08 July 2011

Sumaye aionya CCM

*Asema kundi dogo la matajiri linataka kuimeza
*Rais Kikwete viongozi awataka waache kulindana


Martha Fataely, Moshi na Humphrey Shao, Dar

MJUMBE wa Halmashauri Kuu ya Taifa wa Chama Cha Mapinduzi (NEC-CCM), Bw. Frederick Sumaye amesema chama hicho kina kila dalili ya
kutekwa na kundi dogo la matajiri jambo ambalo ni hatari kwa mustakabli wake.

Bw. Sumaye ambaye pia ni Waziri Mkuu mstaafu, ameonya kuwa kundi hilo isipodhibitiwa litaharibu mwelekeo wa chama hicho mbele ya wananchi na kukiangamiza.

Kauli hiyo ya Bw. Sumaye imekuja wakati ile sheria ya kutenganisha siasa na biashara iliyokuwa imeahidiwa na Mwenyekiti wa chama hicho, Rais Jakaya Kikwete ikiwa imewekwa kando bila taarifa yoyote.

Akihutubia mkutano wa hadhara katika Kata ya Bomambuzi Manispaa ya Moshi jana ikiwa ni sehemu ya maadhimisho ya kuzaliwa kwa TANU, Bw. Sumaye pamoja na kupongeza juhudi za Rais Kikwete, kupitia dhana ya kujivua gamba, Bw. Sumaye alisema kundi dogo la matajiri lililopo ndani ya chama hicho kwa sasa linataka kukiteka na kuondoa malengo ya kuwa cha wakulima na wafanyakazi.

“Sina maana ya kuchukia matajiri, lakini watu hawa wasituharibie chama, nakumbuka kauli ya Waziri Mkuu mstaafu marehemu Rashid
Kawawa, 'tukiwa ndani ya mtumbwi kisha mwezenu akataka kuutoboa mtumbwi huo, mnatakiwa kumtosa ili asiwazamishe wote,” alisema Bw. Sumaye.

Alisema kutokana na kauli hiyo, ndiyo maana sasa CCM inawatosa wale ambao wanataka kutoboa mtumbwi huo, ili chama na Watanzania waendelee kubaki salama.

Alisema hakuna nchi yoyote duniani isiyo na matajiri na maskini lakini tatizo lililopo nchini ni kundi dogo la matajiri kutisha kundi kubwa la masikini, hivyo kuna haja kwa taifa kujenga mfumo mpya wa kumiliki utajiri usioishia kwa wachache bali kwa kila Mtanzania.

Alisema kwa sasa CCM inafanya utaratibu wa kujisafisha na kutaka kurejesha misingi iliyoasisi na waasisi wa taifa na kwamba lazima kiwe chama cha umma na wanyonge na kutoruhusu kutekwa na matajiri ambao wanatishia amani ya nchi.

Alitaja ufisadi, rushwa udini na ukabila kuwa ni mambo yanayotishia amani ya nchi na si CCM pakee na kuonya kuwa mambo yote hayo ni matokeo ya kundi dogo kutodhibitiwa.

Alitaja matatizo ya muungano ambayo yanapaswa kujadiliwa hususani kipindi hiki cha kuandaa katiba mpya ili kupata ufumbuzi wa haraka.

Bw. Sumaye alisema kwa sasa kuna umuhimu wa kujadili kasoro za Muungano hizo na kuwaonya baadhi ya wanasiasa wanauobeza ukiwa umedumu kwa miaka 47 kuacha tabia hiyo kwa mustakabali wa taifa na kizazi kijacho.

Akifafanua kuhusu ufisadi na rushwa, alisema mambo hayo ni hatari zaidi kuliko wizi na kwamba ipo sababu kubwa kwa viongozi wote kila mmoja kwa nafasi yake kuhakikisha anayashughulikia ili kupunguza pengo kubwa kati ya matajiri na masikini.

Akizungumzia maendeleo ya nchi kwa ujumla, Bw. Sumaye alisema Tanzania imepiga hatua kubwa kimaendeleo katika sekta za Elimu, Afya, Maji na Barabara.

Alitoa mfano kwa Wilaya ya Moshi ambayo miaka iliyopita ilikuwa na shule 10 za msingi zenye wanafunzi 1,577 lakini kwa sasa zipo shule 44 zenye wanafunzi 23,802.

Alisema Wilaya hiyo ilikuwa na shule za sekondari mbili na sasa zipo 77, hapakuwa na zahanati wala kituo cha afya bali hospitali moja lakini leo kuna zahanati 52 vituo vya afya saba na hospitali saba, jambo ambalo ni la kujivunia.

Alisema miaka ya nyuma kulikuwa na kilomita saba pekee za barabara za lami lakini sasa zipo kilomita  91 za lami lakini pia wakazi wa Manispaa sasa wanapata maji safi kwa asilimia 95, jambo ambalo halikuwepo awali.

Awali akimkaribisha Bw.Sumaye kuzungumza, Mwenyekiti wa CCM, Mkoa wa Arusha, Bi. Vicky Swai alisema wanaobeza chama hicho tawala ni wadhaifu kwa kuwa wanaona mafanikio yaliyopatikana.

Kikwete na kulindana

Wakati Bw. Sumaye akisema hayo, Mwenyekiti wa chama hicho, Rais Kikwete, amewataka viongozi wa chama hicho ngazi ya mkoa, wilaya na tawi kuacha tabia ya kulindana na kuwaengua wanachama wote wanaoonekana kukosa maadili na msingi wa chama hicho.

Pia Rais Kikwete amewajia juu makatibu wa chama hicho ngazi ya mkoa na wilaya akiwataka kuacha uzembe na ukubwa unaowafanya kushindwa kuimarisha chama hicho ngazi zao kwa kukaa maofisini.

Alisema hayo jana wakati akizungumza na wajumbe wa mashina na wenyeviti wa mitaa Mkoa wa Dar es Salaam katika sherehe za miaka 57 ya kuzaliwa kwa Chama Cha Tanganyika Afrikan Union (TANU) iliyozaliwa Julai 7 mwaka 1954, ambayo baadaye iliungana na Afro Shiraz Party (ASP) kuwa CCM.

Rais Kikwete aliwataka viongozi na wanachama wote kutowaonea aibu wala kuwalinda wanaonekana kukosa sifa kwa kuwang'oa mapema kama hawataki kung'atuka wenyewe, ili chama hicho kiendelee kubaki na watu waaminifu.

"Mara ya kwanza kulikuwa na kisingizio cha vitendea kazi, lakini sasa wamepewa magari, tena ya kisasa, hawaendi vijijini, hivyo basi kuhakikisha kuwa tunakijenga chama ni lazima wote tuwe na misingi ya umoja na moyo wa kujitolea ili tuweze kusonga mbele," alisema Rais Kikwete.

Makatibu hao walitakiwa kuwa na moyo wa kujitolea kwa dhana ya kuiga mifano ya watendaji wa zamani ambao hawakuwezeshwa lakini walifanikiwa kuwafikia watu wengi.

Alisema umefika wakati wa kila kiongozi kuwa na moyo wa kujitolea na kuonya kuwa asiyekuwa na tabia hiyo ana malengo ya kubomoa chama.

Alisema CCM hakina mali za kutosha kama serikali, hivyo wasitegemee kufanya kazi hizo kama serikali kwa kuwa chama zinataka ari zaidi na nguvu zaidi ili kufikia malengo iliyowekea.

Aliwashukuru uongozi wa Mkoa wa Dar es Salaam kumpatia nafasi hiyo kukutana na wazee waliojitoa kuikomboa nchi katika mkono wa ukoloni chini ya TANU.

Katika sherehe hizo ambazo ziliudhuriwa na watu mbalimbali akiwemo mmoja wa waasisi wa TANU Mzee Costantine Milinga (90), Bw. Kingunge Ngombale- Mwiru amboa walipata nafasi kuleza jinsi walivyojitoa kwa hali na mali kuhakikisha nchi inapata uhuru.

Kwa upande wake mmoja wa Kada wa chama hicho Bw. Rajabu Mwilima, alisema ujumbe uliotolewa na Rais Kikwete jana ni ukurasa mpya kwa watendaji na wana CCM kutambua msingi gani uliopo ndani ya chama hicho.

"Umefika wakati wa watu kufanya kazi ndani ya chama na kuachana na tabia ya kupigana majungu ambayo yatasababisha ugomvi wa wenyewe kwa wenyewe na kusahau ustawi wa chama, wakati viongozi wa kada ya chini wametuamini," alisema Bw. Mwilima.

8 comments:

  1. Kikwete anashangaza kweli. Yeye ndiye kinala wa kulindana sasa anasema nini? Yeye aache hii tabia kwanza.

    ReplyDelete
  2. Kikwete ni nani? Anaiangamiza nchi kila siku, kufika 2015 kama atafika, Tanzania itakuwa mbaya sana ukilinganisha na kipindi cha ukoloni, ni mara bilion turudi mwaka 1961 tulipopata uhuru tuishi vile kuliko maisha ya huyu jamaa. Miaka yake imekuwa shida sana, hana kitu kichwani ni zuzu huyo NENO alilo litumia sana Baba wa Taifa, kwa mtu anaye furahia kubadilishana Almasi na kijiwe cheupe, hivyo huyo anaye kubali kijiwe cheupe na akatoa alumasi yake ni zuzu na ndo Kikwete alivyo. Lakini baba wa Taifa aliona siku nyingi kuwa huyu jamaa (Kikwete)bado mtoto akimaanisha ni vigumu kwake kuwa na mawazo endelevu, ni sawa na mtu anaingiza kipato cha TZS 100 kwa siku na anatumia TZS 101 kwa siku, lazima uchakae kama Tz sasa hivi imechakaa kwa muda mfupi.

    ReplyDelete
  3. Wewe uliyetoa maoni hapo juu, sina uhakika una miaka mingapi lakini inaelekea bado u kijana sana. Matatizo ya Tanzania yana historia yake. Mengi yanatokana na siasa zetu za huko nyuma ambazo hazikulenga kuimarisha private sector. Hakuna nchi yoyote iliyoendelea bila kuwa na private sector yenye nguvu ambayo ni chanzo cha kuwa na middle class. Tusiwe wavivu wa kufikiri na kufanya tathmini ya kuna kwa kutoa majibu rahisi kwamba tatizo ni Kikwete. Hayo ni majibu rahisi yanayotolewa na wanasiasa wanaotaka kurithi kiti cha Kikwete. Hata angekuwepo Nyerere leo hii, kama tungeendelea na siasa za nyuma tungeendelea kwenda chini zaidi. Tangu nimezaliwa miaka 57 iliyopita, nimekuwa nikisikia kuwa Tanzania ilikuwa kati ya nchi 25 maskini sana duniani. Siyo kwamba Kikwete alipochukuwa nchi tulikuwa matajiri na sasa ameipeleka nchi yetu katika umaskini. Huu umaskini ulikuwepo. Wakati nikiwa kijana tulikuwa tunapanga mstali kununua sukari. Tuache jazba na siasa kama ya ndugu hapo juu, tunapofanya tathmini ya matatizo yetu kama taifa. Taifa letu liko katika kipindi cha mpito kutoka siasa za huko nyuma na kuingia katika siasa za karne hii, ambazo zina changamoto nyingi. Watanzania tutake tusitake, mtu yeyote anayekuwa rais katika kipindi hiki, hawezi kuongoza kwa style ya Nyerere. Huo wakati umepita.

    ReplyDelete
  4. Hata wewe Mbatia unamatatizo pia inamaana mambo yote ya ajabu yanayofanywa na viongozi wa chama tawala huyaoni?Kikwete alitakiwa kuyakaripia na kuchukuwa hatua kwa viongozi wabovu,Lakini badala yake yeye amebakia kuwaangalia tu na kulalamika kwa wananchi.Je anataka wananchi wajichukulie hatua mikononi mwao.Yeye ni kiongozi na anatakiwa awe mfano kwa walio chini yake.Yeye sasahivi analaumu viongozi kulindana wakati yeye yumo katika kundi hilohilo la kulinda rafiki zake.Tutafika kweli kwa mwendo huu.Hakuna serikali ambayo imekuwa na kashfa nyingi na za kutisha kama hii ya kikwete.Kila kukicha utasikia jambo jipya kuhusu kashfa na hakuna hatua inayochukuliwa.

    ReplyDelete
  5. Kikwete ni mwizi tena mkubwa sana na ndiye kocha wa majambazi mafisadi na waujumu uchumi hapa nchini. Hakuna ubishi hapo na kama kuna mtu anabisha aende maakamani atoe malalamiko. Maandiko matakatifu husema kuwa , Haki haiji ila kwa ncha ya upanga! Hili liko wazi na serekali ya huyo kikwete imekuwa ikitumia ncha ya upanga kuzuia watu kudai haki zao ila siku yaja. Najua mnaogopa ila weka hili akilini, SIKU YAJA ambayo hao polisi wake wasio na elimu yoyote wanaokaa na kumwaga damu za wadai haki watatumika kama ncha ya upanga na wakwanza atakuwa kikwete na vibaraka wake. Naingoja siku hiyo kwa hamu na naamini after tutakuwa na Tanzania ya wastaarabu na watu sawa. Alisema Bush kabla ya kuingia Iraq kuwa anataka kumpiga Sadaam kwakuwa anataka dunia yenye ustaarabu na amani!

    ReplyDelete
  6. Hebu tuache jazba kidogo na kuangalia nini cha kufanya kuliko kufikiria kumwaga damu hebu uliza kwanza madhara ya vita.. Nchi gani ambayo unaijua wameuana na sasa mambo yako safi? mkianza kupigana mapanga mtafanya hivyo vizazi kwa vizazi..Elimisheni wananchi kuchagua viongozi wanaofaa inaweza kuchukua muda lakini watapatikana.. Mdau mpenda Amani

    ReplyDelete
  7. Inabidi ufikirie ncha ya upanga kwa kuwa walio madarakani ndiyo wanao yatengeneza mawazo hayo kwa jamii ya sasa kwa kuto kuchukua hatua yeyote kati ya hizi zote zilipo,habari ndiyo hiyo ndugu.

    ReplyDelete
  8. Wewe unayeitwa Mbatia ni kati ya haohao maana ana mawazo mgondo na unafikiri enzi hizi ni enzi za baba wa Taifa,endelea kujidanganya.Wote hao wanaolalamika wanautaka uraisi mbona haikuwa hivi miaka yote iliyopita ndani ya Tanzania?Kilichopo hapa ni ubaya wa kuwekwa madarakani na watu fulani badala ya kuwekwa madarakani na wananchi unaotegemea kuwatawala,kama hilo hujaliona nakupa hongera na undelea kufunika kope za macho yako.

    ReplyDelete