Na Zahoro Mlanzi
MICHUANO ya Kagame Castle Cup imeingiza sh. 1,073,566,000 kwa mechi zote zilizochezwa katika viwanja vya Taifa, Dar es Salaam na Jamhuri mjini Morogoro.Katika
michuano hiyo mechi ya fainali iliyowakutanisha watani wa jadi Simba na Yanga iliyochezwa juzi Uwanja wa Taifa ndiyo iliyoingiza fedha nyingi kuliko zote ambapo zilipatikana sh. 354,554,000.
Mashindano hayo yalianza kutimua vumbi Juni 26, mwaka huu katika vituo viwili vya Dar es Salaam na Morogoro ambapo mabingwa wa Tanzania Bara, Yanga ndiyo iliyotwaa ubingwa huo kwa kuifunga Simba bao 1-0.
Akizungumza Dar es Salaam jana, Katibu Mkuu wa Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF), Angetile Osiah alisema anashukuru mashabiki, wadau, serikali na wadhamini kwa kufanya mashindano hayo yawe na mafanikio makubwa kwa mwaka huu.
"Mashindano yamekuwa na mafanikio makubwa ambapo kwa upande wa mapato, jumla ya sh. 1,068,638,000 zilipatikana kwa Kituo cha Dar es Salaam tangu yalivyoanza na kwa Morogoro ni sh. 4, 528,000," alisema Osiah.
Alisema mapato yaliyopatikana Morogoro ni mengi kutokana na timu zilizocheza huko ambazo zilikuwa ni za kigeni, hivyo kupata mapato kama hayo ni jambo la kujivunia.
Akizungumzia mapato ya fainali kati ya Simba na Yanga, alisema imeingiza sh. 354,554,000 kutokana na watazamaji 56,626 ambao walijitokeza siku ya mchezo.
Alisema mchanganuo mwingine kuhusu timu zimepata kiasi gani, gharama za mchezo, makato ya uwanja, vyama vya mpira wa miguu na mambo mengine utatolewa baada ya kukamilika kwa mchanganuo huo.
Wakati huohuo, Osiah aliongeza kwamba wanawaomba radhi mashabiki wote waliokuwepo uwanjani kutokana na kukatika kwa umeme, kwani walijitahidi kadri ya uwezo wao kulitatua tatizo hilo bila mafanikio.
Katika hatua nyingine, Osiah alisema wachezaji 13 wa timu ya Red Sea ya Eritrea wametoweka nchini baada ya wenzao kuondoka Jumamosi kurudi kwao.
"Timu iliondoka Jumamosi baada ya Ijumaa kufungwa na ilikuwa na msafara wa watu 26, wenzao baada ya kuondoka ikagundulika kuna wachezaji 13 wamebaki nchini lakini tayari tumeshatoa taarifa kwa chombo husika," alisema Osiah.
Hongela Ynga watoto wa jangwani, huo ndio uzalendo wa vijana
ReplyDelete