08 July 2011

RT kuishauri serikali kuendeleza vipaji

Na Amina Athuamni

KAMATI ya Ufundi ya Chama cha Riadha Tanzania (RT), imesema itaishauri Serikali juu ya mpango wa kuendeleza vipaji vilivyopatikana kupitia mashindano ya Umoja wa
Michezo na Taaluma wa Shule za Sekondari (UMISSETA) na Umoja Michezo na Taaluma wa Shule za Msingi Tanzania (UMITASHUMTA).

Akizungumza Dar es Salaam jana, Mwenyekiti wa kamati hiyo Suleiman Nyambui, alisema katika mashindano hayo, RT iliweka mipango mizuri ya kuviendeleza vipaji vilivyopatikana.

"Tutatoa ushauri kwa Serikali ili tufanye kitu cha pamoja ambacho kitasaidia kwa kiwango kikubwa kuendeleza wanamichezo waliopatikana katika UMISSETA na UMITASHUMTA," alisema Nyambui.

Alisema mashindano hayo yameibua matumaini ya kufufua mchezo huo ambao katika miaka ya hivi karibuni, wanariadha wengi wamekuwa wakishindwa kufanya vizuri.

"Michezo ya shule za msingi na sekondari, ndiyo iliyotuibua mpaka tukapata medali za Olimpiki, lakini tuliendelezwa na ndiyo mafanikio makubwa mwaka 1970," alisema.

Nyambui alisema RT wameandaa programu nzuri ambayo kama serikali wataiunga mkono, itafanikisha kuwaendeleza wanariadha waliotokea katika michezo ya UMISSETA na UMITASHUMTA.

No comments:

Post a Comment