11 July 2011

Kujivua gamba CCM hatihati

*Makamanda wa shughuli waanza kurudi nyuma
*Siku 90 zayeyuka, kikao NEC maswali magumu


Na Tumaini Makene

WAKATI Watanzania wakisubiri kwa hamu kikao cha Halmashauri Kuu ya Taifa (NEC) ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) ambacho
kinatarajiwa kufanya maamuzi magumu, ikiwemo kuwachukulia hatua makada wake wanaotuhumiwa kwa tuhuma mbalimbali za ufisadi, imebainika mpaka sasa chama hicho hakijapangwa kitafanyika lini licha ya siku 90 zilizoahidiwa awali kukamilika.

Katika maamuzi yake ya kikao kilichopita, hasa juu ya tathmini ya uchaguzi mkuu wa 2010, iliamuriwa kuwa CCM kiongeze kasi ya mapambano dhidi ya viongozi na wanachama wanaojihusisha na rushwa, wakitakiwa wawajibike wenyewe kwa maslahi ya chama na wasipofanya hivyo chama kiwawajibishe kwa maslahi ya chama na nchi.

Kwa mujibu wa taratibu za CCM, vikao vya NEC vya kawaida hufanyika mara moja kila baada ya miezi minne, ingawa pia inaweza kufanya mkutano usiokuwa wa kawaida wakati wowote kunapotokea haja au kunapokuwa na maelekezo ya kikao cha juu kufanya hivyo.

Kwa kufuata utaratibu huo na kuzingatia kuwa NEC ya CCM ilifanya kikao chake cha mwisho Aprili 10, mwaka huu, ilitarajiwa kuwa chombo hicho cha juu katika kufanya maamuzi ya chama kitakutana wakati wowote Julai, au mwanzoni mwa Agosti mwaka huu.

Utaratibu wa kuitisha kikao cha dharura ulitarajiwa pia kutumika kwa sababu mojawapo ya maamuzi yaliyopaswa kutekelezwa ni pamoja na umuhimu wa suala lenyewe la kuwabana makada wanaodaiwa kukisababisha kupoteza mvuto mbele ya jamii.

Kutokana na kauli mbalimbali za viongozi waandamizi wa CCM, makada ambao wanaonekana kulengwa na maamuzi hayo ya kujivua gamba ni pamoja na Mbunge wa Monduli, Bw. Edward Lowassa, Mbunge wa Bariadi Magharibi Bw. Andrew Chenge na Mbunge wa Igunga, Bw. Rostam Aziz.

Awali ilielezwa kuwa shughuli ya kuvuana gamba ndani ya chama ingefanyika siku 90 baada ya kikao cha Aprili, baadaye kauli hiyo ikabadilishwa kuwa hazikutajwa siku, bali ingetegemea kikao cha NEC kinachofuata.

Akizungumza jana kwa njia ya simu na Majira, Katibu wa Itikadi na Uenezi wa CCM, Bw. Nape Nnauye ambaye amekaririwa mara kadhaa akisisitiza kuwa hatua dhidi ya makda hao haikwepeki, alisema jana kuwa mpaka sasa sekretarieti ya chama hicho haijapanga ratiba ya kikao kijacho cha NEC na haijulikani itapangwa lini.

Kwa kawaida moja ya majukumu ya sekretarieti ya CCM, ambayo mwenyekiti wake ni Katibu Mkuu, ikiwa na wajumbe wakiwemo Manaibu Katibu Mkuu wa CCM, Katibu wa Halmashauri Kuu ya Taifa wa Oganaizesheni, Katibu wa Halmashauri Kuu ya Taifa wa Itikadi na Uenezi, Katibu wa Halmashauri Kuu ya Taifa wa Mambo ya Siasa na Uhusiano wa Kimataifa, Katibu wa Halmashauri Kuu ya Taifa wa Uchumi na Fedha, Makatibu Wakuu wa Jumuiya za CCM, ni pamoja na kusimamia shughuli zote za utendaji na kuandaa shughuli za vikao vya chama katika ngazi ya taifa.

Majira lilitaka kujua kutoka kwa Bw. Nnauye ukweli wa habari kuwa sekretarieti ya CCM imeshakutana kupanga ratiba ya kikao kijacho cha NEC, lakini pia kutaka kujua kitafanyika lini hasa ikizangatiwa kuwa kumekuwepo na mshawasha mkubwa katika jamii juu ya kikao hicho, hasa juu ya maamuzi kinachotarajiwa kuyafanya.

"Hatuna ratiba...hatujapanga ratiba ya kikao hicho cha NEC na haijulikani kitafanyika lini...hizo habari kuwa sekretarieti imekutana kupanga kikao cha NEC si za kweli. Hakuna document zinazoonesha hivyo. Kwa kweli sijui sekretarieti itakutana lini na kikao cha NEC kitafanyika lini. Hatujapanga vikao hivyo, hivyo siwezi kupanga wala kubuni hapa

Akizungumzia juu ya maamuzi 26 ya NEC iliyopita ambayo yanahusu mabadiliko makubwa, alisema "tatizo waandishi mmeamua kufuatilia moja tu la kuwavua watu...lakini hata hilo tulisema wazi kuwa tunawavua watu nafasi zao katika vikao vya maamuzi ya chama... sisi kama chama hatuna haja ya kuwawajibisha kisheria, bali tutawawajibisha kisiasa, kwani hatuna ushahidi wa kisheria kama wengine wanavyotaka.

Uchunguzi wa Majira umebaini kuwa baadhi ya watuhumiwa waliotarajiwa kujiuzulu kutoka katika uongozi hakuna ambaye yuko tayari kufanya hivyo, na kwamba hata uongozi wa CCM wameanza kurudi nyuma katika kutekeleza azma yao.

Hivi karibuni ilielezwa kwenye vyombo vya habari kuwa watuhumiwa watatu ambao majina yao yalitajwa na wajumbe kwenye NEC ya Aprili waliitwa na kuhojiwa na Makamu Mwenyekiti wa CCM (Bara), Bw. Pius Msekwa kuhusiana na tuhuma dhidi yao lakini hakuna taarifa yoyote rasmi iliyotolewa na chama hicho kuhusu mahojiano hayo.

Hivi karibuni akizungumza na wanachama wa CCM, mkoani Morogoro, Katibu Mkuu wa CCM, Bw. Wilson Mukama alinukuliwa akisema kuwa 'lazima wavue gamba' ambapo alifafanua kuwa yeye ni sawa na mtu aliyeteuliwa kufanya kazi ya kunyonga baada ya mahakama kupitisha hukumu, hivyo hataogopa kutekeleza hukumu hiyo.

Alinukuliwa zaidi akisema kuwa uamuzi wa ngazi za juu wa CCM ukishatolewa kuhusu kuvua gamba watuhumiwa wa ufisadi, hakuna kiongozi atakayepuuza kuutekeleza.

"Ufisadi unasemwa dhahiri na wananchi kwa kuwataja watuhumiwa hadharani wakiwahusisha na EPA (Akaunti ya Malipo ya Nje ya Benki Kuu), Dowans, ununuzi wa rada na Richmond, na vikao vya chama vimetoa uamuzi. Kilichobaki ni utekelezaji tu, na hukumu ikishatolewa na mahakama hakuna njia nyingine isipokuwa kutekeleza agizo hilo," alisema Bw. Mkama akinukuliwa katika moja ya magazeti ya kila siku.

Katika nukuu hiyo, Bw. Mkama aliongeza kusema kuwa hakuna mwananchi asiyejua kuwa ndani ya CCM wapo viongozi wenye nyadhifa kubwa wanaotuhumiwa kwa ufisadi kuanzia wa EPA, Richmond, Dowans, Rada na kashfa nyingine.

13 comments:

  1. Tatizo la Chama chetu blaa blaa ni nyingi sana. Mimi sioni sababu ya Mwenyekiti kutamka kabisa siku tisini angesema tu wahusika wajiondoe peke yao mapema kabla ya kuondolewa kwa nguvu bila ya kusisitiza siku 90 kwa sababu siku 90 zimeisha hatua za kweli zisipochukuliwa ni dharau na kebehi kubwa kwa chama kikubwa kama hiki. Tena haswa kwa Mwenyekiti. Tutaonekana kuwa kawaida maneno mengi tu vitendo hakuna. Haya mambo jamani hayaishii humu humu ndani ya nchi yanahojiwa hata nje ya nchi wenzetu wanasikilizia hatua gani zitachukuliwa sasa wakiona kimya hiyo ni kashfa kubwa kwa chama na haswa Mwenyekiti wake ataonekana ana mambo ya kiswahili swahili tu si mtekelezaji makini. Halafu hawa wakina Nape nao wameropoka ropoka saaana hatua zisipochukuliwa uso wao watauweka wapi?

    ReplyDelete
  2. hakuna jipya watu ni wale wale,chama ni kilekile,wanatufumba macho tusione.lakini inasikitisha sana inaonesha jinsi watu wasivyo makini ktk maamuzi,hii ni hatari sana.haya ndo maamuzi magumu aliyokua anayasema jamaa ingawaje ilionekana anajisafisha, lakini alichokiongea kulikua na ukweli ndani yake oooh!!! tz sijui inakwenda wapi

    ReplyDelete
  3. Yaani ni mtu tahira tu ndiyo anayeweza kuamini kwamba ccm ina ubavu wa kuwaondoa hao mafisadi watatu waliobobea. Hiyo ni ndoto to kwani viongozi karibu wote wa chama hicho ni mafisadi wa kutupwa. Ni nani atamng'oa mwenzie. Huyo mwenyekiti anajua wazi kwamba pesa iliyomfanya "ashinde" chaguzi zote mbili ilikuwa ya ufisadi. Viongozi wengi wa ngazi ya juu wa ccm walishiriki kuiba pesa za EPA, na nyinginezo kwa kutumia Deep Green (rangi za ccm), Kagoda, n.k. Wanajua wazi kwamba nchi sasa iko kwenye giza kutokana na pesa za hazina kutumika kwenye uchaguzi uliopita hata kuifilisi nchi. Wote ni wachafu na wanajua hilo. Ndio maana hawathubutu kumchukulia hatua fisadi yoyote.

    ReplyDelete
  4. Msitegemee kwamba mafisadi hao watajiangua uanachama kwa hiari yao. Wala msitegemee kwamba ccm itawang'oa kwani wote wameshiriki katika kuibia hii nchi. Vigogo (mafisadi) hao watatu wanayo confidence kubwa kwamba atakayejaribu kuwang'oa siri zake zitaanikwa wazi. Idadi kubwa ya vigogo wa sisiemu nimafisadi wakubwa. Nyie lieni tu wakati sisiemu wakiwangong'a. Mnayosikia wakisema ni porojo tu zisizo na ukweli wowote.

    ReplyDelete
  5. Nape acha uongo, kama hamna ushahidi juu ya hao mapacha watatu kuhusu ufisadi wao ni kwanini muwapoke nyazifa zao ndani ya chama chenu? Au mnafikiri watz wa leo ndio wale wa zamani, kwa sasa hatudanganyiki. Tunajua kwamba hao jamaa watatu hamuwezi kuwafukuza kwenye chama. Ni rahisi kumfukuza KIKWETE kwenye chama kuliko hao mapacha watatu kuwaondoa kwenye uongozi.Kifupi ccm ni chama cha kinafiki pamoja na viongozi wake!!!

    ReplyDelete
  6. najua CCM hawana nia ya kuwfukuza ila mazingira yanawalizimisha! Watawafukuza tu nyie subirini. Kwanza ni vita ya 2015 lazima kumwahi mwenzio ngwala pili wasipofanya hivyo watadharaulika zaidi na hii ni hatari kwa 2015, tatu wakiwaacha ni hatari kwa waliowatuhumu kwani watalipa kisasi kwa urahisi wakiwa ndani, nne katika mgogoro wowote lazima upande mmoja uonekana mshindi! Kwa kifupi kamwe hawa hawawezi kuishi pamoja tena!

    ReplyDelete
  7. Hawana jipya, mbwembwe tu!

    ReplyDelete
  8. Sasa hapa ndio utajua kama wananchi wana akili au la,Tusubiri uchaguzi wa 2015 Kanga,t-shirt,skafu vitagawiwa kwa watu pamoja na kupikiwa pilau na shillingi elfu kumi juu basi wajinga wameshasahau kila kitu utawaona wakishabikia ccm kama punguwani alafu baada ya muda kidogo tu wana anza kulia kuhusu viongizi waliowachaguwa wao wenyewe kuwa hawana msaada.Wananchi wanatakiwa kuamka sasa katika usingizi mzito.Mfano mzuri wala hauko mbali ni kwa majirani zetu Kenya tujiulize leo hii Kanu ikowapi na kwanini?

    ReplyDelete
  9. Tusubiri Uchaguzi ujao, Tanzania nayo ijivue gamba la CCM.Wakidhani kuwafukuza wenzao akina Lowasa na wenzake ndiyo CCM itakuwa SAFI, wanajidanganya. WaChukue tu Chao Mapema, CCM, mwisho wao tunaujua sisi Wananchi.

    ReplyDelete
  10. Bila tume huru ya uchaguzi,tunaota ndoto kuitoa ccm madarakani,labda maandamano!!!

    ReplyDelete
  11. Chonde chonde jamani tupiganieni tume huru ya uchaguzi.Bora katiba ichelewe lakin tupate tume huru ya uchaguzi in place.
    Mambo ya hao akina Kiravu na wenzie walivyo tufanyia uchaguz uliopita cpend hata kukumbuka make inatia hasira sana!!! watoke waende kupumzika hatuwataki kabisa!!!jamani watanzania tuungane tuwe ki2 kimoja tuwang;oe hao matapeli wa nchi hii!!

    ReplyDelete
  12. Anonymous said.....
    Tanzania inahitaji siasa safi za vitendo na siyo maneno matupu.
    July 12,2011

    ReplyDelete
  13. huyo nape ni mtoto wa mapacha watatu,wamemlea kapendeza,anajua mbwembwe za kutuliza wana-ccm; kama ana uchungu sana na nchi hii,naye ni cha mtoto,ajiuzulu madaraka alopewa awe tu mwana-ccm wa kawaida.asikae na cheo chochote,na asitegemee hao baba zake mapacha wana mpango wa kutoka walipo.aanze yeye kujiuzulu madaraka alopewa ndo tutajue na yeye mwanamme wa jando.watu wanapenda kula nchi hii.embu huyo dogo kwa hasira ajiuzulu yeye maana ni ndoto kwa hao pacha tatu.atulie.watampiga chini sasa hivi.

    ReplyDelete