*Yatinga fainali Kagame Castle Cup
Na Zahoro Mlanzi
NI kipa Juma Kaseja ndiye atakayepewa pongezi za pekee kwa kuokoa penalti iliyopigwa na Jonas Sakwaha na kuiwezesha timu yake ya
Simba kutinga fainali ya Kagame Castle Cup kwa kuiondosha El Merreikh ya Sudan kwa penalti 5-4.
Mara baada ya kuokoa penalti hiyo, Kaseja alishangilia kwa furaha uwanja mzima, huku akionesha fulana yake ya ndani iliyokuwa na maneno yaliyoandikwa 'There is only one Kaseja', akiambatana na wachezaji wengine wa timu hiyo.
Hakika ilikuwa ni furaha ya aina yake kwa maelfu ya mashabiki wa Simba waliokuwepo uwanjani hapo, huku wengine wakisikika wakishangilia kwa kusema 'Bado Yanga', 'Bado Yanga', 'Sisi hatubebwi, kazi moja tu'.
Kwa ushindi huo, Simba sasa inasubili mshindi katika mchezo wa leo kati ya Yanga na St. George ya Ethiopia, ambapo fainali inatarajiwa kupigwa Jumapili kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.
Katika mchezo huo wa jana, El Merreikh ilianza kwa kasi kwa kuliandama lango la Simba na dakika ya nne walibisha hodi, baada ya Balla Gabir kupiga shuti lililopanguliwa na Kaseja na mabeki kuondosha hatari langoni kwao.
El Merreikh iliendelea kuliandama lango la Simba na dakika ya nane, kiungo Ahmed Albasha alipiga shuti la kushtukiza nje ya eneo la hatari, lakini Kaseja alikuwa makini kuokoa na kuwa kona isiyo na madhara kwa Simba kutokana na mabeki kuokoa.
Kutokana na Simba kushindwa kuhimili presha ya El Merreikh, dakika ya 12, Adiko Rima aliifungia timu yake bao la kwanza akiunganisha mpira wa krosi uliopigwa na Sakwaha kutokana na mabeki wa Simba kushindwa kuondosha mpira langoni mwao kwa wakati.
Baada ya kushambuliwa kwa mfululizo, Simba ilitulia na kujipanga ambapo dakika ya 24, Ulimboka Mwakingwe aliisawazishia bao timu yake kwa kichwa, akimalizia mpira uliotemwa na kipa Isam Elhadary kutokana na krosi iliyopigwa na Shija Mkina.
Kipindi cha pili kilianza kwa kasi huku El Merreikh ikicheza kwa kupoteza muda na kuifanya Simba iliandame lango la wapinzani wao kwa kufanya mashambulizi mengi zaidi, dakika ya 75, Mkina nusura aifungie Simba bao la ushindi, lakini kichwa alichopiga kilipaa juu ya goli.
Simba ilizidi kuliandama lango la wapinzani wao, na dakika 13 za mwisho ilihamia langoni mwa wapinzani wao kutokana na muda mwingi kucheza nyuma zaidi na kufanya sehemu ya kiungo itawaliwe na Simba, lakini mpaka dakika 90 zikimalizika timu hizo zilifungana bao 1-1.
Kwa mujibu wa kanuni za mashindano hayo, hatua hiyo ni lazima ziongezwe dakika 30, hata hivyo kuongezwa kwa dakika hizo hazikusaidia kitu mpaka mwamuzi Sylivester Kirwa kutoka Kenya alipoamuru mikwaju ya penalti itumike.
Katika penalti hizo, Simba ilipata penalti tano kati ya sita, ambapo wachezaji waliopata ni Nassor Said 'Chollo', Jerry Santo, Patrick Mafisango, Salum Kanoni na Mwakingwe na Salum Machaku penalti yake iligonga mwamba na kutoka nje.
No comments:
Post a Comment