01 August 2011

Mrema amvutia pumzi mbunge Chiku Abwao

Na Godfrey Ismaely

Dodoma

MWENYEKITI wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Hesabu za Serikali za Mitaa, Bw. Augustine Mrema amesema kuwa mara baada ya Mbunge wa Viti Maalumu-CHADEMA, Bi. Chiku Abwao kumtuhumu kuwa ni wakala wa CCM asubirie dozi yake bungeni.


Kauli hiyo aliitoa jana mjini Dodoma wakati akizungumza na gazeti hili kutaja kujua maoni yake kuhusu tuhuma kuwa ni yeye na Mbunge wa Bariadi Mashariki, Bw. John Cheyo ni mawakala wa CCM.

“Huyo Chiku Abwao asubirie, si ana mdomo mzuri sana wa kusema hata mimi nina mdomo pia wa kusema sana, alinishambulia wakati akichangia hoja, na mimi nitampa yake wakati wa bunge, huyu mama hawezi kunichafua namna hii, hivyo tuachie hapo hapo ili nijipange,” alidai Bw. Mrema.

Awali, wakati akichangia katika hotuba ya Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Mambo ya Ndani kwa mwaka wa fedha 2011/12, Bi. Chiku Abwao aliionya serikali kuwa iliridhia mfumo wa vyama vingi, hivyo inapaswa kuhuheshimu na kuhituhumu kuwatisha wananchi hasa wa upinzani.

“Serikali imekuwa ikiwatisha wananchi hasa wa vyama vya upinzani ndiyo maana wabunge wa upinzani ambao walikuwa bungeni tangu 1995 pamoja na mimi, leo hii hawapo wamekata tamaa na kurudi CCM na wachache waliobakia ni mawakala wa CCM kama Mrema na Cheo,” alisema Bi. Abwao.

Katika mchango wake huo, Bi. Abwao licha ya kukatishwa na Mwenyekiti wa Kikao cha Bunge na kuambiwa asiyataje majina ya viongozi hao aliendelea kusisitiza kuwa kama wabunge wataendelea kuzuiliwa kuwasilisha hoja zao bungeni watalazimika kuziwasilisha kwa njia ya maandamano.

“Kwa mfumo huu wa sisi wabunge kuzuiwa kuwasilisha hoja zetu mbele ya bunge nchi itaelekea kubaya zaidi, tutakosa uvumilivu, na kama mtaendelea hivi tuziwasilisha hoja hizi hizi kwa wananchi kwa njia ya maandamano kwa kuwa tayari wametuunga mkono kwa asilimia kubwa ili popote mnapopita wawazomee,” alidai Bi. Abwao.

Hata hivyo mara baada ya gazeti hili kufanya mahojiano na mbunge huyo mjini Dodoma alisema tuhuma dhidi ya Bw. Mrema na Bw. Cheyo kuwa mawakala wa CCM ni za kweli kwa kuwa ushahidi wa kutosha anao.

“Ninayoyazungumza ninamaanisha na wala siwezi kuufurahisha umma, kwani hawa viongozi tangu nilipoingia katika mapinduzi ya vyama vingi 1992, Mrema tulimfuata sisi wenyewe hivyo hamna cha vyama vya upinzani bali hao ni mawakala tu wa CCM,” alidai Bi. Abwao na kuongeza:

“Hivi umewahi kumuona Mrema akiipinga CCM kama mpinzani hata siku moja, ni kwa sababu anajua yeye siyo mpinzani bali ni wakala tu wa CCM. Mfano mzuri ni ile kamati ya hesabu za serikali hakupaswa kupewa nafasi ya kuwa mwenyekiti, bali sisi CHADEMA ndiyo tulipaswa tuisimamie lakini vifungu vya kanuni vilibadilishwa mara moja na yeye kupewa nafasi hiyo.”

Majira ilipotaka kuwasiliana na Bw. Cheyo ili kupata ufafanuzi juu ya tuhuma hizo, simu yake ya mkononi ilikuwa inaita bila kupokewa.

MWISHO

6 comments:

  1. Mrema hata ajitee vipi yeye ni wakala wa CCM na hana tena mvuto katika jamii,kura za vunjo walimpa kwa kumuhurumia afya yake,anajikomba aone kama na yeye anaweza kupewa mafao ya waziri mkuu mstaafu kama alivyopewa maalimu Seifu,2015 kama atakuwepo hai Bunge alisahau kabisa.

    ReplyDelete
  2. Mzee Mrema nimetunza kadi uliyonipa ukiwa NCCR-MAGEUZI Nnachoshangaa Lyatonga huyu ni yuLeyule maanA kabadilika ile mbaya.Naona Ubunge kapewa zawadi na CCM NDO MAANA SIO MPINZANI TENA

    ReplyDelete
  3. Mrema ana hali mbaya sana kisiasa na kafya pia.
    Hoja zake za kuisifia CCM kila mara inaonyesha ukibaraka wake, na kwa hilo hachomoi, kwani hata mtoto mdogo anaweza kuhukumu nani mkweli kati yake na Abwao.
    Mimi nafikiri amekula rushwa ya kisiasa kwa kupewa ushindi wa ubunge na sasa analipa fadhila na pia anjiandalia mazingira ya baada ya ubunge maana hata TLP tumeshamchoka,hana jipya tena.
    Aondoke arudi CCM.

    ReplyDelete
  4. jamani,mwacheni,afya yake ni mgogoro.anahitaji utulivu wa hali ya juu,mkipandisha sukari yake,akiwafia,mchawi ni nyie mtakaomuuwa.mwacheni akae alivo,lazima uangalie mtu wa kulumbana nae,hasa kiafya.tunahitaji utulivu kwa hili Amen.

    ReplyDelete
  5. Kwa mtazamo tu wa nje hasa Mrema hana upinzani wa kweli maana yeye hata akiambiwa amchague raisi atachagua wa CCM sasa huyo mpinzani au msanii..Ktk hilo bwana Mrema asipinge wala asilete malumbano ndani ya bunge ukifatialia hotuba zake nyingi utakuta nakifagilia sana chama tawala.

    ReplyDelete
  6. Mrema hana maana
    kilichomwondoa sisiem siku hizo ni kihoro cha ubinafsi na masifa. alppoona huko wamemgundua uroho wake wa mdaraka na sifa akakimbilia upinzani. ameendeleza hayo na kwa hulika hiyo sisiem wame mpata tena awatumikie maana kwa ubinafsi wake ataingia kila mahali. hana lolote la maana.

    ReplyDelete