04 July 2011

CUF: Ngeleja aachie ngazi

*Wasema ameshindwa kumaliza tatizo la umeme
*Wahoji JK kutafuta wawekezaji kwenye giza


Na Godfrey Ismaely

SAKATA la mgawo wa umeme unaoendelea katika maeneo mbalimbali hapa nchini limeendelea kuibua mapya huku Chama cha Wananchi (CUF) kumtaka
Waziri wa Nishati na Madini, Bw. William Ngeleja kujiuzulu kwa kushindwa kusimamia TANESCO kudhibiti mgawo huo.

Hayo yalisemwa jana jijini Dar es Salaam na Naibu Katibu Mkuu wa Chama hicho Tanzania Bara, Bw. Julius Mtatiro wakati akitoa taarifa juu ya mgawo unaoendelea hapa nchini.

"CUF tunamtaka Waziri wa Nishati na Madini William Ngeleja ajiuzulu kwani ameshindwa kusimamia TANESCO walau katika mfumo huo huo mbovu wa serikali ya CCM, ili apewe mtu mwingine ambaye anaweza kujaribu kuiondoa Tanzania kwenye tatizo la mgawo wa umeme usiokwisha," alisema Bw. Mtatiro.

Aidha alisema kuwa kitendo cha waziri huyo cha kuendelea kung'ang'ania kuongoza wizara hiyo wakati inaonesha wazi kuwa imemshinda ni dhahiri kwamba TANESCO kuna maslahi yake na wala hafikirii kuwahudumia Watanzania.

"Kuendelea kung'ang'ania madarakani kwa Bw. Ngeleja inaonesha wazi kuwa TANESCO kuna maslahi yake ilihali wizara tayari imemshinda na ni ishara ya wazi kwamba kwa mfumo huo hawafikirii hata kidogo Watanzania bali maslahi yake binafsi," alisema Bw. Mtatiro.

Wakati huo huo CUF imetamka kuwa mgawo wa umeme hapa nchini unachangiwa na chama tawala (CCM) kwa kufikia ukomo wa kufikiria namna ya kutatua kero za wananchi, huku Rais Jakaya Kikwete akiwa anatafuana fedha za umma kwa safari za nje kwa madai anaenda kuonana na wawekezaji ili waje kuwekeza kwenye nchi isiyokuwa na umeme.

"Sababu zimekuwa zile zile za uongo wa kila namna mabwawa hayajajaa, mitambo imeharibika, mafuta yameisha, hizi kwetu ni sababu za kijinga sana kwa nchi ambayo imepata uhuru wake kwa miaka 50 iliyopita, huku ikiwa na viongozi waliosoma kila aina ya elimu pamoja na rasilimali za kutosha zilizopo hapa nchini," alisema Bw. Mtatiro.

Bw. Mtatiro alisema kuwa pamoja na hali ngumu ya upatikanaji wa umeme Rais Kikwete kupitia hotuba yake ya kufunga mwaka 2010, aliwajulisha wananchi kuwa katika kipindi cha miaka mitano 2005 hadi 2010 TANESCO kupitia msaada wa serikali iliongezewa uwezo wa kuzalisha umeme kwa Megawati (MW)145 (MW 100 Ubungo na MW 45 Tegeta) kwa kutumia gesi asilia hali inayoonesha udhaifu.

"Hali halisi Rais ameendelea kuhaidi utekelezaji wa miradi mingine kadhaa inayotoa takribani megawati 1,130 katika kipindi cha 2011 hadi 2013, jambo ambalo litakuwa maajabu ya dunia. Serikali iliyoongeza uzalishaji wa megawati 145 kwa kipindi cha miaka mitano itaweza vipi kuzalisha megawati 1,130 katika kipindi cha miaka mitatu tu? Watanzania wanadangaywa kweupe tena bila chembe ya aibu," alisema Bw. Mtatiro na kuongeza.

"Serikali ya CCM, Wizara ya Nihati na Madini na TANESCO wanaendelea kuua uchumi wa Watanzania kutokana na uzembe hasa kwa kushindwa kutafuta suluhisho la matatizo makubwa ambayo ni misingi ya ahueni ya kiuchumi mahali popote hali inayodhirisha wazi kuwa wana udhaifu mkubwa na hata mtu mwenye ubongo mzuri anapojaribu kuwasaidia watanzania kupitia CCM anafeli kabla hajaanza," alisema Bw. Mtatiro.

Aliongeza: "Watanzania wasitafute mchawi wa mgawo wa umeme, mchawi wanamjua vizuri sana – Rais Jakaya Mrisho Kikwete, Serikali ya CCM na Waziri wa Nishati na Madini Bw. Ngeleja."

Alisema kuwa licha ya hali ya mgawo inayoendelea kwa sasa Rais ameendelea kutumia fedha nyingi za umma kwa ajili ya kufanyia safari za nje dhumuni likiwa ni kuwatafuta wawekezaji ambao hajui wakifika hapa nchini watatumia nishati gani ili kuendeshea shughuli zao kwa kuwa mgawo umeendelea kushika kasi.

"Kwa maana nyingine kama Rais anapotafuta fedha za umma kwa safari za nje 'kiguu na njia' kwa ajili ya kuonana na wawekezaji ili kuwashawishi waje kuwekeza hapa nchini anawahadaa ama kuwadanganya kwani hadi sasa wawekezaji waliopo ukiongeza na zaidi ya asilimia 10 ya nyumba zilizounganishiwa umeme wapo katika mgawo mkubwa ambao hauna ukwamo," alisema Bw. Mtatiro.

Alisema chama hicho kinamshauri Rais Kikwete aachane na safari zake zinazomfanya kupoteza muda kwa ajili ya kwenda kuwasaka wawekezaji nje ya nchi kwa kuwa walioko kwa sasa serikali imeshindwa kuwapatia umeme wa uhakika.

"Gharama anazotumia kwenda kutafuta wawekezaji ni kiini macho tu kwa sababu duniani haijawahi kutokea wawekezaji wenye mitaji yao ya uhakika kuja kuwekeza gizani.

"Gharama anazotumia kwenda kutafuta wawekezaji ni kiini macho kwa sababu duniani kote hajawahi kutokea mwekezaji au wawekezaji wenye mitaji yao ya uhakika kwa ajili ya kwenda au kuja kuwekeza gizani," alisema Bw. Mtatiro na kuhitimisha:

"Kwa kifupi mgao wa umeme usiokwisha ni sawasawa na shetani litialo umasikini kwa jamii ya watu ambao tayari ni masikini. Na kwa hakika, Serikali ya Tanzania imebadilisha umeme kutoka kuwa tatizo linalotatuliwa hadi kuwa janga la taifa.

Juhudi za gazeti hili kumtafuta Waziri Ngeleja kupata maoni yake zilishindikana jana baada ya simu yake kutopatikana.

No comments:

Post a Comment