Na Godfrey Ismaely
MAMLAKA ya Udhibiti wa Huduma za Nishati na Maji (EWURA) imesema imeanza kufanya uchunguzi kuwabaini wafanyabiashara wanaoendelea kuuza mafuta ya dizeli na petroli kwa bei ya juu ili wachukuliwe hatua kali za kisheria.
EWURA imesema baada ya serikali kushusha kodi katika bidhaa hiyo wafanyabiashara wote walitakiwa kuanza kushusha bei tangu Julai mosi mwaka huu.
Mamlaka hiyo imesema kwa mujibu wa tangazo la serikali namba tano la Januari 9, 2009 EWURA imepewa wajibu wa kudhibiti na kusimamia mwenendo wa mafuta nchini ikiwa ni pamoja na kutoa machapisho ya bei elekezi na kikomo kwa mafuta hayo.
Akizungumza na Majira jana, Ofisa Uhusiano wa mamlaka hiyo Bw.Titus Kaguo, alisema mabadiliko ya awali katika marekebisho ya mafuta hayo yalianza kutekelezwa rasmi kuanzia Julai mosi na kwamba mfanyabiashara yeyote anayeendelea na bei ya juu anafanya makosa.
"Baada ya marekebisho ya kodi katika kanuni ya ukokotoaji wa bei za mafuta, Dizeli imepungua kwa asilimia 4.86 hivyo bei elekezi ikiwa ni sh.1,939 kwa lita.
"Kwa upande wa bei mpya ya mafuta ya taa ikiongezeka kwa asilimia 21.88, bei elekezi ikiwa ni sh. 1,940 kwa lita," alisema Bw.Kaguo.
Hata hivyo alisema bei hizo zinaweza kutofautiana kadri mafuta yanavyosafirishwa mbali na soko la Dar es Salaam kuanzia kilomita 30.
Alisema licha ya kurekebisha tozo za gharama zingine kwenye mafuta pia EWURA imeanza mchakato ambao utawezesha kupungua kwa gharama za nishati hiyo ifikapo Agosti Mosi mwaka huu.
"Ushirikiano ni jambo la msingi sana kutoka kwa wananchi na wadau mbalimbali, kwa kuzingatia shughuli za ukusanyaji wa maoni na uhandaaji wa kanuni mpya ya rasimu kwa ajili ya maandalizi ya kukokotoa bei za mafuta kwa lengo la kupunguza gharama hizo," aliongeza Bw. Kaguo.
Alisema mamlaka hiyo itaendelea kutoa takwimu sahihi mara kwa mara kwa umma na wafanyabiashara ili waweze kutambua mabadiliko na hata viwango vya bei za mafuta zinavyokwenda.
Uchunguzi wa Majira ulibaini kuwa licha ya serikali kupunguza kodi ya mafuta ya dezeli na petroli wafanyabiashara wameendelea kuwalangua wananchi kwa kuwauzia kwa bei ya zamani huku wakisingia kuwa walikuwa na akiba kubwa kwenye maghala.
No comments:
Post a Comment