuandaa utaratibu rasmi wa kuwa na taasisi moja tu yenye nguvu itakayoongozwa na mke au mume wa rais aliye madarakani kama mlezi na kupokewa na wake au waume wa marais wajao, na hii itaondoa picha mbaya ya kila mmoja kujianzishia taasisi au mfuko wake.

3 comments:

  1. Ni vizuri serikali ikajua kwamba bila wahalifu wa ufisadi kufikishwa mahakamani kwa dhati hali itakuwa ngumu sana. Angalia nchi za kiarabu. Kiongozi kushindwa kuchukua hatua kwa manufaa ya nchi unajiingiza kwenye tatizo na iko siku utakamatwa na kuhojiwa.
    Shukrani kwa People's Power Party

    ReplyDelete
  2. Mimi naomba wabunge wa upinzani wamtumie hii habari Leonie Foster wa BAE system (Email yake inapatikana kwenye website ya BAE) ili wafahamu kwamba Watanzania kweli tumedhamilia pesa hii isirudishwe serikalini kwasababu serikali haiaminiki.

    Please wabunge wa upinzani fanyeni hima time is no longer our side. Membe na team yake washidwe hadi walegee mpaka watakapotueleza wamefanya nini kuhusu hawa watuhumia wa ufisadi, ingawa ninasikia serikali ya CCM iko tayari kuzikosa hizo pesa kuliko kuwachukulia hatua Chenge, Idrissa Rashid and co.

    ReplyDelete
  3. Inasemekana mwanasheria mkuu wa serikali kipindi hicho alichangia huu ubadhirifu, kumbe vile vijisent ndo 10% ya RADA, huyu jamaa sijui haoni aibu au vip, kila siku kashfa mara unga bungeni, mara kuua kwa bajaji, RADA nk... serakiali inakaa kimya sjui wana mikakati gani.. Nawaambia hivi siku ya mwisho wananchi ndo watakuwa majaji.

    ReplyDelete