*Yanga na 'wachovu' Red Sea
Na Zahoro Mlanzi
BAADA ya kutoka suluhu na Red Sea ya Eritrea katika mchezo wa mwisho wa Kundi A jana, mabingwa mara sita wa mashindano ya Kagame Castle Cup, Simba itakutana na
Bunamwaya ya Uganda katika robo fainali ya mashindano hayo.
Wakati Simba ikijiuliza kwa Bunamwaya kesho, watani zao wa jadi Yanga itacheza na Red Sea Jumatano ambayo inayoonekana dhaifu kutokana na jinsi inavyocheza katika mchezo utakaopigwa Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.
Timu zingine zilizotinga robo fainali ya mashindano hayo ni Ulinzi ya Kenya itakayoumana na El Merreikh ya Sudan kesho saa nane mchana na St. George ya Ethiopia itacheza na Vital 'O ya Burundi Jumatano.
Simba imepangwa kucheza na Bunamwaya baada ya kuongoza kundi A kwa pointi nane na Bunamwaya imetinga hatua hiyo kutoka kundi B baada ya kuwa timu yenye matokeo mazuri zaidi miongoni mwa zilizoshindwa kutinga hatua hiyo.
Mchezo huo utapigwa kesho kuanzia saa 10 za jioni ukitanguliwa na mchezo kati ya Ulinzi na El Merreikh ambapo timu hizo zimefuzu baada ya kushika nafasi za pili katika makundi yao ya B na C ambapo Ulinzi ilikuwa na pointi tano na El Merreikh pointi tano.
Michezo mingine ya robo fainali itapigwa keshokutwa kwa mabingwa wa Tanzania bara, Yanga kuumana na Red Sea mchezo utakaopigwa majira ya 10 jioni ambapo Yanga imetinga hatua hiyo baada ya kuongoza kundi B na Red Sea yenyewe imeshika nafasi ya pili katika kundi A.
Kabla ya kuanza kwa mchezo huo, St. George itajiuliza kwa Vital 'O mchezo utakaoanza saa nane za mchana ambapo St. George imetinga hatua hatua hiyo baada ya kuongoza kundi C na Vital 'O imeshika nafasi ya tatu katika kundi A.
Katika mchezo wa jana ambao Simba uliwafanya waongoze kundi lao, ilipata nafasi nyingi za kufunga lakini washambuliaji wao waliokuwa wakiongozwa na Mussa Hassan 'Mgosi' hawakuwa makini kukwamisha mpira wavuni.
Katika mchezo huo tukio la kukumbukwa ni lile na beki Nassor Said 'Cholo' kupiga shuti lililogonga mtamba wa panya na mpira kutua katikati ya mstari na kurudi uwanjani lakini mabeki waliondosha hatari.
Kwa upande wa Red Sea, watajutia nafasi waliyopata dakika ya 77 baada ya kufanya shambulizi la kushtukiza lakini Samuel Berhane alishindwa kukwamisha mpira wavuni akibaki na kipa Juma Kaseja kwa kupiga shuti lililotoka nje.
No comments:
Post a Comment