01 August 2011

Ndugai atetea mikopo ya mashangingi

Na Godfrey Ismaely

 Dodoma

NAIBU Spika, Bw. Job Ndugai amewataka wananchi kuacha kuwashambulia wabunge juu ya magari wanayonunua kwa mikopo kwa kuwa kufanya hivyo wanakuwa hawawatendei haki.


Amesema badala yake wakae pamoja na kupendekeza njia ambazo zinaweza kutumika serikalini ili ununuzi wa mgari katika idara na taasisi zake mbalimbali upungue kwa lengo la kupunguza gharama za uendeshaji na matumizi makubwa ya fedha za umma.

Bw. Ndugai ambaye pia ni Mbunge wa Kongwa (CCM), alitoa wito huo juzi katika mahojiano na gazeti hili Mjini Dodoma juu ya mashangini hayo ambayo yamekuwa yakilalamikiwa na wananchi.

“Hamna mbunge hata mmoja ambaye anatumia fedha za umma kununulia gari la kufanyia kazi, iwe ni kutoka upinzani au chama tawala, kinachofanyika wabunge wote wanapewa mikopo ambayo inasimamiwa na Ofisi za Bunge kwa kuwapa dhamana wakati wa kwenda kukopa fedha hizo ili waweze kununua magari ya kufanyia kazi,” alisema na kuongeza:

“Ofisi ya Bunge inahusika na dhamana tu, kinachofuatia ni mbunge kujaza fomu husika na kufuata taratibu zote za kukopa fedha za gari. Kwa safari hii zinatakiwa zisizidi sh. milioni 60, kati yake sh. milioni 45 ndizo wanakopeshwa na kupitia mishahara yake na posho zitakuwa zinakatwa kidogo kidogo hadi miaka mitatu awe amemaliza
kurejesha,” alifafanua Bw. Ndugai.

Alisema utaratibu unaotumika hapa nchini kwa kuwakopesha wabunge fedha za kununulia magari ya kufanyia kazi ni mzuri tofauti na nchi jirani kama Kenya na Uganda ambazo zinawapa bure wabunge wote kila mmoja gari lenye thamani ya sh. milioni 200.

“Tumekuwa tukiwabebesha wabunge mizigo mizito mara kwa mara likiibuka suala la posho, magari, mishahara wao tu ndiyo wanaonekana wanapendelewa, lakini siyo kweli ndiyo maana serikali kwa kutambua nafasi yao katika kulitetea taifa inawajengea uwezo wa kujitegemea katika magari, kwa kuwa utaratibu wa kumkopesha mbunge gari inaipunguzia serikali gharama ya kununua magari mengi, gharama za matengenezo, mafuta na dereva wa kuwaendesha kwenda katika shughuli zao,” alisema Bw. Ndugai.

Kuhusu magari ya serikali

Alisema kama serikali itaanzisha utaratibu wa kuwakopesha watendaji wake fedha za kununulia magari yao binafsi ili ipunguze gharama, ikiwa ni pamoja na Wakuu wa Wilaya na Mikoa, hatua hiyo itaokoa fedha nyingi za umma.

“Nimewahi kutembelea katika Wizara moja ya Mazingira nchini Afrika ya Kusini nikakuta ina magari mawili tu kwa ajili ya dharura, lakini hapa
nyumbani suala hilo halipo, hivyo ninaona kama tunaweza kuiga wenzetu kwa kuwakopesha fedha ambazo zitakuwa zinarejeshwa kwa awamu na hivyo kupunguza gharama serikalini kama Rwanda ilivyowahi kufanya kwa kuuza asilimia kubwa ya magari ya serikali,” alifafanua Bw. Ndugai.

Bw. Ndugai aliongeza kuwa umefika wakati kwa kila mwananchi kuliamini bunge lao kwa kuepuka maneno ya upotoshaji ambayo wakati mwingine yanaweza kuwafanya kugawanyika katika makundi mbalimbali, bali washirikiane na wabunge wao katika kuwawasilishia kero zao ili zipatiwe ufumbuzi bila kujali itikadi zao za chama.

2 comments:

  1. jamii haiwajibiki kumnunulia mbunge gari kwani siku alipogombea ubunge alikuwa anajua kuwa kazi ya ubunge inahitaji usafiri kwahiyo kama alikuwa anajua hawezi kuwa na usafiri hakupaswa kugombea kazi hiyo. swala la bunge kuwadhamini wabunge hicho akikutakiwa kiwepo kabisa kwa maana hiyo ni special preference kitu ambacho ni cha ubaguzi na pili kudai kuwa inawadhaminitu pia sio kweli bali inawalipia magari hayo kwa mlango wa uwani mishahara na posho makubwa wasiostahili kwahiyyo sio kweli kusem kuwa serikali haiwalipii wabunge magari. kuhusu kufananisha Tanzania na kenya kuhusu magari huo ni weu kwani kenya ni nchi ya kifisadi inafahamika wazi. kwanini ujifafanishi na nchi kama Rwanda ambapo wabunge wanajinunulia magari yao wenyewe??. wabunge kama raia wengine wanatakiwa kwenda kukopa gari kama wananchi wengine wanavyofanya na sio kuwatengeneza mazingira maalum kwa ajili yao tu.

    ReplyDelete
  2. Mbona hatujaelezwa kuhusu fedha ya mafuta na matengenezo ya mashangingi hayo inatokaq wapi?

    ReplyDelete