12 July 2011

Mr. II afikishwa mahakamani

Na Charles Mwakipesile Mbeya

MBUNGE wa Jimbo la Mbeya Mjini, Bw. Joseph Mbilinyi (CHADEMA),  amepandishwa kizimbani katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Mkoa wa Mbeya kujibu mashtaka
la kufanya mkutano bila ya kibali cha polisi.

Mbunge huyo maarufu kama Mr. II alifikishwa mahakamani chini ya ulinzi mkali wa polisi saa 3.00 asubuhi.

Mbele ya Hakimu Mkazi Mfawidhi wa Mahakama ya Mkoa, Bw. Michael Mtaite, ilidaiwa na upande wa mashtaka kuwa mbunge huyo alikusanya watu bila kibali cha Ofisa Mfawidhi wa Jeshi la Polisi, jambo ambalo ni kinyume sheria.

Mwendesha Mashtaka, Bw. Apimak Mabrouk alidai kuwa Julai 8, mwaka huu mbunge huyo alifanya kosa hilo na kuwahutubia bila ya kibali cha  cha polisi.

Alidai kwa kufanya hivyo alikiuka kifungu cha 43 (i) na 46 (ii) (A) na Sheria ya Jeshi la Polisi sura ya 322 ya mwaka 2002.

Mbali na mbunge huyo, pia waliosomewa mashtaka ni pamoja na
Mwenyekiti wa chama hicho Wilaya ya Mbeya, Bw. John Mwambigija maarufu kwa jina la 'mzee wa upako' na Bw. Job Manyerere.

Washtakiwa wote walikana mashtaka. Upande wa mashtaka ulidai upelelezi wa kesi hiyo umekamilika na hivyo kinachotakiwa ni mahakama kupanga tarehe ya kuanza kusikilizwa.

Hakimu, Mtaite alisema dhamana kwa watuhumiwa iko wazi kwa ajili ya kutoa nafasi kwa Bw. Mbilinyi kuendelea na vikao vya Bunge. Kesi hiyo imepangwa kuanza kusikilizwa Agosti 6, mwaka huu.

Washtakiwa wote walipata dhamana baada ya kujidhamini
kwa sh.100,000 kila mmoja.

Baada ya kupata dhamana walikwenda moja kwa moja kwenye magari yao na kuondoka na polisi waliokuwa wameimarisha ulinzi wakatawanyika.

Mbunge huyo alikamatwa na polisi juzi kwa kile kilichodaiwa  kuhutubia wananchi wa kata ya Nzovwe bila ya kibali.

Huu ni mwendelezo wa wabunge wa upinzani kukamatwa na kushtakiwa kwa sababu mbalimbali, nyingi zikiwa za kuitisha mikutano au maandamano bila kibali.

Hivi karibuni Mbunge wa Viti Maalumu (CUF), Bi. Magdalena Sakaya alikamatwa na kushtakaiwa mkoani Babora, Mbunge wa Singida Mashariki, Tundu Lissu na mwenzake wa Viti Maalumu, Esther Matiko wanashtakiwa mkoani Mara wakituhumiwa kufanya uchochezi katika kushughulikia mazishi ya raia waliouawa kwa kupigwa risasi na polisi katika mgodi wa North Mara.

Mbali na wabunge hao, wabunge wengine wa CHADEMA waliokwisha kukamatwa na polisi ni Kiongozi wa Kambi ya Upinzani na Mwenyekiti wa chama hicho, Freeman Mbowe, Godbless Lema (Arusha Mjini), Joseph Selasini (Rombo) na Philemon Ndesamburo (Moshi Mjini). Mbunge wa Kigoma Kaskazini, Bw. Zitto Kabwe alikamatwa kwa muda na kuachiwa baadaye kwa kuzidisha muda wa mkutano wake mkoani Singida mwezi uliopita.

3 comments:

  1. siku zote kizuri lazima kifatiliwe hukiona hufatiliwe ujue hakuna dili so chadema songeni mbele.

    ReplyDelete
  2. sio kihivyo na ndio maana hata serikali ya Marekani imeleta sheria ya ugaidi na kwa kila anayeshukiwa hukamatwa lengo lao ni kulinda usalama na ndvyo ilivyo kwa vyombo vya usalama kuwafuatilia wale ambao wana element za uvuragaji amani kama huyu Mr II. wananchi wa Mbeya mjini mmechemsha kuweka galasa likuongozeni.

    ReplyDelete
  3. naona Tanzania mshaanza uongozi wa kiimla kama ule Moi Kenya. Poleni sana

    ReplyDelete