11 July 2011

Wajumbe wa NEC-CCM kuchaguliwa wilayani

Na Suleiman Abeid, Shinyanga
 
CHAMA Cha Mapinduzi (CCM) kimetangaza utaratibu mpya wa kuwapata wajumbe wake wa Halmashauri Kuu ya Taifa (NEC), ambapo hivi sasa watachaguliwa katika
mikutano mikuu ngazi ya wilaya.
 
Naibu Katibu Mkuu wa CCM (Bara), Bw. John Chiligati alitangaza utaratibu huo hivi karibuni mjini hapa, akisema una lengo la kuwawezesha wajumbe watakaochaguliwa kuwajibika zaidi na kudhibiti vitendo vya rushwa.

Bw. Chiligati alisema utaratibu huo mpya utaanza kutumika mwakani wakati wa uchaguzi wa ngazi zote ndani ya CCM.

Alisema CCM imeona utaratibu wa awali ambao sehemu kubwa ya wajumbe wa NEC walikuwa wakichaguliwa na Mkutano Mkuu wa CCM Taifa, na ulisababisha wajumbe waliochaguliwa kutowajibika kikamilifu kwa wanachama kwa kuwa hawakuwa wamewachagua, na wengine walikuwa na tabia ya kuzunguka mikoani kuwanunua wajumbe.

“Kuanzia uchaguzi ujao, wajumbe wa NEC sasa watachaguliwa katika ngazi ya wilaya kila wilaya itatoa mjumbe mmoja mmoja, tumeamua kurejesha jukumu hili katika ngazi ya chini," alisema.

“Utaratibu wa awali sehemu kubwa ya wajumbe wa NEC walipigiwa kura na wajumbe wa mkutano wa CCM wa Taifa kitu ambacho ilikuwa rahisi kwa wagombea kuwazungukia wote kabla ya siku ya uchaguzi," alisema na kuongeza;

“Tumebaini utaratibu huu hautufai unasababisha wajumbe kutowajibika kikamilifu kwa wanachama."

Kwa upande mwingine, Bw. Chiligati alikemea tabia ya baadhi ya viongozi ndani ya CCM ambao baada ya kuchaguliwa kushika nyadhifa mbalimbali husahau kuwatumikia wanachama.

Aliwataka viongozi wa CCM kuacha kuvaa makoti ya uongozi kwa mbwembwe na kwamba kuanzia sasa chama hicho hakitawavumilia.

Alisema katika kukabiliana na viongozi wenye tabia hiyo, CCM imeamua kurejesha utaratibu wa zamani wa kuwa na tume ya maadili ya viongozi badala ya kamati za maadili ambazo wajumbe wake wengi walikuwa ni viongozi hao hao ndani ya CCM.
 
“Tumeamua hivi sasa kurejesha utaratibu wa zamani wa kuwa na Tume ya maadili ya viongozi, wajumbe wa tume hizi hawatatokana na viongozi wa ndani ya CCM ambapo kwa ngazi ya Taifa watakuwa ni marais na mawaziri wastaafu na wazee wengine maarufu
ndani ya Chama,”

2 comments:

  1. ccm ijirekebishe kwa kushirikisha wananchama wake wote katika kutafuta mustakabali wa kuiongoza badala ya marekebisho kufanywa na viongozi wachache tu.........viongozi wote serikalini waondolewe katika shughuli za chama katika ngazi zote ili kuleta uwajibikaji zaidi

    ReplyDelete
  2. Pambaf! Hao jamaa wana mihela ya kuzunguka nchi nzima hata kwa siku mmoja tu! Ndio kwanza mnasambaza kansa ya rushwa hadi ngazi za chini kabisa! Kama ni kwa ajli ya rushwa, TAKUKURU haipo? Wakamateni muwafunge muone kama rushwa haitaisha. CCM mmekosa wataalam kiasi hiki? Kweli mmekwisha!

    ReplyDelete