Na Mwali Ibrahim
TIMU ya taifa ya mchezo wa judo ya nchini Kenya imewasili jana kwa ajili ya kujiandaa na mashindano ya Kanda Tano Afrika Mashariki ya mchezo yanayotarajia
kufanyika Julai 17 hadi 18 katika ukumbi wa Landmark, Ubungo Dar es Salaam.
Sambamba na timu hiyo, pia baadhi ya wachezaji wa timu ya Taifa ya Burundi wamewasili jana, huku wengine wakitarajiwa kuwasili kesho.
Akizungumza Dar es Salaam jana, Katibu Mkuu wa Chama cha Mchezo wa Judo Tanzania (JATA), Kashinde Shabani, alisema nchi za Zambia, Uganda na Zanzibar bado hazijawasili.
Alisema kwa upande wa timu ya Taifa ya Tanzania, inaendelea na maandalizi yake katika kambi yao iliyopo shule ya Sekondari ya Filbert Bayi, Kibaha mkoani Pwani.
"Hatujapata taarifa ya nchi nyingine kuwasili, lakini kila timu imethibitisha kushiriki isipokuwa Rwanda ambayo ilijitoa mapema kutokana na kukosa fedha na kusaidiwa na serikali yao, ingawa ilikuwa tayari imethibitisha," alisema Shabani.
Katibu huyo alisema kila nchi itakuwa na wachezaji 23 na viongozi wawili ili kuweza kufanikisha kila kitu cha muhimu katika michuano hiyo.
Alisema kutokana na mashindano hayo kuwa ya uzito, wamezingatia kila nchi kutoa wachezaji wa kila uzito ili kuwa na ushindani mzuri.
No comments:
Post a Comment