05 July 2011

Mishahara juu

*Serikali yapandisha kwa asilimia 40

Na Grace Michael, Dodoma

SERIKALI imetangaza kurekebisha mishahara ya watumishi wake kwa asilimia 40.2 kwa kuzingatia uwezo wake wa bajeti, makubaliano yaliyofikiwa na
Baraza la Majadiliano ya Pamoja na kukabiliana na kasi ya mfumuko wa bei.

Kutokana na hatua hiyo, fungu la mishahara limeongezwa kwa sh bilioni 938, sawa na ongezeko la asimilia 40.2 ya fedha zilizotengwa kugharamia mishahara mwaka jana.

“Kiasi hiki cha fedha kwa ajili ya kulipa mishahara kimeongezeka kwa sh. bilioni 938 ambayo ni sawa na ongezeko la asimilia 40.2 ya fedha zilizotengwa kugharamia malipo ya malipo hayo kwa mwaka wa fedha 2010/2011,” alisema Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais Menejimenti ya Utumishi wa Umma, Bi. Hawa Ghasia wakati akiwasilisha hotuba ya bajeti ya ofisi yake ya mwaka 2011/2012.

Katika mwaka wa fedha 2011/2012 serikali inatarajia kutumia sh. trilioni 3.2 kwa ajili ya malipo ya mishahara, upandishwaji vyeo na kulipa madai ya malimbikizo mapunjo ya mishahara kwa watumishi wa Serikali Kuu, Serikali za Mitaa, Wakala na Taasisi za Serikali.

Mbali na hayo, alisema kuwa katika mwaka huu wa fedha, serikali inatarajia kuajiri watumishi wapya 64,024 ambapo kipaumbele kitakuwa katika sekta ya elimu, afya, kilimo na mifugo huku ikitarajia kuwapandisha vyeo wengine 80,050 kwa kada mbalimbali.

Alisema kuwa katika jitihada za kuboresha maslahi ya watumishi wa umma, serikali itaendelea na utekelezaji wa sera ya malipo ya mishahara na motisha katika utumishi wa umma ya mwaka 2010.

Aidha alisema kuwa wizara yake itashirikiana na Wizara ya Fedha katika siku maalumu ya kulipa mishahara ya watumishi wa umma katika vituo mbalimbali vya malipo badala ya mishahara kupitia benki kwa lengo la kuondoa tatizo la watumishi hewa.

Kutokana na majukumu na mipango ya utekelezaji kwa mwaka 2011/2012, aliwasilisha mapendekezo ya maombi ya fedha, ambapo katika fungu 20, Ofisi ya Rais Ikulu, iliombewa sh. bilioni 8.5, fungu 30, Ofisi ya Rais na Sekretarieti ya Baraza la
Mawaziri iliombewa sh. bilioni 200.5 kwa ajili ya matumizi ya kawaida na sh. bilioni 66.7 kwa ajili ya maendeleo.

Fedha zingine zilizoombwa ni pamoja na fungu 32, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma, sh. bilioni 16 ya matumizi ya kawaida, miradi ya maendeleo sh. bilioni 17.3, fungu 33, Ofisi ya Rais, Sekretarieti ya Maadili ya Viongozi sh. bilioni 2.3, miradi sh. milioni 910, fungu 67, Ofisi ya Rais, Sekretarieti ya Ajira katika utumishi wa umma sh. bilioni 2.9 na fungu 94, Ofisi ya Rais, Tume ya Utumishi wa Umma, sh. bilioni 8.2 kwa ajili ya matumizi ya kawaida.

Kwa upande wa kambi ya upinzani, walipendekeza kiwango cha mishahara cha kima cha chini kutoka sh. 135,000 ya sasa hadi 315,000 ili watumishi wakabiliane na makali ya kupanda kwa gharama za maisha.

Aidha kambi hiyo, ilipingana na fumula inayotumika sasa katika kuongeza mishahara ya watumishi kwa kufuata kiwango cha asilimia, ikisema ni cha kibaguzi na upendeleo kwa kuwa hupendelea zaidi wenye mishahara ya juu lakini huongeza zaidi pengo la mapato kati ya watumishi wa kada za juu na chini.

“Hali hii imefanya kuwepo kwa ubaguzi wa kimfumo, hivyo kuchochea kuibuka kwa matabaka na pengo baina ya walionacho na wasionacho, hivyo wakaitaka serikali kubadilisha utaratibu huo na ipandishe kwanza kima cha chini hadi sh. 315,000,”
alisema Bi. Suzan Lyimo ambaye aliwasilisha hotuba hiyo.

Aidha alisema kuwa ili serikali iongeze kiasi hicho cha mshahara, inatakiwa kupunguza posho na huduma za kuwalipia watumishi wa ngazi za juu kama huduma za maji, umeme, simu na zingine kwa kuwa hizi hazilipwi kwa watumishi wa ngazi ya chini.

“Tunaishauri serikali kupunguza misamaha ya kodi, kutumia vyanzo vya mapato vilivyoainishwa katika hotuba ya kambi hiyo, kuachana na matumizi yasiyo ya lazima ili iweze kupata fedha za kutosha zitakazowezesha kuongeza na kupandisha kima cha chini kwa mwaka huu wa fedha,” alisema Bi. Lyimo.

Bi. Lyimo pia alitumia mwanya huo, kuiomba serikali kupunguza kodi inayotozwa kwenye mishahara ya wafanyakazi ili waweze kubaki na fedha itakayowasaidia kutumia katika uchumi na kukuza uzalishaji.

Akizungumzia madai ya walimu, aliitaka serikali kutotumia vibaya uvumilivu wa walimu na badala yake iwalipe haraka madai yao.

12 comments:

  1. Hii hesabu unapoandika ni kama kuzuga maana kama ni asilimia40 toka 135,000 ni 189,000, ukweli ni hakuna kitu piga hesabu ya daladala kila siku kwenda na kurudi kwa mwezi tena awe anapanda basi moja ni 18,000
    +kila siku aache elfu 5 kwa mwezi 150,000
    kodi ya nyumba nje ya mji chumba ni 30,000 x2= 60,000,watoto 2 wa shule nauli 400x26 10,400= 238,400 watoto hawajaumwa,hapo mke hajatoka nyumbani mwezi mzima hujamnunulia hata kanga mkeo,hivi wao hawajaribu kukaa mwezi mmoja tu kwa mshahara huo? je, mtu anaekaa gongo la mboto kazi mikocheni au wazo nauli kiasi gani? tunadharauliana kiasi hiki?

    ReplyDelete
  2. Du wafanyakazi poleni.Heri yetu wajasiriamali wadogowadogo.Bunge la wabunge wa CCM ni boot leakers na yes men,hakuna jipya wakiulizwa kama wanaikubali bajeti wote watasema Ndiyoooooooo,atakayesema hakubaliani watamzomea,ole wenu hukumu yenu ni 2015 I swear nusu yenu hamtarudi,sisi tuko mitaani tunasikia maoni ya watu wanavyojadili kikao cha bunge kinachoendelea,unajua huko nyuma bunge lilikuwa in camera,hivyo wananchi walikuwa hawajui kinachoendelea mjengoni,mlipokuwa mkirudi na kuwadanganya kuwa mmewawakilisha ipaswavyo ila bajeti ni finyu mtawatetea awamu ijayo walikuwa wanawaamini,leo hii thubutu,tunawaona live mnavyotusaliti na kutetea posho zenu eti ikiwezekana mlipwe hata laki 5 kwa mwezi,hivi mnajisikiaje mnapopitisha kima cha chini kwa mwezi sawa na posho yako ya siku moja?huu ni usaliti na kama hamta hukumiwa na wananchi basi Mungu atawahukumu siku ya mwisho.

    ReplyDelete
  3. Kama kweli kuna mfanyakazi wa kawaida (toa wale maofisa) ambaye atampigia mbunge wa CCM kura 2015, then we are cursed.

    CDM wametoa mfano mdogo tu kwamba serikali ikiweza kufuta SITTING ALLOWANCE ingeweza kuokoa bilioni 900 ambazo zingeweza kuboresha mishahara ya wafanyakazi bila kutafuta vyanzo vingine vya mapato.

    Lakini wabunge wa CCM wakiongozwa na mtoto wa mkulima (SIC) wakawabeza na kuwazomea.

    Sasa sisi wafanyakazi kwanini tuendelee kuwaweka wabunge na serikali ya CCM madarakani. Kwanini tusijaribu CDM ambao angalau wameonesha kutujali?

    Bila kuondoa huu ugonjwa wa CCM-ISIM tutakuwa watu wa kulia na kusaga meno hadi mwisho wa dunia.

    ReplyDelete
  4. Kwa mtu asiye na uelewa anaweza kufurahi eti mshahara umepanda asilimia 40. Naomba niwakumbushe watanzania wenzangu. mwezi wa 12 mwaka jana shiringi ya Tanzania ilikuwa inabadilishwa na EURO (Fedha ya Ulaya) kwa EURO 1 = Tsh. 1800. ndani ya miezi hii sita hela yetu imeshuka dhamani mpaka EURO 1 inabadilishwa kwa Tshs. 2350, kwa hali hiyo kupanda kwa asilimia 40 hakuna lolote la maana. Hizo hesabu ukimpa mtu asiye kuwa na elimu anaweza kufuhi.

    wewe mwalimu unalipwa 300,000 mwenzako Mbunge analipwa 7,000,0000. hivi ni miezi mingapi wewe ufanye kazi ili umfikie mwezi mmoja wa Mbunge?

    Heri utawala wa Mkoloni kuliko utawala wa Kikwete na CCM.

    ReplyDelete
  5. Mishahara itaongezwa asilimia 40 na gharama ya maisha itapanda asilimia 80 ni sawa kutoka sufuriani kuangukia motoni na hivo ndivo itavokuwa.

    ReplyDelete
  6. inasikitisha sana na inauma sana, haya ndo maneno ya mkata tamaa, asiye na mbele wala nyuma, ila ni maneno ya muungwana asiyetaka fujo,, lakini pale uonevu unapozidi usishangae neno kama nimechoka kuonewa au uungewana umenishinda. Hii ndivyo itakavyokuwa kwa CCM siku za mwisho. Hebu angalia, 135,000 kwa 7,000,000 ni kama mara 51.85. Yaani ukiwa mfanyakazi wa sirikali utafanya kazi miezi 51.85 ni sawa na miaka minne na ushehe bila kutmia hata single cent ndo umlute mbunge anayelipwa 7,000,000 kwa mwezi. Kumbuka we ndo uliyemwajiri kwa kura yako moja, then hajali, matusi kwa kwenda mbele na kejeli za hapa na pale.

    Ndugu zangu inauma sana, ila tusichoke umasikini ungekuwa sumu hakuna mtu angeishi. 2015 siyo mbali lazima tulaumiwe kwa kufanya mahamuzi sahihi ya kubadilisha CCm kuliko tulaumiwe kwa kutofanya... Jua siyo kizazi cha sasa kitaona haya maovu ni cha baadaye ambapo watasema kizazi hiki hakiwa na dira. Chenge mwenyewe anaweza kulisha mikoa kadhaa ya Tanzania kwa hela aliyoiibia Tanzania, lakini aliovyopewa dhamana ya ubunge hakuwa hata na chupi ya kubadilisha..... Haki itawahukumu AMEN

    ReplyDelete
  7. Kudadadekeeeeee..... yani kunge kuwa na uwezekano wakuchapa mbunge vibao akiwa ana changia direct kwenye TV wabunge wa CCM wage kuwa wana lia kila saa!
    na tunge wavuta matai yao na kutumia kuwa nyoganayo!
    Kweli mshahara wa mtu mwezi mzima 13500
    alafu posho kwa siku laki 5 !!!!!!
    Heri ngamia kupita katika tundu la sindano kuliko mbunge!

    ReplyDelete
  8. kwel noma ni nilizani iyo asilimia 40.ni kama kitu cha laki hv ndo kimeongezeka kumbe looooooooooooo

    ReplyDelete
  9. sasa nyiny w2 wa magazeti mnaposema MISHAHARA JUU. mna maana gan? kumbe kilicho ongezeka kiduchu si muwe mna ponda 2

    ReplyDelete
  10. mnapiga kelele wakati nyie ndio wa kwanza kuipigia ccm kula ya ndio inapofika siku ya kupiga kula ndio maisha meme hayo kwa kila mtanzania,

    ReplyDelete
  11. Mungu Baba yetu uliye mbinguni ninaomba achilia masamaha yako kwa kila mtanzania na simama mwenyewe katika hili upate kuhukumu kwa haki wewe mwenyewe na sio sisi na kutetea watu wako ambao haki haitendeki inavyotakikana, hofu ya Mungu ikawe kwa kila mmoja katika JINA LIPITALO MAJINA YOTE LA YESU KRISTO, AMEN.

    ReplyDelete
  12. hivi hiii serikali inafanya nini maaana ukiangalia hata katika sekta binafsi kama makampuni ya simu mfano wa airtel tanzania waruhusu uwekezaji ili watanzania wapate ajira lakini serikali haipiti kukagua mishahara na kazi wanazofanya wa tz hawa maana wanafanya kazi kuubwa na wanaingiza mapato makubwa then wanalipwa laki na nusu kwa mwezi mzma na mtu amesota kuipata degree yake...kweli nyie ccm na kikwete dawa yenu ipo 2015

    ReplyDelete