13 July 2011

Lady Jaydee kuwazawadia mtalimbo Yanga leo

Na Zahoro Mlanzi

MWANAMUZIKI mahili wa muziki wa kizazi kipya (Bongofleva), Judith Wambura 'Lady Jaydee', atawaburudisha mabingwa wapya wa mashindano ya
Kagame Castle Cup, Yanga, katika hafla ya chakula cha jioni itakayofanyika leo katika ukumbi wa Nyumbani Lodge, Dar es Salaam.

Lady Jaydee, kwa sasa anatamba na kibao chake kipya cha mtalimbo, akiwa na bendi yake ya Machozi.

Yanga ilitwaa ubingwa huo Jumapili katika mchezo wa fainali uliopigwa Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam kwa kuifunga Simba bao 1-0 na kutwaa kombe, medali za dhahabu na dola 30,000.

Akizungumza katika Makao Makuu ya klabu hiyo Mtaa wa Jangwani, Dar es Salaam, jana, Katibu Mkuu wa klabu hiyo, Selestine Mwesigwa, alisema hafla hiyo itahusisha wachezaji na benchi la ufundi, ikiwa ni kuwapongeza kwa kutwaa ubingwa Kagame Castle Cup.

"Yanga kwa kushirikiana na mwanamuziki Lady Jaydee tumeandaa chakula cha jioni, mara baada ya kumaliza hafla hiyo, wachezaji watakwenda mapumziko na watarudi kambini Julai 20, mwaka huu," alisema Mwesiga.

Alisema anawapongeza watu wote walioshiriki katika kufanikisha timu yao kutwaa ubingwa wa Kagame Castle Cup na kwamba, watahakikisha wanajipanga kutwaa vikombe zaidi.

Mbali na hilo, Mwesigwa pia aliwapongeza watani zao wa jadi, Simba kwa kushika nafasi ya pili katika michuano hiyo na kutamba itaendelea kuwa wa pili kwani imeshafanya hivyo katika mashindano ya Muungano na Ligi Kuu Bara.

Katika hatua nyingine, Mwesigwa alizungumzia wachezaji wao Nadir Haroub 'Canavaro', Haruna Niyonzima na Oscar Joshua ambao wamekuwa wakipigiwa simu kutokana na taarifa zao mbalimbali.

Alisema kuhusu suala la Canavaro kuhitajika na El Merreikh ya Sudan, hilo suala halijafika kwao rasmi kwa maana ya kimaandishi, lakini yanazungumzwa mengi na vyombo vya habari.

"Ukiachilia mbali hilo, suala la Haruna Niyonzima nalo limekwisha kwani Katibu Mkuu wa APR tayari ametupa barua rasmi tangu Alhamisi ikimruhusu mchezaji huyo kubaki nasi, kilichobaki ni taratibu nyingine," alisema Mwesigwa.

Aliongeza, suala la Joshua na timu yake ya Ruvu Shooting, wao wamemalizana kwa kukamilisha kila kitu ikiwemo kulipa fedha zao, lakini walizikataa wakati tayari wametoa barua ya kumruhusu kuichezea timu hiyo.

1 comment:

  1. Sawa Yanga msiishie kufanya sherehe tu pia mkumbuke yakuwa sasa hivi mna pesa za kutosha hivyo mkumbuke pia kumpeleka mchezaji wenu Mwasika huko India kwa matibabu ya goti lake.Zinahitajika millioni saba tu na hizo fedha mnazo.Msije mkaanza kuleta visingizio na kuilalamikia TFF.Hilo ni jukumu lenu.

    ReplyDelete