29 July 2011

Mbunge ataka pool utambuliwe

Na Mwandishi Wetu, Dodoma

MBUNGE wa Jimbo la Kibakwe mkoani Dodoma, ambaye pia ni Mwenyekiti wa vikao vya Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, George Simbachawene,   ameitaka
serikali kuutambua mchezo wa pool kama ilivyo michezo mingine.

Mbunge huyo aliyasema hayo jana wakati alipokuwa mgeni rasmi katika ufunguzi wa fainali za taifa za mashindano ya pool yanayojulikana kama Safari Lager Nationa Pool Championship 2011.

Fainali za mashindano hayo  zinashirikisha mikoa 14 ya Tanzania Bara, zimedhaminiwa na Kampuni ya Bia ya Tanzania (TBL), kupitia bia yake ya Safari Lager zinafanyikia kwenye ukumbi wa Kilimani mkoani Dodoma.

Simbachawene alisema kuwa,  awali kulikuwa na dhana ya kuwa mchezo wa pool ni mchezo wa   wahuni hadi serikali ikawa inafikiria kuuzuia, lakini dhana hiyo haipo tena, hivyo serikali haina budi kuupokea na kuutambua kama ilivyo michezo mingine ikiwemo soka.

“Naiomba serikali kuanzia sasa iutambue mchezo wa pool kama ilivyo michezo mingine kwani ni mchezo mzuri ambao unashirikisha watu wenye heshima zao, ikiwemo hata sisi wabunge ambao wiki iliyopita tuliucheza na kuufurahia,” alisema Simbachawene.

Alikitaka Chama cha Mchezo Pool Tanzania (TAPA),  kuhakikisha kinausajili mchezo huo kwa kutumia sheria ya mchezo wa ridhaa, badala kuusajili kama mchezo wa kamari.

“Mchezo wa pool ni mchezo wa kutumia akili na viwango, hivyo TAPA usajili mchezo huu kwa kutumia sheria ya mchezo wa ridhaa badala ya kuusajili kwa sheria ya mchezo wa kamari, na wanaotaka kucheza michezo ya kubahatisha (kamari) waende kwenye klabu za usiku,” alisema.

Mbunge huyo aliipongeza TBL kupitia bia ya Safari Lager  kwa kuweza kuupatia mafanikio makubwa  mchezo huo kutokana na udhamini wao .

Naye, mwakilishi wa kampuni  ya TBL mkoani Dodoma, Niki Tesha,  alisema mafanikio ya mchezo huo yametokana na kampuni hiyo kudhamini michezo nchini.

“Kampuni ya TBL  inadhamini na kujali michezo na ndiyo maana mchezo huo ambao zamani ulikuwa ukibezwa, umeweza  kupiga hatua na kufikia hapa ulipo,” alisema Tesha.

Ufunguzi wa fainali hizo ulihudhuriwa na Afisa Michezo Mkoa wa Dodoma, Patrick Ernest,   na Afisa Utamaduni wa Mkoa huo, Abuu Layya.

No comments:

Post a Comment