LA PLATA, Argentina
TIMU ya taifa ya Brazil imeanza vibaya michuano ya kuwania Kombe la Copa America, baada ya kulazimishwa kwenda suluhu na Venezuela zikiwa ni siku
mbili baada ya wenyeji wa michuano hiyo, Argentina kufanya hivyo.
Kwa mujibu wa Shirika la Habari la Marekani (AP), katika mchezo huo wa kundi B uliofanyika juzi mjini La Plata, Venezuela ambayo inafahamika kuwa ni dhaifu katika ukanda wa Marekani ya Kusini ilijaza viungo ili kuweza kuzuia mashambulizi ya Brazil, licha ya mabingwa hao mara tano wakicheza kwa kuelewana ikiwatumia wachezaji wenye vipaji Neymar, Robinho na Alexandre Pato.
“Hatukuweza kumalizia vizuri kwani tumepoteza nafasi nyingi nzuri,” alisema Neymar. "Lakini kwa sasa tutajipanga ili tuweze kushinda,” aliongeza mchezaji huyo.
Kwa upande wake kocha wa Brazil, Mano Menezes aliweka wazi kuwa matokeo hayo ni mabaya kwao na yanashangaza katika soka, kwani walikosa nafasi nyingi hususani kipindi cha kipindi cha pili.
Ijumaa uliyopita Argentina walitoka sare ya bao 1-1 na Bolivia, katika mechi ya ufunguzi wa michuano hiyo na inavyoonekana Brazil ambayo iliichapa Argentina katika mechi mbili za fainali, huenda zikakutana kwenye mechi ya fainali itakayofanyika Julai 24 mwaka huu.
Wakati timu ya taifa ya wanaume ikibanwa mbavu, kwa upande wao timu ya wanawake ilikuwa ikitakata kwenye michuano ya fainali za Kombe la Dunia, inayoendelea nchini Ujerumani baada ya kufanikiwa kuilaza Norway mabao 3-0 hivyo kushika usukani wa kundi D.
Alikuwa ni Marta, mchezaji mahiri wa Brazil aliyeweza kuipatia timu yake ushindi huo, baada ya kufunga mabao mawili na kusaidia kupatikana kwa bao jingine lililofungwa na Rozana.
Kabla ya mchezo huo, awali wawakilishi wa Afrika, Guinea ya Ikweta ilishindwa kufurukuta mbele ya Australia, baada ya kuchabangwa mabao 3-2.
No comments:
Post a Comment