06 July 2011

Andrew Chenge kikaangoni

*Wabunge waliokwenda London wataka ashtakiwe
*Waziri Mathias Chikawe azidi kumkingia kifua


Na Grace Michael, Dodoma

SAKATA la ununuzi wa rada ya ulioingizia serikali hasara, limechukua sura mpya baada timu ya wabunge iliyotumwa Uingereza kufuatilia malipo ya
fedha hizo kutoka Kampuni ya BAE kupendekeza kuangaliwa uwezekano wa kuwafikisha wahusika hao mahakamani.

Pendekezo la timu hiyo iliyokuwa chini ya Naibu Spika, Bw. Job Ndugai na wenzake Bw. Azan Zungu, Bi. Angela Kairuki na Bw. John Cheyo yamefanana na yaliyotolewa na Kambi ya upinzani bungeni juzi, kuwa wahusika katika kesi hiyo washtakiwe.

Kamati ya Ndugai ilisema kuwa pamoja na kesi hiyo kufungwa au kumalizika nchini Uingereza lakini Tanzania inayo nafasi ya kuwaburuta mahakamani watuhumiwa wa kashfa hiyo.

Ingawa timu hiyo haikutaja majina ya wahusika, miongoni mwa waliokuwa wanachunguzwa na Taasisi ya Makosa ya Jinai ya Uingereza (SFO), ni aliyekuwa Mwanasheria Mkuu wa Serikali wakati wa sakata hilo, Bw. Andrew Chenge, aliyekuwa Gavana wa Benki Kuu ya Tanzania (BoT), Dkt. Idris Rashid na mfanyabiashara Sailesh Vithlan.

Lakini baadaye jioni, akijibu hoja za wabunge kwenye kuhitimisha mjadala wa Bajeti ya Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma jana, Waziri wa Utawala Bora, Bw. Mathias Chikawe alimkingia kifua Bw. Chenge akisema Uingereza ilikwishamsafisha na hivyo hastahili kushtakiwa.

Mbali na wabunge hao kuitaka serikali kuchukua hatua za haraka kwa watuhumiwa hao zikiwemo za kuwafikisha mahakamani, pia wamelitaka bunge kutenga muda wa kujadili suala hilo ili wajue undani wake.

Akikabidhi taarifa ya safari hiyo kwa Spika wa Bunge, Bi. Anne Makinda jana, Bw. Ndugai alisema kuwa baada ya kamati hiyo kujadiliana na SFO, wameona bado kuna uwezekano wa kuchukua hatua zaidi kwa wahusika wote.

“Wakati tukiwa huko, moja ya changamoto ambayo tulikumbana nayo ni pale tulipohojiwa ni hatua gani tulizochukua kama nchi kuhusiana na suala hilo,” alisema Bw. Ndugai.

Alisema kuwa wao walijibu kwamba wamekwenda kwa nia ya kushinikiza kulipwa fedha zilizoamuriwa na Mahakama ya Uingereza kama chenji ya rada iliyouzwa kwa Tanzania kwa bei ya kuruka, kupitia serikalini badala ya asasi za kiraia za nchi hiyo, kwa kuwa ni za wananchi na wao ni wawakilishi wao, hivyo suala la kufungua kesi ni suala la serikali.

Makamu Mwenyekiti wa Kamati ya Ulinzi na Usalama ambaye pia alikuwa miongoni mwa timu hiyo, Bw. Mussa Zungu, alisema kuwa mafanikio yaliyopatikana katika ziara hiyo, ni pamoja na bunge la Uingereza na Serikali kutambua mchezo mchafu uliofanywa na Kampuni ya kuuza zana za kijeshi iliyouza rada hiyo, BAE Sustem, kwa kuiba na kuidhalilisha Tanzania kwa kutaka kulipa fedha hizo kupitia asasi za kiraia.

Hata hivyo alisema kuwa Julai 19 mwaka huu, timu hiyo imekaribishwa kwenye mjadala wa wazi ambao utakutanisha wadau mbalimbali wakiwemo SFO, BAE, Kamati ya Bunge ya Maendeleo ya Kimataifa, Wizara ya Sheria ya Uingereza kwa lengo la kuweka mambo wazi kuhusiana na kitendo kilichofanywa na BAE, pia hiyo itakuwa ni fursa kubwa kwa timu ya bunge la Tanzania kuhoji maswali mbalimbali kuhusiana na mchakato huo.

Timu hiyo inataka fedha hizo zilipwe kwa riba inayoendelea kupatikana kutokana na fedha hizo kuwa katika akaunti ya BAE ambako zimehifadhiwa.

Kutokana na hali hiyo, wameitaka serikali kushirikiana na bunge kuhakikisha fedha hizo zinarudi na kuwa endapo hazitarudi mpaka Septemba 2011 hatua zaidi zichukuliwe kwa kampuni ya BAE.

Bw. Musa Zungu alisema kuwa hata baada ya kukutana na wahusika wa kampuni ya BAE, bado wamebaki na msimamo wao kuwa fedha hizo si tozo bali ni msaada.

Aidha timu hiyo pia ilikutana na Mkurugenzi wa SFO ambaye aliomba radhi kwa Serikali ya Tanzania kutokana na kushindwa kuishirikisha katika kesi hiyo wakati ikiendeshwa.

Mara kadhaa, Chenge amekuwa akikana kuhusika kwa namna yoyote na ufisadi huo wa rada na mara ya mwisho alijitokeza hadharani na kutangaza usafi wake baada ya SFO kuitimisha kesi hiyo bila kutaja chochote juu yake.

Utetezi wa Chikawe

Waziri Chikawe jana aliweka msimamo kwa niaba ya serikali kuwa
haiko tayari kumchukulia hatua yoyote Bw. Chenge kwa tuhuma za ununuzi wa rada hiyo.

Ilisema kuwa haina ushahidi wowote dhidi ya Bw. Chenge kuhusiana na tuhuma zinazoelekezwa kwake hasa kwenye sakata la ununuzi wa Rada ambao unadaiwa ulighubikwa na rushwa.

Hata hivyo, Bw. Chikawe alisema kuwa kama kuna mbunge yoyote au mtu yoyote mwenye ushahidi dhidi ya Bw. Chenge autoe na serikali itafanyia kazi siku hiyo hiyo.

“Suala la Rada limezungumzwa sana na limepotoshwa kwa kiasi kikubwa, SFO kwa kushirikiana na TAKUKURU walifanya uchunguzi wa kashfa hiyo na kubaini kuwa kwa hapa Tanzania hakuna mtu hata mmoja aliyehusika bali waliobainika katika makosa hayo ni watuhumiwa watatu kutoka nchini Uingereza,” alisema Bw. Chikawe.

Alisema kuwa waliohusika na kashfa hiyo, ni Bw. Sailesh Vithlan ambaye alikuwa dalali wa rada hiyo, Meneja Biashara wa Kampuni ya BAE, Bw. Jonathan Calman na mwingine aliyetajwa kama Bw. Christopher.

“Tutafanya kama kanisani kuwa mwenye ushahidi alete na asipoleta  hatutakwenda mahakamani kwa kuwa hatuna ushahidi, mahakamani huwezi ukaenda mikono mitupu ni lazima uwe na ushahidi wa kutosha...Chenge hatuna ushahidi naye na hili suala sasa nadhani mngeliacha,” alisema Bw. Chikawe.

Msimamo wa Upinzani

Juzi, Kambi ya Upinzania ilipinga fedha za rada kulipwa kupitia serikalini kwa madai kuwa haiaminiki na hasa ikizingatiwa kuwa fedha hizo zilipotelea mikononi mwake.

Msemaji wa Kambi ya Upinzani, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma, Bi. Sazan Lyimo alisema, "Kambi ya upinzani tunaona kuwa bila watuhumiwa hao kuchukuliwa hatua, ni dhahiri kuwa taifa haliwezi kuwa na uhakika wa kuzilinda vizuri fedha hizo za rada pindi zikilipwa pamoja na fedha zingine za umma ambazo zinaendelea kupotea kwa kuwa umekuwa ni utamaduni wa serikali kutochukua hatua.

“Tunataka Bunge lako tukufu lijadili na liazimie kuanzishwa kwa akaunti ya muda ya fedha za rada, itakayosimamiwa kwa pamoja na wawakilishi wa Asasi zisizo za kiserikali za Tanzania, wawakilishi wa sekta binafsi na mwakilishi wa serikali na tunataka fedha hizi zilipwe haraka iwezekanavyo kupitia akaunti hiyo,” alisema Bi. Lyimo.

Kambi hiyo pia iliomba bunge lichukue wajibu wa kujadili na kuamua kipaumbele cha matumizi ya fedha hizo chini ya usimamizi wa akaunti hiyo kwa kuzingatia zaidi maslahi ya wengi kadri fedha hizo zitakavyoonekana kutosha.

Kuhusu kesi ya rada

Kashfa hiyo ya rada, ambayo ndiyo ilisababisha kujiuzulu kwa aliyewahi kuwa Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Bw. Chenge, iliibuliwa kwa mara ya kwanza na vyombo vya habari vya Uingereza na Tanzania, ambapo ilielezwa kuwa iliuzwa kwa bei ghali isivyo halali, huku kiasi kilichoongezwa kikitumika kama mlungula kuwahonga baadhi ya vigogo wa Tanzania waliokuwa wakihusika kupitisha mkataba wa ununuzi huo.

Tangu kuibuka kwa kashfa hiyo, imekuwa ikidaiwa kuwa 'mchezo' wa kuongeza bei ya rada hiyo kwa kiasi cha sh. bilioni 12, kisha kugawa mlungula huo kwa vigogo ambao ni wanasiasa na watendaji waandamizi serikalini, ilifanywa kwa ustadi mkubwa na dalali Mtanzania mwenye asili ya Kiasia aitwaye Sailesh Vithlan, ambaye tangu kuibuliwa kwa kashfa hiyo alipotea katika mazingira ya kutatanisha.

Akiwa wakala, Vithlan alifanikisha ununuzi wa rada hiyo, huku akituhumiwa kuishawishi Tanzania itoe sh. bilioni 16 zaidi ya bei halisi, ambapo inadaiwa tena kuwa alipewa sh. bilioni 12 kama bakishsi ya kufanikisha biashara hiyo. Ni kiasi hiyo alichopewa kama kamisheni ndiyo kilitumika kuwahonga vigogo serikalini.

Mbali ya Bw. Vithlani kuripotiwa kukimbilia nje, akitoroka nchini katika mazingira ya kutatanisha akiwa nje kwa dhamana baada ya kufunguliwa mashtaka.

Imewahi kuripotiwa mara kadhaa na vyombo vya habari kuwa BAE Systems imekiri kuwapo kwa malipo ya kamisheni kwa dalali wa biashara ya ununuzi wa rada hiyo.

Katika uchunguzi wao, SFO waligundua kuwa pesa hizo ziliingizwa katika benki moja huko Uswisi katika akaunti iliyokuwa ikimilikiwa na Bw. Vithlani. Baadaye Bw. Chenge alilazimika kujiuzulu mwaka 2008 baada ya wachunguzi kugundua zaidi ya Paundi za Uingereza 500,000 kuingizwa kwenye akaunti yake huko Jersey lakini alikana fedha hizo kutokana na BAE.

Mbali na Bw. Chenge pia vyombo mbalimbali vya habari viliripoti kuwa fedha nyingine zilihamishwa kutoka kwenye akaunti ya Bw. Chenge kwenda kwenye akaunti ya Dkt Rashid.

15 comments:

  1. HAPA NI UBABAISHAJI WATU WAMESHAMEGEWA DONGE WANAWEWESEKA,MAANA HATA UCHAWI ULISHIRIKISHWA KTK HAYA WKT CHENGE ALIPOBAMBWA AKIMWAGA UNGAUNGA BUNGENI LKN LIKAZIMWA KIAINA!!SASA LEO HIZO GHARAMA ZINAONGEZEKA ZA NINI? KUWATUMA WABUNGE KWENDA KUDAI,HIVI NINI KAZI ZA BALOZI ZA NJE?TUNAOMBA WATOE HESABU YA NAULI YA WABUNGE 4 NA SIKU WALIZOKAA NA POSHO WALIZOLIPANA JE, ZIMETOKA KTK FUNGU LIPI?
    NA HATA UPINZANI HAWAKUWASHIRIKISHA KIINI MACHO WAMEMCHUKUA JOHN CHOYO BILA HATA KUWASILIANA NA KAMBI RASMI KULIKONI?JAMAA HUYO MBUNGE WA BARIADI NDG CHONGO ANATISHA UKIMFATAFATA UTAKULA JIWE!!

    ReplyDelete
  2. Hivi wewe Mathiasi Chikawe kwa nini unamkingia kifua Andrea Chenge? Unatuudhi wapiga kura wako uchaguzi ujao tutakutosa bila huruma kwani na wewe ni mmojawapo wa mafisadi wanoitafuna nchi hii pasipo huruma

    ReplyDelete
  3. chenge tutamuazibu,mtakemsitake,hamtaki kumpeleka mahakamani,tutampiga na mawe.yule si mwizi kwa imani yetu anpondwa na mawe mpaka afe.tumechoka na huu ubabaishaji wa akina chikawe.nadhan ata uwazriri alipewa kwa sababu mkuu kaoa kwao

    ReplyDelete
  4. mimi binafsi sijajua na nikifikiria sipati jbu, inakuwaje huyu Chenge anayehusishwa na kashfa nyingi lkn serikali inamkingia kifua? au walikula pamoja? na hiyo CCM kwa nini inaendelea kumlea mtu ambae si safi? C huyo tu kwa ccm lkn wapo kibao na bado wanadunda. inshangaza sana.

    ReplyDelete
  5. Hii ni aibu, aibu kwa serikali na chama tawala.hata mkisimama na kujinadi kuwa uchumi unakua kwa asilimia 7 lkn zinazoingia mfukoni mwa kina chenge ni zaidi ya asilimia 7. ACHENI UHUNI.

    ReplyDelete
  6. chenge anafuata mfano wa jakaya, acheni nae ale

    ReplyDelete
  7. NYIE WACHANGIAJI WOTE HAMUELEWI KINACHOFANYIKA HAPA NA WAZIRI CHIKAWE, ANACHOKIFANYA HAPA SI KUMLINDA CHENGE HAPA ANACHOKIFANYA NI KUILINDA SERIKALI NZIMA AKIWEMO ALIYEKUWA RAIS WA TATU BW.MKAPA
    KWA MAANA UKISEMA UANZE NA CHENGE ITABIDI UMFUATE YULE MUHINDI VITHLANI NA UKISEMA UMFUATE VITHLANI NDIO MAANA YAKE UMEMFUATA MKAPA NA KUNDI LAKE MAANA KAMA MNAKUMBUKA ZILE DOLA MIL.12 ALIZOCHUKUA VITHLANI KAMA KAMISHENI YAKE NYINGINE ALIZIKATA AKAZITUMA USWISS KWENYE ACCOUNT ZA VIGOGO NDIO HAO WANAOJARIBU KULINDWA MAANA YULE MUHINDI HATOKUBALI KUFA PEKE YAKE.

    ReplyDelete
  8. ENZI ZA MKAPA KILA KASHFA IKITOKA ALIKUWA ANAGEUKA MBOGO ALIYEJERUHIWA MATAKONI.TUNAOMBA VYOMBO VYA HABARI MUWE MNATUNZA KUMBUKUMBU YA CHECHE ILI SIKU TUNAPOPATA USHAHIDI KAMA HIVI WAWEZE KUTUJIBU KWA NINI WALISIMAMIA UOZO.TUKIANZA NA CHIKAWE AT THE END OF THE DAY ATATWAMBIA SABABU YA HUO UTUMBO ANAOWAWAKILISHIA WATANZANIA.NI KASHFA KUBWA SANA SERIKALI KUWA NA MCHEZO MCHAFU HAITAKUWA NA SAUTI,HEBU SUBIRINI SERIKALI ZINAZOJIJENGEA HESHIMA KAMA UINGEREZA MUONE WATAKAVYOWAANDAMISHA HAO BAE PINDI ITAKAPOKUWA HADHARANI.

    ReplyDelete
  9. Nyie viongozi wa Tanzania mnatia aibu sana kwa mambo ya kijinga mnayo fanya pamoja na wizi wenu ndio maana hata hao wawekezaji wanawazarau.Hebu tujiulize kwanza zile fedha za huyo mbunge mwizi wa bariadi alizo weka kule katika kisiwa cha jearsey alizipata wapi? na kwa biashara gani anayo fanya?,Au anauza unga?.Na wewe Chikawe inaonekana ni mmoja kati ya watu waliopata hili fungu.Hizo fedha kwenye account ya chenge ni ushaidi tosha pamoja na BAE kukubali ya kuwa kulikuwa na rushwa ndani ya huo mkataba lakini cha ajabu wewe bado unazidi kumtetea huyo mwizi.

    ReplyDelete
  10. Tuseme hivi kwa hao wanao kana kwamba Chenge hakuhusika kuwa, ukimuuliza huyo Chikawe au Hosea wa TAKUKURU hizo dola 500,000 zilizoingia kwenye akaunti ya Chenge 2008 zimetoka wapi? Ni muda gani ziliingizwa kulinganishwa na kipindi cha hiyo tenda ya rada? Kwa nini Dr. Rashid alikatiwa kiasi cha fedha kutoka kwenye akaunti ya Chenge, kwa mahusiano gani? Haya maswali lazima wayatolee majibu yaliyo makini na siyo kutupa hoja za kipuuzi zilizo rahisi rahisi. Kama wao akili zao ni rahisi rahisi wasifikiri watanzania wote wako kama wao. Haiwezekani kabisa kwa mtu mwenye akili hata ndogo tu kudai kwamba rushwa alipokea Vithlani tu peke yake halafu akatulia na hizo hela. Je, wameshindwa kufuatilia akaunti ya huyu mhindi? Au wanatufanyia danganya toto? Mambo ya Vithlani ni kama yale ya Balali, kuna hila za kumficha kupoteza ushahidi na kitendo cha serikali kudai kwamba Chenge hakuhusika wakati Vithlani hajakamatwa na kuhojiwa inaonyesha serikali inajua kabisa kilichoendelea. Ukweli ni kwamba, mindhali Vithlani yuko porini, bado hawa wezi wataendelea kusafishana na kujidai wako safi. Waache tu, iko siku watatutolea majibu ya yote haya mbele ya sheria. One day must. Huwezi kuendelea kuwadanganya watu wote siku zote.

    ReplyDelete
  11. Very simple question,hizo hela alizowekewa Chenge kwenye akaunt zilitokana na biashara gani ya nje aliyofanya?Je aliuza nini hadi alipwe mapato yote hayo,aliliap TRA na VAT katika biashar hiyo?Je Balai alikuwa na share kwenye huo mzigo waliouza uingereza au alikuwa business share holder? kama sio ilo donge alilommegea alikuwa anamlipa kwa service gani aliyomfanyia? je hivyo vijisent alipata wapi au aliuza ng'ombe wote wa Bariadi huo Uingereza.Akishindwa kujibu hayo maswali basi awe condemned to death.

    ReplyDelete
  12. Mnatuambia siku zote waislam tuende shule hatuna akili. nyie wakiristo ndio hicho mlichosomea? tuacheni na ujinga wetu na moto mnaouona hapahapa duniani. NCHI INAFILISIWA NA WAKIRISTO HII. MAPADRI NA MAASKOFU MKO WAPI? HAWA WATU WENU NDIO WALIOTUFIKISHA HAPA TULIPO NA MKANYAMAZA KIMYA,ALIPOINGIA KIKWETE TU KWA SABABU YA DINI YAKE BASI MKAANZA KUMSAKAMA. YATAWASHINDA NI AIBU HII,TIMU NZIMA HIYO YA UFISADI HUU UNAWEZA KUKUTA MUISLAM MMOJA AU WAWILI WENGINE WOTE NDIO HAOHAO.

    ReplyDelete
  13. Wewe idiot unayeleta Udini hapa sipo, havina uhusiano vitu hivyo viwili! Tafuta hoja nyingine upenyeze udini wako! (pointless)

    Salam kwa Chenge
    Mjomba hizo pesa zitaku-cost mjomba! chagua moja, sacrifice au toa sadaka yaishe!

    ReplyDelete
  14. Nawaomba Waislamu wote tufike mahali tuangalie maendeleo ya nchi yetu, tusidanganywe na maswala ya dini. mwizi ni mwizi tu awe mristu, mpagani au muislamu. Ukisema Wakristu ndo wezi mimi nitakuambia mwizi mkuu ni Kikwete ambaye ni muislam. kama si mwizi kwa nini anawalea hawa wazi akina Chenge?

    Tusidanganywe na Udini, wezi lazima wakamatwe hata wawe dini gani.

    Hivi hawa wabunge wezi mbona kwao wanapigiwa kura? Hivi hakuna watu wengine wanaoweza kuwa wabunge wasiokuwa wezi?

    Walaaniwe watu wote wanao mtete Chenge, Rostam na Lowasa.

    ReplyDelete
  15. serikali ya kifisadi haiwezi kuchukua hatua kwan inawezekana nao walipata mgao wao,mbona wanateteana!

    ReplyDelete