01 July 2011

Basena akacha waandishi U/Taifa

Na Elizabeth Mayemba

KOCHA Mkuu wa Simba, Moses Basena juzi alikacha kuzungumza na waandishi wa habari mara baada ya mchezo wa michuano ya Kagame Castle Cup dhidi ya
Zanzibar Ocean View kumalizika, ambapo timu hiyo ilishinda bao 1-0. Mchezo huo ulichezwa Uwanja wa Taifa,Dar es Salaam.

Kama ilivyo kawaida, mchezo husika unapomalizika makocha wa timu zote mbili hufanya mahojiano na waandishi wa habari, lakini Basena juzi baada ya kufuatwa na Msemaji wa Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF), Boniface Wambura kumtaka afanye hivyo aligoma na hivyo msaidizi wake, Amatre Richard akalazimika kuzungumza.

Akizungumzia mchezo huo, Amatre alisema timu yake imeanza rasmi mashindano hayo baada ya kutoka kidedea na kwamba ushindi wa bao 1-0 hauna tofauti na ule wa mabao 10.

"Kwa matokeo ya leo (juzi), tumejiweka katika nafasi nzuri ya kucheza robo fainali, lakini bado kuna kazi ya kurekebisha makosa kwa wachezaji kwa kuwa wamekosa nafasi nyingi za wazi," alisema Amatre.

Alisema wamejipanga kushinda kila mchezo watakaocheza na lengo lao ni kufika fainali katika michuano hiyo.

Kwa upande wake Kocha Mkuu wa Ocean View, Abdul Abbas alilalamikia maamuzi kwa madai kwamba yalilenga kuwabeba Simba, hivyo waamuzi waliidhoofisha timu yake.

"Kilio changu ni kwa waamuzi wameionea sana timu yangu na kuipendelea Simba, kama hali itaendelea hivi waamuzi watatuweka katika mazingira magumu sana," alisema Abbas.

No comments:

Post a Comment