Na Mwandishi Wetu
KLABU ya soka ya Majimaji ya Songea, imeliandikia Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF), kuondoa pingamizi lililowekwa awali dhidi ya mchezaji
Ulimboka Mwakingwe.
Mwakingwe aliyeichezea timu hiyo msimu uliopita, alisajiliwa na klabu yake ya zamani, Simba kwa ajili ya msimu wa 2011/2012.
Kwa mujibu wa taarifa iliyotumwa na Msemaji wa TFF, Boniface Wambura, alisema Majimaji kupitia Katibu Mkuu wake, Henry Kabera, imesema baada ya kukutana na uongozi wa Simba, imeamua kuondoa pingamizi dhidi ya mchezaji huyo ambaye ilimsajili kwenye dirisha dogo msimu uliopita.
Awali, Majimaji iliwasilisha pingamizi TFF kwa wachezaji wake 11, iliosema kuna tetesi wamesajiliwa na klabu mbalimbali za Ligi Kuu ya Vodacom, lakini hawajafanyiwa uhamisho ingawa bado wana mikataba na timu hiyo.
Wachezaji hao ni Said Mohamed (Yanga), Ulimboka Mwakingwe (Simba), Ally Bilaly (Villa Squad), Juma Mpola (Kagera Sugar), Evarist Maganga (Villa Squad) na Kulwa Mobby (Polisi Dodoma).
Wengine ni Paul Ngalema (Ruvu Shooting), Mohamed Mpola, Lulanga Mapunda (Toto Africans), Hamad Waziri na Yahya Shaban Haruna.
Wakati huo huo, Wambura alisema kuwa, mechi ya kirafiki ya kimataifa kati ya timu ya Taifa ya Vijana wenye miaka chini ya 23 'Vijana Stars' na Shelisheli iliyochezwa juzi mjini Arusha iliingiza sh. 5,014,000.
Katika mechi hiyo, Vijana Stars ilishinda mabao 3-1. Timu hizo zitarudiana tena kesho kwenye Uwanja Sheikh Amri Abeid mjini Arusha.
Shelisheli iko kwenye ziara ya maandalizi ya michuano ya nchi za visiwa vilivyoko katika Bahari ya Hindi barani Afrika, itakayofanyika mwezi ujao.
Visiwa hivyo ni Shelisheli, Mauritius, Comoro, Mayotte, Reunion na Madagascar.
No comments:
Post a Comment