08 July 2011

Majambazi wateka jahazi, watupa abiria baharini

Na Masau Bwire, Kibaha

WATU sita waliokuwa wakisafiri katika bahari ya Hindi kwa kutumia jahazi wakitokea kisiwa cha Mafia kwenda Kilwa mkoani Pwani, wamevamiwa na majambazi na
kuwatosa baharini.

Majambazi hao waliwavamia na kuwashambulia watu hao katika bahari ya Hindi kati ya
Mafia na Kilwa kwa silaha za jadi ikiwa ni pamoja na mapanga, nondo na marungu saa 8
usiku wa kuamkia Oktoba 6 mwaka huu.

Ilielezwa kuwa baada ya kutoswa baharini na jahazi lao lililokuwa likitumia injini kuporwa na majambazi hao watu hao walianza kuogelea katika harakati za kujaribu kujiokoa.

Wawili kati yao walifanikiwa kufika ufukweni wakiwa salama japo walikuwa wamechoka na hawawezi kuongea.

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Pwani Bw. Ernest Mangu, aliwataja watu hao waliogelea hadi ufukweni mwa kisiwa cha Bwejuu kuwa ni nahodha wa jahazi hilo Bw. Yunus Yusuph (35), mkazi wa Kiombini Mafia aliyefika ufukweni hapo sita  mchana na msaidizi wake Bw. Omary Juma (30) ambaye yeye alifika kisiwani hapo saa 11 jioni.

Kamanda Mangu alisema watu hao walipofika katika ufukwe wa kisiwa hicho walisaidiwa
na wakazi wa kisiwa hicho ambao waliwachukua kwa boti hadi kisiwa cha Kilindoni
ilipo hospitali kwa ajili ya matibabu na huduma nyingine za kipolisi.

Alisema mtu mwingine aliyetambuliwa kwa jina moja la Chinga ambaye alikuwa mhudumu
katika jahazi hilo linalomilikiwa na kikundi cha Majanjara, Rufiji mkoani hapa na
watu wengine watatu ambao majina yao hayajafahamika walioomba msaada katika jahazi
hilo bado hawajapatikana.

Alisema polisi wametawanyika katika maeneo ya fukwe wilaya za Mafia Kilwa na Rufiji kuwasaka majambazi hayo na kuwatafuta watu wanne waliotoswa baharini ambao hawajaonekana.

Alisema tayari amewasiliana na polisi Zanzibar na kikosi cha Polisi Marini Dar es
salaam kwa ajili ya kuongeza nguvu katika msako huo kuhakikisha majambazi hao
wanakamatwa.

Kamanda Mangu ametoa mwito kwa wananchi hasa maeneo ya fukwe ya bahari ya Hindi kushirikiana na polisi kuhakikisha majambazi hayo wanakamatwa na kusaidia kuwatafuta watu wanne waliotoswa baharini wawe hai au wamekufa.

5 comments:

  1. Kuweni makini basi ktk kutoa habari, Ni tukio tarehe 6 Octoba mwaka huu au vipi? na hicho kijiji cha Bwejuu ni cha Zanzibar au Rufiji? Tunaweza kuwa tumewaona lakini sasa hizi tarehe zinatukanganya tutawezaje kutoa msaada?

    ReplyDelete
  2. Wewe mwandishi wa habari hizi uitwae Masau Bwire kazi hii ya uandishi haikufai.Tafuta kazi nyengine utakayoimudu.

    Taarifa yako inaeleza watu hao walishambuliwa na majambazi usiku wa kuamkia Oktoba 6 mwaka huu !
    Leo ni tarehe 8 Julai.Bado siku 89 kufikia tarehe ya tukio ulilolitaja !

    Nakushauri baada ya kuandika taarifa zisome mwenyewe kabla kuzitoa kwa wasomaji au tafuta kazi nyengine.

    ReplyDelete
  3. Sasa hili gazeti halina wahariri hata kuangalia tarehe za habari. Mnakuwa waswahili mno katika uandishi. Kuweni serious na taaluma ya uandishi

    ReplyDelete
  4. nasikitika kukumbuka maneno aliyoyasema mkapa wakati fulani.and i quote"waandishi gani uchwara hawa".hivi hamjui maana ya proof reading?nikikosea mimi wasomaji watanielewa.lakini wewe ndugu yangu watakukomalia.

    ReplyDelete
  5. Pengine huyu mwandishi anafikiri leo ni April Fool

    ReplyDelete