*APR yakiona chamoto Morogoro
Na Zahoro Mlanzi
MABINGWA wa Tanzania Bara, Yanga jana ilipata ushindi wa mbinde katika mechi ya Kagame Castle Cup iliyopigwa Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam dhidi ya
Elman ya Somalia.
Katika mehi hiyo iliyopigwa saa 10 jioni, ambayo mashabiki walijua ingekuwa na mabao mengi kutokana na Elman kutopewa nafasi, Yanga ilianza kwa uchu wa mabao ambapo dakika ya kumi, Julius Mrope aliachia shuti kali lililopanguliwa na kipa Kamal Omari.
Yanga ililiandama tena lango la Elman dakika ya 15 kwa pasi fupifupi ambapo Mrope tena, alipiga krosi safi iliyokosa mmaliziaji.
Dakika ya 27 Yanga, iliandika bao la kwanza kupitia kwa Davies Mwape kwa kichwa, baada ya kuunganisha krosi ya Godfrey Taita, aliyepokea pasi ndefu ya Rashid Gumbo.
Baada ya kushambuliwa kwa muda mrefu Elman, ilipata nafasi nzuri dakika ya 44 baada ya mabeki wa Yanga, kumwachia Mohamed Nur wakidhani ameotea lakini shuti lililopaa juu ya lango.
Kipindi cha pili kilianza kwa Yanga kuhamia langoni mwa Elman ambapo dakika ya 48, Mwape alipiga shuti lililopanguliwa na kipa Omari.
Yanga ilikuja juu tena dakika ya 56, Kigi Makasy aliachia shuti lililomlenga na kipa Omari na mpira kuangukia katika miguu ya Keneth Asamoah, aliyeshindwa kutumbukiza mpira kimiani akiwa katika nafasi nzuri ya kufunga.
Baada ya mashambulizi hayo, Yanga ilionekana kutoelewana kwani pasi nyingi walizopigiana ziliishia miguu mwa Elman na kufanya timu hiyo kuzinduka kwani walipata sapoti ya kushangiliwa kutoka kwa mashabiki wa Simba waliokuwepo uwanjani hapo.
Kupoteana kwa Yanga kulifanya mashabiki wao wamzomee Kocha Mkuu wa timu hiyo, Sam Timbe kwa kumtaka afanye mabadiliko katika nafasi zilizoonekana kupwaya.
Kocha huyo alifanya badiliko kwa kumtoa Mwape na kuingia Hamis Kiiza ambaye alibadili mchezo na dakika 90 aliifungia timu yake bao la ushindi kwa kichwa akiunganisha krosi ya Taita.
Kwa matokeo hayo Yanga sasa imefikisha pointi nne sawa na Bunamwaya, inayoongoza Kundi hilo la B, isipokuwa zimetofautiana mabao ya kufunga na kufungwa.
El Mereikh inakamata nafasi ya tatu kwa kuwa na pointi mbili huku Elman ikishika mkia ikiwa haina pointi.
Katika mechi iliyochezwa saa 8 mchana ya kundi hilo katika uwanja huo, timu za El Mereikh na Bunamwaya zilitoka sare ya bao 1-1.
Nayo St. George jana ilitakata katika Uwanja wa Jamhuri Morogoro, baada ya kuwafunga mabingwa watetezi wa michuano hiyo APR mabao 3-1.
Mchezo mwingine uliopigwa uwanja huohuo, Ulinzi ya Kenya iliishushia mvua ya mabao 9-0 Port FC ya Djibouti.
No comments:
Post a Comment