11 July 2011

CHADEMA: Tanzania ijifunze kutoka Sudan

Na Mwandishi Wetu

SIKU moja baada ya nchi mpya ya 54 barani Afrika na ya 193 duniani ya Jamhuri Sudan Kusini kuzaliwa kwa kupata uhuru wake kutoka Sudan Kaskazini, Chama cha
Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) kimetuma salamu za pongezi, huku kikiitaka serikali ya Tanzania kujifunza kutoka nchi hiyo namna ilivyoandaa mchakato wa kuwaunganisha watu kuamua mstakabali wa taifa lao.

Chama hicho kimetoa wito kwa Serikali ya Tanzania inayoongozwa na Rais Jakaya Kikwete ijifunze kutokana na matukio ya Sudan ili kuwaunganisha Watanzania kuwa na katiba mpya ambayo itarekebisha kasoro za kihistoria na kutoa mwelekeo muafaka wa kitaifa kwa ili kudumisha uhuru na umoja nchini.

Mbali ya hilo, chama hicho pia kimeihimiza serikali kupitia Wizara ya Mambo ya Nje na Mahusiano ya Kimataifa ya Tanzania, chini ya Bw. Bernard Membe kuharakisha kupanua ushirikiano wa kisiasa, kiuchumi na kijamii na Sudani Kusini, ambayo imeshaonesha nia ya kujiunga na Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC), ili kunufaika na fursa mbalimbali zilizoko katika nchi hiyo mpya.

Katika taarifa hiyo iliyosainiwa na Mkurugenzi wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa wa chama hicho, Bw. John Mnyika, chama hicho kimepongeza wananchi wa Jamhuri ya Sudani Kusini na chama tawala cha nchi hiyo, Sudanese People Liberation Movement(SPLM) kwa kupata uhuru na kuwa taifa jipya.

Kwa mujibu wa taarifa hiyo iliyotumwa kwa vyombo vya habari, kuundwa kwa taifa hilo ni matokeo ya kura ya maoni iliyofanyika Januari 2011, na kuwa uhuru huo umefungua ukurasa mpya wa amani na ustawi katika taifa hilo, ikiwa ni sehemu ya utekelezaji wa makubaliano mapana ya amani yaliyofikiwa mwaka 2005 baina ya vyama vya SPLM/SPLA na Serikali ya Sudani ili kusitisha vita na migogoro ya muda mrefu katika nchi hiyo.

Pia kimetoa wito kwa pande zote zinazohusika katika suala la mstakabali wa nchi hiyo mpya duniani kutumia njia za amani katika kutekeleza vipengele vilivyobaki vya makubaliano hayo ikiwemo kutatua masuala tete kama vile mgawanyo wa mapato, utata kuhusu maeneo ya Abyei, Milima ya Nuba, Kordofani Kusini, Blue Nile na masuala mengine yenye mvutano.

"Kurugenzi ya Mambo ya Nje na Mahusiano ya Kimataifa ya CHADEMA inatambua kwamba kuna changamoto nyingi zilizojitokeza mpaka kufikia hatua ya kuzaliwa kwa Jamhuri ya Sudani Kusini ambazo Watanzania wanapaswa kuzitafakari mathalani uwepo wa lindi la umaskini kwenye nchi yenye rasilimali hususani mafuta; uhasama kutokana na mipasuko ya kijamii na mivutano ya migawanyo ya mapato.

“Ni vizuri serikali ya Tanzania ikazingatia kwamba baadhi ya changamoto hizi zimeanza kujitokeza katika taifa letu hususani kwenye migogoro ya kirasilimali katika maeneo mbalimbali ya nchi, kero mbalimbali za muungano baina ya Tanganyika na Zanzibar na pia katika mjadala wa Shirikisho la Afrika ya Mashariki, hivyo uchambuzi wa kina ufanyike na tahadhari za mapema ziweze kuchukuliwa.

"Kurugenzi inaitaka serikali kuchukulia kwa umakini na utashi mchakato wa kuandikwa kwa katiba mpya ili uweze kutoa fursa ya kuwa na muafaka wa kitaifa utakaoweka misingi ya kushughulikia changamoto hizo ili kuepusha Tanzania kupitia njia ambayo Sudan imepitia katika kipindi cha takribani miaka 50," alisema Bw. Mnyika katika taarifa yake hiyo.

No comments:

Post a Comment